JE HAYA NI MAPENZI!! 95: - UHONDO KITANDANI

Hot

Post Top Ad

https://play.google.com/store/apps/details?id=chumba.cha.wakubwa

Thursday, February 20, 2020

JE HAYA NI MAPENZI!! 95:





Neema akaanza kuropoka kamavile mtu
aliyechanganyikiwa,
"Yule mwanaume, mwanaume yule anaota miba.
Yule mwanaume ana misumali, yule mwanaume
anatoa usaha, yule mwanaume ana........."
Neema akaanza kuweweseka sasa na kugeuza
geuza macho.
Aisha uoga ukamjaa na kujikuta akianza kupiga kelele ila wakati anapiga kelele alimuona Neema akiwa kimya kabisa, hofu ikazidi kumtawala Aisha kwani hakujua cha kufanya.
Akaamua kutoka nje ili kwenda kutafuta msaada, kwa bahati akakutana na Sam akiwa nae anaenda hapo kwa Neema na ndiye aliyemuuliza Aisha kuwa kulikoni.
Aisha akamueleza kuhusu kuweweseka kwa Neema.
"Kwani kuna kitu kakwambia?"
"Kitu gani? Ameanza gafla tu"
Sam akagundua kuwa pale Aisha hajui chochote kile kisha akaingia nae ndani ili na yeye apate kumuangalia Neema.

Aisha akashtuka kumuona Neema amekaa wakati alimuona akiweweseka chini na kuwa kimya kabisa.
Sam hakushtuka kwavile hakujua hali halisi ilivyo, ila tu alikuwa anamshangaa Aisha kwa kushtuka vile.
Kisha Aisha akamuuliza Neema kwa sauti iliyojaa uoga,
"Kumbe mzima dada?"
"Kheee ulijua nimekufa?"
Neema alipojibu, Aisha akamsogelea karibu sasa kwani ilikuwa rahisi kugundua kuwa Neema ni mzima kweli.
Alisogea karibu zaidi na kumpa pole, ambapo Neema alicheka na kuweka kama utani,
"Duh Israel kanibeep ila sijapiga"
Huku akicheka kanakwamba tukio lililotokea ni la kawaida kabisa.
Kitu hicho ndio kilichozidi kumshangaza zaidi Aisha.
Sam naye alikaa akiwaangalia sasa, Neema naye alimuangalia Sam na kumwambia kwa hasira
"Nini kimekuleta Sam?"
"Nimekuja kukuona Neema"
"Nenda kapatane na mkeo kwanza ndio uje"
"Napatana nae vipi na hana kumbukumbu zozote?"
Neema akajisikia vibaya kwani yeye ndio chanzo cha yote yaliyompata mke wa Sam ila hakuweza kujieleza kwani alijua wazi kuwa akijieleza basi itakuwa ngumu kwa Sam kuja kumuona mara kwa mara kwani atajua kama ni mtu aliyejitakia yale yaliyompata.
"Ila jaribu kuwa nae karibu basi"
"Najitahidi ila kwao hawataki hata kuniona kutokana na yale yaliyotokea"
Neema akafikiria kitu ila kutokana na hali yake akaona   ni wazi atashindwa kulitenda lile analolifikiria.
Akamfikiria rafiki yake Rose ambaye ndio alikuwa msiri wake na kuona wazi kuwa yeye ndio angeweza kufanya lile analofikiria yeye ila aliamua kumwambia Sam aende tu kwani roho yake ilikuwa ikimuuma sana kwa kuendelea kumuona Sam mahali hapo.
Hivyo Sam akaacha kiasi cha pesa cha kuwasaidia na kuondoka.

