"Eeh eleza shida yako mama"
"Kwanza kabisa, kabla ya yote niangalizie kama
huyu mtoto wa Sabrina ni wa mumewe kweli"
Mtaalamu akacheka, kisha akasema,
"Yule mtoto si wa mumewe"
"Mmmh amezaa na nani sasa?"
"Ni damu yako"
Sakina akashtuka na kumuangalia kwa makini yule
mtaalamu.
Kisha akamuuliza,
"Damu yangu kivipi?"
"Inamaana hujua ninachomaanisha kwa kusema ni damu yako?"
"Sijui ndio"
"Basi huo na uwe mtihani kwako, nenda ukajitafakari utapata jibu kwa ninachomaanisha"
"Inamaana huwezi kuniambia?"
"Ndiomana nimekupa kama mtihani, halafu nenda umchunguze vizuri yule unayehisi ni mkweo"
"Kivipi?"
"Nenda kamchunguze tu"
Sakina akaonekana kuchukizwa na lile jibu la mtaalamu na kumfanya aondoke bila ya kumuaga wala kumuuliza swali jingine.
Akiwa njiani ni njia nzima kumlaani yule mganga tu,
"Miwaganga mingine kama michoko, yani mi nimeenda kwake linipe jibu eti na lenyewe linanipa mtihani ndiomana halina watu. Kesho asubuhi nitawahi kwa yule mtaalamu wangu. Hili choko limenikera sana"
Alichukia sana hadi anaingia nyumbani kwake alikuwa akiongea peke yake huku akimlaani yule mganga.
Alimkuta Dorry ndani akiwa ameandaa kila kitu, na kumkaribisha kwa ukarimu sana, hadi akajikuta akiongea kimoyo moyo.
"Miwaganga mingine bhana, sasa binti mzuri kama huyu nimchunguze kitu gani maana huyu ndiye mkwe wangu."
Alimalizia kwa kuongea kwa sauti,
"Ndiomana yule mganga hana wateja pale"
Ikabidi Dorry amsikilize kwa makini huyu mama mkwe wake na kumuuliza kuwa anazungumzia kitu gani.
"Hamna kitu, ila kuna miwaganga inaishi kwa uongo tu. Mi nilijiuliza kuwa kwanini huyu mganga hana wateja kumbe ni liongo bhana"
"Pole mama, kakudanganya nini tena?"
"Yani wee acha tu mkwe wangu"
"Ila mama, waganga karibia wote ni waongo sio wa kuwaamini kabisa"
Huku akikumbukia alivyochukua yale makaratasi halafu mama mkwe wake kuambiwa na mganga kuwa yale makaratasi yaliondoka kichawi.
"Hujui tu Dorry, wamenisaidia sana hapa mwanangu"
Dorry hakutaka kumpinga zaidi kwa kuhofia kugundulika.
Kwahiyo akamuitikia kuhusu swala lake la kubadilisha mganga kama alivyopanga mwenyewe.
Sam alitoka ofisini na kuanza safari ya kurudi nyumbani kwake ila alipokuwa njiani alijikuta akitamani kumuona Neema.
Hamu ile ilimzidia na kumfanya ageuze gari na kuelekea kwa Neema.
Alipofika alikuta mlango umefungwa, akajaribu kumpigia simu ila haikupokelewa na kujikuta moyo wake ukiumia sana.
Akaamua kukaa na kumsubiri kidogo, ila muda ukaenda bila Neema kurudi na kumfanya Sam aumie zaidi na kuamua kuondoka kuelekea nyumbani kwake.
Alipofika nyumbani kwake alijifikiria sana, alifikiria tatizo lake ni nini.
"Mbona sijisikii kwenda kumuona mke wangu niliyempenda sana? Kwanini niende kumuona mtu asiyenihusu halafu niumie kiasi hiki?"
Sam hakujielewa kabisa, alijiona kuchoka sana na kuamua kwenda kulala.
Kulipokucha kama kawaida akajiandaa na kwenda kazini kwake ila mawazo yake yote yalikuwa kwa Neema tu na akapanga kwenye mida ya saa nne aende tena kumuona Neema maana alikosa raha kabisa kwa kutokumuona jana yake.
Kwahiyo muda aliopanga ulipofika tu akatoka ofisini na kuelekea nyumbani kwa Neema.
Alipofika, aligonga na kufunguliwa na Neema kisha akaingia ndani.
Neema alikuwa akifikicha macho kuonyesha kuwa alikuwa amelala.
"Karibu Sam"
"Khee umelala muda huu Neema?"
"Uchovu tu, kwani saa ngapi saivi?"
"Saa tano hii ndio bado umelala!"
