Jeff akakwamia hapo na kushtuka kwani mlango ulifunguliwa na aliyeingia alikuwa ni Sakina.
Alimuangalia mwanae na kusimama pale mlangoni kama kwa dakika mbili hivi kisha akamwambia,
"Endelea nami nikusikilize"
Jeff akamtazama mama yake na kuona aibu kisha akaikunja ile barua na kuirudishia mfukoni.
"Vipi Jeff? Au mi sipaswi kusikia unachotaka kusoma? Mbona umeifunga hiyo barua? Endelea nami nisikie."
Jeff akaona aibu kwa mama yake na kuamua kujichekesha kidogo huku akijitetea kama ishara ya kuondoa aibu aliyokuwa nayo.
"Sio barua hii mama"
"Ila ni nini?"
"Ni kama stori tu nilikuwa nataka kumsimulia mamdogo"
Sakina akasogea na kumsalimia Sabrina kisha akakaa na kumwambia mwanae,
"Haya simulia na mimi napenda nisikie hiyo stori"
Jeff akacheka tu kisha akainuka na kumuaga Sabrina halafu akamwambia mama yake,
"Utanikuta nyumbani mama"
Sakina alitamani hata kumfokea au kumkaripia mwanae ila atamfanyiaje hivyo wakati sasa ni mtu mzima tayari, ikabidi amuangalie tu hadi alipotoka nje kabisa.
Sakina akamtazama Sabrina sasa,
"Kwani alikuwa anakwambia vitu gani huyu?"
"Sijui, ila nimemshangaa tu hata mimi"
Sakina akamtazama sana Sabrina kisha akamchukua mtoto wa Sabrina na kumshika kidogo huku akitabasamu bila ya kusema chochote.
Akakumbuka udogo wa Jeff, mtoto huyu ndio alizidi kufanana na Jeff, aliiona sura ya Jeff kabisa kwa mtoto huyu.
Akajikuta chozi likimtoka kwani kuna kitu kilimuumiza moyo.
Sabrina hakumuelewa Sakina na kumuuliza,
"Kwani vipi dada? Mbona unamuangalia mtoto huku unatabasamu halafu chozi linakutoka?"
"Aah nakumbuka udogo wa mwanangu, mtoto huyu ni mzuri sana"
Kisha akamrudisha mtoto kwa Sabrina na kuaga na kurudi nyumbani kwake.
Sakina alirudi nyumbani kwake na kumkuta Jeff kweli nyumbani ila alikuwa katika harakati za kujiandaa kutoka.
"Mmh! Unaenda wapi mwanangu?"
"Naenda kwakina Dorry"
"Mmh kufanya nini tena ikiwa ulikataa kuwa mtoto si wako?"
"Na si wangu kweli ila kuna kitu nataka nikafanye"
"Mmh kitu gani mwanangu?"
"Nitakuja kukwambia nikirudi"
"Kuwa makini tafadhari, usiniletee majanga"
Jeff akatoka na kuondoka huku mama yake akiwa na mawazo mfululizo haswa kuhusu Sabrina na kujikuta akiongea mwenyewe,
"Ila kwanini wananificha? Hivi inawezekana kweli? Sabrina kaolewa, iweje sasa watoto wale jamani mbona wanafanana na Jeff? Hivi Sabrina kama Sabrina anaweza kutembea na Jeff kweli mtoto wa kumlea mwenyewe?"
Hilo swala halikumuingia akilini kabisa Sakina na wala hakuweza kuelewa na kufanya kichwa chake kiwaze bila kuwa na muafaka wa mawazo.
Jeff mpango wake kwa Sabrina aliona umekwamishwa na mama yake ila bado alijua kuwa anayo nafasi ya kumfanya Sabrina arudi katika hali yake ya kawaida ila kwasasa aliamua kumuacha kwanza ili apate japo nguvu.
Na ndipo alipoamua kwenda kwakina Dorry tena bila hata ya kumpa taarifa kuwa anaenda.