Neema alibaki na Aisha sasa ambapo Aisha alikuwa bado akimshangaa Neema kwani tukio lililotokea kabla lilikuwa la kustaajabisha mno.
"Mbona unanishangaa sana Aisha, yani tangu umeingia hapa na Sam unanishangaa tu"
Aisha aliamua kumueleza Neema jinsi ilivyokuwa na hadi pale,
"Kiukweli niliwaza mambo mengine kabisa, kwakifupi nilichanganyikiwa dada. Yani nilichanganyikiwa sana."
Neema akafikiria kwa dakika kadhaa na kujua wazi kuwa kilichomfanya apone ni kitendo cha Sam kwenda pale kwake ambapo imekuwa jambo jema kwake na la uzima ila kupona kwake yeye kwa   staili hiyo ni kuendelea kumtesa Sabrina, ni kumfanya Sabrina aendelee kuteseka na kupata ugumu zaidi.
Akakumbuka dawa, ya kuwa kuna dawa moja hajaiondoa.
Ni dawa hiyo hiyo aliyoiwaza hata wakati Sam yupo ila je anawezaje kuiondoa.
Ndio hapo alipomkumbuka Rose kwani ndio aliyekuwa anajua mipango yote kwavile walikuwa wakipanga pamoja.
Neema hakuweza kwenda kuitoa hiyo dawa ila anamuagizaje Aisha kwenda kutoa dawa hiyo? Hapo ni lazima Aisha ajue siri yake na hapo ndio pagumu kwake.

Sabrina naye siku hiyo alijihisi maumivu makali ya shingo kanakwamba alikandamizwa na majinamizi usiku.
"Mwanangu sasa hapo hali ni mbaya, yani wewe ukiacha hili unaanza kuumwa lile, tufanyaje hapa jamani"
"Sijui mama"
"Ila usijali, Mungu atakusaidia. Utapona tu mwanangu"
Wakapeana imani na mama yake.

Muda kidogo siku hiyo alifika shangazi wa Sabrina ambaye ilikuwa ni siku nyingi sana bila kuwatembelea ndugu zake hao kutokana na yale mambo yaliyotokea baina yao, na kilichompeleka pale ni kwa lengo la kumsalimia Sabrina kwani alikuwa amesikia habari za kuumwa na kila kitu ila hakwenda kuwaona.
Alipofika pale alijua mama wa Sabrina hatompokea vizuri ila alipoingia mama Sabrina ndiye aliyekuwa wa kwanza kuinuka na kumpokea kwa furaha huku akifurahia sana kufika kwake.
Shangazi wa Sabrina akafurahi kukaribishwa vile na kuwafanya wazungumze mambo mengi sana bila kugusia ule ugomvi wao kwani mama Sabrina aliamini kuwa hakuna tena cha kugombana na wifi yake huyu.

Shangazi wa Sabrina alimuhurumia sana Sabrina kwa kile kitendo cha kupoteza kumbukumbu zake kwani hata shangazi yake hakumkumbuka.
"Pole sana Sabrina ila Mungu ni mwema utapona kabisa tu."
Sabrina akatabasamu tu ila akamshangaa huyu shangazi yake kuwa na maneno mengi kiasi kile kwani alikuwa anaongea tu.
"Yani nilikuwa naota ndoto mbaya mbaya kuhusu Sabrina na kunifanya    niingie kwenye maombi kwaajili yake naona naye ilibaki kidogo kupatwa na majanga. Watu ni washirikina jamani"
Wakazungumza pale namna ya kuweza kumsaidia Sabrina kutoka kwenye yale matatizo.
Mpaka jioni shangazi wa Sabrina alipoondoka bado hawakujua cha kufanya katika kumsaidia Sabrina kurudisha kumbukumbu zake.

Bado Sam alikuwa na matumaini ya kwamba Sabrina anaweza kusaidiwa na Jeff juu ya kurudisha kumbukumbu zake ila alipoona siku zinaenda bila ya Jeff kumpa jibu linaloeleweka alionekana kukata tamaa juu ya hilo na kuruhusu mawasiliano kati ya yeye na Sia kupamba moto kwani Sia hakuchoka kumtafuta Sam na lengo kubwa ni kuwa nae karibu kama wapenzi.