Alifanya vile ili Dorry asikimbie kwa uoga wa makosa yake.
Dorry alikuwa nyumbani kwao, kwa yule mama yake ambaye alipata ajali.
Akashangaa kuambiwa kuwa kuna mgeni wake amekuja, ambapo mgeni huyo alikaribishwa moja kwa moja ndani.
Dorry alijikuta akiona aibu baada ya kumuona Jeff ndiye mgeni wake.
Ila Jeff alikuwa kawaida tu na kumsalimia Dorry aliyekuwa kampakata mwanae.
Jeff alikaa pale sebleni kwakina Dorry,
"Hebu na mie nimshike kidogo mtoto niweke baraka"
Dorry akampa Jeff mtoto kwa aibu, Jeff alimuangalia mtoto huku akitabasamu, kisha akamuangalia Dorry na kumwambia
"Kweli Dorry hapa ulipaniki jamani, mtoto wa kichina kabisa huyu ndio useme ni wangu?"
Dorry aliinama chini,
"Nisamehe Jeff"
"Nilishakusamehe ndiomana umeniona hapa kwenu. Na hata usiwe na shaka, Sam kashanieleza kila kitu"
Dorry akaona aibu zaidi na kuona kuwa Sam ni msaliti kwani hakutegemea kama angeweza kusema ukweli wa mambo kiasi kile.
"Ila haikuwa lengo langu kukudanganya Jeff, tafadhari nisamehe sana, sikuwa na nia ya kukudanganya. Badae niligundua kosa langu na ndiomana nikaandika barua ya kuomba msamaha Jeff"
"Natambua hilo, ila siku ile ungefanikiwa kulala na mimi ndio ungenisingizia kabisa bila chenga. Ila hata kama ungenisingizia, kwa muonekano huu wa mtoto lazima ningekataa tu na hata nisingekuwa na haja ya kupima D.N.A yani hapa najua wazi uliteleza kwa wale wachina waliokuwa wanajenga ile hoteli kule Bagamoyo"
Dorry alikuwa akiona aibu tu,
"Shida ndio iliyonifanya hivi, sikuwa na lengo la kuwa na mchina ila ni shida tu"
"Pole sana, ila siku nyingine ukitaka kumsingizia mwanaume mtoto angalia na wanaume uliotembea nao kama wanarandana. Kweli kabisa mswahili na mchina wapi na wapi? Wachina wanadamu kali sana, na uelewe wazi kuwa huyo ni mwanao peke yako sababu wale hawapeleki watoto wa nje kwao"
"Nimefanya makosa Jeff, nisamehe tu maana hapa moyo wangu unanisuta hadi basi"
Kisha Dorry akaamua kumpongeza Jeff kwa ujasiri alionao, akampongeza kwa uwezo alionao wa kukwepa vishawishi.
"Kwakweli mke wako atakuwa ni mwanamke mwenye bahati sana, kwani hata mimi ningependa kuipata bahati kama hiyo"
"Asante, namshukuru Mungu kwa hili kwani nimejikuta nikiwa na moyo wa kuridhika kwa niliye naye."
"Hongera sana, natumaini siku moja nami Mungu atanipa mume mwema kama wewe"
"Ila kumbuka kuwa Mungu atakupa mtu wa kufanana nawe, kwahiyo kama wewe utakuwa mwema basi utapewa mwema mwenzio ila sio wewe uwe mwovu na utegemee kupewa mwema. Na ukiona imetokea hivyo basi ujue Mungu analengo la kukufanya ubadilike ila ukishindikana lazima Mungu amtoe yule Mwema kwako na kumpatia mwema mwenzio kisha wewe kurudishiwa mwovu mwenzio wa kufanana nawe"
"Jamani Jeff, maneno makali hayo"
"Ila yana ukweli ndani yake, cha msingi jiangalie vizuri"
Wakazungumza mengi sana kisha Jeff akaaga kwaajili ya kuondoka, naye Dorry akamuacha mwanae pale kwao na kuamua kumsindikiza Jeff.