Neema hakuwa na wa kumsaidia katika kuitoa dawa mahali alipoweka na kuamua kujitoa ufahamu kwa kumuomba Aisha amsaidie swala lake la kwenda kuitoa ile dawa.
Ingawa aibu ilimjaa ila hakuwa na jinsi zaidi ya kumwambia Aisha kwenda kuitoa ile dawa.
  "Naomba unisaidie mdogo wangu tafadhari, nakuomba sana nisaidie"
Aisha alikuwa akimuangalia tu Neema huku akimuhurumia na kumshangaa pia.
Neema akamueleza Aisha mahali alipoweka hiyo dawa.
"Kwahiyo dada uliweka hiyo dawa kwa madhumuni yapi?"
"Acha tu mdogo wangu, nilimpenda Sam na alikuwa mume wa mtu kwahiyo nikaenda kuchukua dawa kwa mganga na hapo ninapokuelekeza ni mahali ambapo niliweka dawa moja wapo ya kumvutia. Ila dawa ile ilikuwa ikimdhuru huyo mke wa Sam"
Aisha akashangaa sana,
"Kwahiyo mimi haiwezi kunidhuru?"
"Haiwezi kukudhuru wewe, hata hivyo kumbuka kuwa dawa ile ilikuwa na dawa zingine huku nyumbani ambapo kuna siku uliona nachoma choma moto kwahiyo lazima imezidiwa nguvu na haiwezi kufanya chochote. Nisaidie kuitoa, nataka hata kama nikifa basi nife kwa amani"
"Amini utapona dada"
Neema akatabasamu tu, kwani ukweli wa mambo aliujua kuwa hawezi kupona kabisa, na alimshukuru Aisha kwa moyo aliokuwa nao, kwani ilikuwa si rahisi kwa mtu kuendelea kuvumilia ile harufu iliyokuwa ikitoka kwenye mwili wake.
Kwahiyo kwake Aisha alikuwa ni mtu muhimu na wa kipekee sana.
Huku Aisha naye akiwaza mambo mengi bila ya majibu yoyote yale ingawa alikubali kile alichotumwa na Neema na kuahidi kukitelekeza.

Jeff naye alifikiria sana jinsi ya yeye kuweza kumsaidia Sabrina, na alijua wazi kuwa ni lazima akimsomea ile barua Sabrina ataelewa tu.
Muda huo akaamua kutoka pale kwao na kumuaga mama yake kuwa anaenda kwakina Sabrina ambapo mama yake akamwambia,
"Ila Jeff mwanangu, mficha maradhi kifo humuumbua"
"Jamani mama, kwani mi nimeficha kitu gani?"
"Unajua mwenyewe unachonificha ila ipo siku nitajua tu ingawa inakuwa ngumu kwa mimi kuamini hili"
Jeff akamuangalia mama yake na kuhisi kuwa kuna kitu mama yake ameanza kukihisi juu yake, ingawa kwa binafsi yake haoni tatizo kwa mama yake kutambua hilo ila tu anahofia kwa upande wa Sabrina ambaye hakutaka ijulikane sehemu yoyote ile.
Basi Sam akaondoka pale kwao na kuelekea kwakina Sabrina.

Sam alikuwa nyumbani kwake huku akiwa na mawazo sana na kumngoja mgeni ambaye ametoka kuongea nae kwenye simu, huku yeye akiendelea taratibu kunywa vinywaji vyake vyenye kilevi huku akiamini kuwa ndio vitakavyomsaidia kupunguza mawazo au kuyaondoa kabisa.
Muda kidogo aliwasili mgeni wake ambaye alikuwa ni Sia.
Sam alitabasamu kumuona na kumkaribisha.
"Nashukuru umekuja Sia, sikujua kama ungekuja tena toka siku ile kwani ilionyesha umechukizwa sana. Ingawa tulikuwa tukiwasiliana ila sikujua kama ungekuja. Nisamehe sana"
"Usijali Sam, ila hujaniambia hadi leo. Vipi yule mtu alikusaidia?"
"Anisaidie wapi? Hadi leo kimya. Yule naye mzushi tu, alifanya nikuondoe wewe huku nikiamini kuwa atakuwa na msaada kwangu ila hadi leo hajanijibu chochote yani"
"Pole, ila hutakiwi kuwa na mawazo kiasi hicho. Naomba uniangalie mimi na kunisikiliza, nakuhakikishia kwa kupitia mimi utasahau kila kitu."
Sam akatabasamu pale na kuanza kumuangalia Sia sasa.