Dorry aliamua kumsindikiza kwani aliamini kuwa kuna mengi bado hajaongea na Jeff.
Na wakiwa njiani akamueleza jinsi alivyokuwa akipigiwa simu na kupewa maelekezo ya kumsaidia Sabrina.
"Kwakweli hadi mama yako alinihisi uongo ila nilipigiwa simu na namba ngeni na sauti ilikuwa kama yako ila ya upole sana. Cha kushangaza namba hiyo hatukuiona tena kwenye simu"
"Pole Dorry ila hata mie hiyo khabari inanishangaza jamani, maana mambo kama hayo nimezoea kuyaona kwenye filamu na kusoma kwenye vitabu vya hadithi mmh! Inamaana umepigiwa simu na jini au ni kitu gani hicho?"
"Hata mimi sielewi hadi leo, kuna siku hata nilipigiza simu chini ila mama yako aliiokota ikiwa nzima kabisa. Mambo ya ajabu haya, si umemuona mama anachechemea yani alipata ajali kwa mambo haya haya"
Jeff alizidi kushangaa tu hiyo taarifa kwani hakuwa na wazo lolote juu ya majini, kwahiyo aliona kuwa ni taarifa ya ajabu kwake.
Pia akamueleza kuhusu swala la yeye kutoa makaratasi na jinsi mama yake alivyoambiwa kuwa ile nyumba yao ina majini kwani ndio yaliyotoa yale makaratasi.
"Mwambie mama yako awe makini sana na waganga, ni waongo na wamekula hela zake bure tu"
Ila Jeff alicheka kwa hii taarifa ya sasa kuwa karatasi zilitolewa na Dorry ila mama yake akaambiwa ni jini.
Wakaongea mengi na Dorry akamuahidi kumpelekea kile kitabu chake alichokichukua katika harakati za kukimbiza ile barua.
Wakaagana hapo na Jeff kurudi nyumbani kwao.
Sam alitulia nyumbani kwake siku ya leo huku akitafakari baadhi ya mambo.
Alikuwa akitafakari kuwa Sabrina akirudisha kumbukumbu zake itakuwaje.
"Mungu asaidie ili Sabrina aendelee na upendo ule ule aliokuwa nao mwanzoni juu yangu. Hata kama kazaa na wanaume gani huko ila bado nampenda Sabrina. Kitu kimoja tu ambacho anashindwa kunielewa ni kuwa siwezi kumuua. Nitamuuaje mwanamke ninayempenda kama yeye? Sielewi hata kwa Neema ilikuwaje, Mungu naomba nisamehe"
Simu yake ikaita na mpigaji alikuwa ni Sia ambapo alikuwa akimsalimia Sam.
"Mmh ila usije leo, nitakwambia ni lini uje"
"Sawa"
Ila Sia alisononeka kwa jibu hili kutoka kwa Sam kwani alipenda akubaliwe ombi lake kwa siku hiyo.
Jeff alirudi nyumbani kwao na ilikuwa ni jioni tayari ila leo aliamua kumueleza mama yake vitu kidogo kumuhusu Dorry,
"Yani siku zote hizo niko nae hapa kumbe alikuwa akinidanganya jamani!"
"Msamehe bure mama, shida ndio zilimfanya atende haya ila kaniomba sana nimuombee msamaha kwako. Tafadhari mama msamehe"
"Kale katoto ni kapumbavu sana, yani kunidanganya mtu mzima kama mimi kweli na akili zangu timamu!"
"Mama, usilaumu sana. Kila kitu hutokea kwasababu fulani mama yangu, si unaona alisaidia kwa matatizo ya mamdogo Sabrina. Kwahiyo tusilalamike tu, tuangalie na upande wa pili"
"Hata kama, ila mi ameniudhi sana"
Kisha Jeff akamuelezea mama yake kuhusu kitu kinachomsumbua Dorry na pia jinsi mama yake alivyodanganywa na mganga.
"Kheee yani yule mganga alinidanganya jamani loh! Yani anavyojaza watu kiasi kile sikutegemea kama anaweza kuwa mganga wa uongo jamani"
Sakina akatafakari na kuona kuwa ni wazi ameshaliwa pesa zake nyingi sana na mganga huyo.
"Sikutegemea kama yule mganga alinidanganya kiasi hicho"
Jeff alimwacha mama yake pale akijisikitikia kisha yeye akaenda chumbani kwake kutuliza akili yake.
Sakina pale sebleni akajikuta akikumbuka maneno ya yule mganga wa pili na kuhisi kuwa huenda yana ukweli ndani yake kwani alishamwambia amchunguze sana Dorry, akakumbuka na alivyoambiwa kuhusu Sabrina.
Akakumbuka mara ya mwisho mganga alipowakaribisha alipoenda na Sabrina.
"Mmh! Kwanini alimuita Sabrina kuwa mkwe wangu? Mbona naona mambo yanarandana na kule hospitali? Ila bado hainiingii akilini kabisa, yani Jeff alale na Sabrina? Hapana hapana nakataa"
Kwa kipindi hiki Sakina alijiona wazi kuto kujielewa kabisa na alikuwa akijiuliza vitu na kujijibu mwenyewe.
Alishindwa kuamini wala kuelewa chochote.
Jeff alikuwa akitafakari namna atakavyoweza kuzungumza na Sabrina kwani aliona wazi kwa pale kwakina Sabrina itakuwa ngumu ila je ni sehemu gani ataweza kuzungumza nae.
Wakati akiwaza hayo, akapigiwa simu na Dorry
"Yule mtu kanipigia simu tena Jeff"
"Kakupigia tena? Alikuwa anasemaje? Vipi umebahatika kuikariri namba yake?"
"Sijabahatika kwakeli, leo iliita na kutokea jina rafiki. Nikapokea na kusikia sauti yake. Ila kwenye simu yangu hakuna jina rafiki na hata alipokata nimepekua sijaliona"
"Mmh pole sana, unatakiwa ufanye ibada Dorry yasije yakawa makubwa bure"
"Sawa, ila kaniambia kuwa nikwambie wewe umpeleke mamako mdogo sehemu ya mwisho uliyokuwa naye kwa muda mrefu na umsomee barua yake"
Jeff akashtuka na kumuuliza Dorry,
"Je amekwambia kuwa hiyo barua inahusu nini?"
"Hapana hajaniambia"
"Haya nashukuru, nitafanyia kazi hilo swala"
Jeff akakata simu na kupumua kidogo huku akimuona huyo mtu kuwa ni nuksi sasa na kuona wazi kuwa anaweza kumuumbua muda wowote ule.
Jeff akaamua kulala sasa kwani alishatafakari vya kutosha.
Kulipokucha nyumbani kwa Neema alionekana kuwa hoi sana siku ya leo kuliko siku zote.
Aisha akajaribu kumuandalia uji ili ampe ila hakuweza kunywa, alionekana kutokwa na machozi tu.
"Jamani dada, kunywa japo kidogo jamani"
"Sitaki kufa Aisha, sitaki kufa kabla ya kutubu. Nahitaji kumwambia ukweli mtu huyu, nimemkosea sana"
"Nani huyo dada?"
"Sabrina, nahitaji kumwambia ukweli Sabrina. Nimekoma kutembea na waume za watu, tamaa imeniponza Neema mimi"
"Dada, unajua sikuelewi jamani, sikuelewi kabisa dada yangu kwani una nini leo?"
Neema akaanza kuropoka kamavile mtu aliyechanganyikiwa,
"Yule mwanaume, mwanaume yule anaota miba. Yule mwanaume ana misumali, yule mwanaume anatoa usaha, yule mwanaume ana........."
Neema akaanza kuweweseka sasa na kugeuza geuza macho.
Itaendelea
No comments:
Post a Comment