Jeff akafika nyumbani kwakina Sabrina na kumkuta akiwa ametulia na mama yake kwani watoto walikuwa wamelala.
Jeff akawasalimia kisha kumuomba Sabrina,
"Naomba twende mahali, kuna kitu nataka kukuonyesha"
"Mmh wapi huko?"
Mama Sabrina aliuliza kwa mshangao,
"Sio sehemu mbaya bibi, na wala hatutachelewa"
"Ila si unajua kama hana kumbukumbu"
"Natambua vizuri bibi, ila nitakuwa nae makini kupita maelezo ya kawaida na kama una kikitokea chochote kibaya basi iwe mimi wa kulaumiwa"
Mama Sabrina akamuangalia Jeff na kukubali ila Sabrina alikuwa kimya kabisa kanakwamba anayezungumziwa pale si yeye.
Mama Sabrina akamtazama Sabrina na kumwambia,
"Hivi haya tunayozungumza hapa unayaelewa kweli?"
"Nawaelewa ndio"
Sabrina akainuka na kumwangalia Jeff  kisha akamwambia,
"Ndio tunaenda au?"
Jeff hakutaka kusita kwani alijua wazi kuwa iwapo Sabrina akibadili maamuzi basi itakuwa ni ngumu sana kuendelea kumshawishi kwenda, kwahiyo alipokubali tu akatoka naye.

Jeff aliita gari ya kukodi kisha safari ya yeye na Sabrina kuanza kuelekea kwenye ile hoteli aliyoenda mara ya mwisho na Sabrina kabla ya yeye kwenda nje kusoma.
Walipofika hotelini wakashuka na kumfanya Sabrina amuulize Jeff kwa mshangao,
"Mbona umenileta hotelini?"
"Nimekuleta si kwa nia mbaya ila kwa lengo la kukuonyesha kitu na kuangalia kama unaweza kurudiwa na kumbukumbu zako"
Jeff akamuomba Sabrina kuwa waingie ndani ila Sabrina alionekana kusita kwa hilo mpaka pale Jeff alipombembeleza na kumuhakikishia kuwa hawezi kufanya chochote kibaya.

Waliingia ndani kwenye chumba ambacho Jeff alikodi.
Kisha akamuomba Sabrina akae kwenye kochi na yeye kukaa kitandani, halafu akatoa ile barua ili   amsomee.
"Tafadhari nisikilize kwa makini ninapoisoma hii barua na wala sina nia yoyote zaidi ya kusoma hii barua"
Sabrina alitulia na kumsikiliza Jeff ambaye alianza kuisoma ile barua sasa,
"Ni usiku sana nimeamka na kuandika haya. Kwako Jeff mpenzi, najua utashtuka sana baada ya mimi kukuita mpenzi hapo juu, yote hiyo imetokana na swala moja tu nalo ni upendo unaonipatia. Umekuwa mstari wa mbele katika kunipenda mimi, ni mara nyingi sana nimekuwa nikikukatisha tamaa kwa kukufokea hata kukufukuza lakini wewe umekuwa mwanaume mvumilivu kwangu.
Kesho unasafiri Jeff ndiomana nimeamua niandike haya maana hatujui mambo yajayo, jua kwamba nakupenda sana tena sana. Kitu kinachonizuia kuwa na wewe ni aibu, aibu ya umri, aibu ya mazoea.
Jeff wewe umekuwa kama mtoto kwangu, ni nani anayeweza kukubali mahusiano ya mimi na wewe? Ni nani atakayeweza kututazama mara mbili katika familia zetu? Jibu ni hakuna, ila   moyo wangu na wako ndio unaojua ni jinsi gani tunapendana. Napenda iwe siri ingawa watu husema kuwa penzi ni kikohozi kulificha huwezi.
Napenda kukiri jambo hili kwako, hakuna mapenzi niliyowahi kuyafurahia kama yako. Pia napenda ujue kuwa wewe ni mwanaume wa pekee uliyefanikiwa kuwa na mimi kimwili, najua utakuwa unajiuliza kuhusu Sam ila siri ya Sam ninayo mimi. Napenda kukwambia kwamba.........."
Jeff akakwamia hapo kwani aliona kimya kimetanda, akamtazama Sabrina pale kwenye kochi alipokaa, akamuona amefunga macho huku kichwa chake kikiangalia juu ila alikuwa akitokwa na machozi mfululizo.
Jeff akainuka na kumfata pale kwenye kiti, Sabrina alionekana kuwa na maumivu ya moyo kwani alikuwa akilia kwa uchungu.
Jeff alipojaribu kumbembeleza, Sabrina alimtazama Jeff na kumzaba kibao cha nguvu.

Itaendelea



No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

https://play.google.com/store/apps/details?id=chumba.cha.wakubwa