"Sina la kufanya ndiomana nikalala hadi muda huu"
Basi Sam akatulia mule ndani akimuangalia tu Neema.
Muda kidogo alifika rafiki wa Neema ambaye hakujua kama ndani kuna mtu kwani alianzia mlangoni kuongea huku akifungua mlango,
"Kheee Neema sebene la jana ndio ume......"
Akashtuka kumuona mgeni ndani na kumsalimia,
"khabari yako shemeji"
Sam akamuangalia na kuitikia,
"Nzuri tu"
Neema nae akatoka ndani na kuanza kusalimiana na rafiki yake ambaye alikuwa ni Rose kisha akamtambulisha kwa Sam,
"Huyu ni rafiki yangu mkubwa sana, anaitwa Rose"
Kisha akamgeukia Rose na kumwambia,
"Na huyu anaitwa Sam"
Rose akamuangalia Sam kwa jicho la aibu kisha wakasalimiana tena.
Muda kidogo Sam akawaaga na kuondoka.
Neema alipobaki na rafiki yake huyo waanza kujadiliana kuhusu Sam,
"Mmh sijui atanikumbuka?"
"Kwanini?"
"Si unakumbuka mpango wetu wa kipindi kile?"
"Nakumbuka ndio, kwani ulikutana nae kweli?"
"Nilikutana nae ndio"
"Mmh tuipotezee hiyo, jifanye kama sio wewe siku nyingine"
Wakakubaliana kuhusu hilo swala.
Sam akiwa njiani akaikumbuka ile sura ya Rose yule rafiki wa Neema.
Akakumbuka jinsi alivyomwambia kuwa anamfahamu sana yeye na mkewe.
Hapo hapo swala la mkewe pia likamjia kwenye akili yake na kujishangaa kuwa kwanini anakuwa mzito vile, akakumbuka na jinsi alivyomjibu mkwe wake.
"Kwanini akili yangu imekuwa hivi jamani? Inastahili kweli kumfanyia Sabrina hivi? Ila naona ni sawa sababu amenionea sana"
Hakuona zuri lolote tena kutoka kwa Sabrina kwani muda wote Mawazo yake yalikuwa kwa Neema tu kipindi hiki, hadi akaamua kwenda kwake moja kwa moja kwani hakujisikia tena kurudi ofisini.
Sakina aliamua kwenda kwanza kwa wakina Sabrina kumuangalia mdogo wake.
Alifika na kumkuta Sabrina na mama yake huku akijaribu kumuelekeza baadhi ya mambo.
Cha kushangaza Sabrina akawa na zile kumbukumbu za alipokuwa mdogo kwani alipomuona Sakina akamshangaa na kumuuliza,
"Kheee dada ulishajifungua? Mbona tumbo lako halipo tena?"
Sakina na mama Sabrina wakacheka kidogo na kujaribu kumuelewesha hali halisi ilivyo, kama alishajifungua na mtoto yupo nje ya nchi na kila kitu kumuhusu Jeff lakini bado Sabrina hakuelewa chochote wala kukumbuka kitu.
"Ila taratibu utaelewa tu, maana kama umeanza kukumbuka mambo ya zamani basi itakuwa rahisi kukumbuka na mapya"
Wakajipa moyo pale, kisha Sakina akaaga na kuondoka.
Njiani akapanga kwenda kwa mganga kama kawaida yake, ila alipanga kwenda kesho yake ili aweze kumuwahi yule mganga anayedhani yeye kuwa ndio wa ukweli.
Sam akiwa nyumbani kwake mida ya saa nne usiku, wazo la Neema likazidi kumtawala katika kichwa chake na kuamua kupiga simu.
Ile simu iliita mara ya kwanza bila ya kupokelewa, na mara ya pili ikapokea sauti ya kiume na kumfanya Sam ashangae kuwa kwanini simu ya Neema ipokelewe na mwanaume.
Sam akaikata ile simu, na muda huo huo akapigiwa yeye na kuipokea,
"Mbona unapiga simu huongei?"
"Aaah samahani, nilikosea namba"
"Umekosea namba wapi wewe, umepiga simu ya mdada umeona kapokea mkaka ndio oooh samahani nimekosea namba. Unafikiri mi sijui? Nimejua vizuri, huna lolote wewe"
Kisha akaanza kumtukana Sam na kumfanya Sam aikate ile simu kwa hasira.
"Yani mi natukanwa sababu ya mwanamke?"
Akajisikitikia sana ila bado mawazo yake yalikuwa kwa Neema tu, ambapo aliona ndio mwanamke pekee anayemfaa kwa wakati huo katika maisha yake.
Sam aliamua kulala huku mawazo yakiwa mengi zaidi.
Alipopitiwa na usingizi akajiwa na ndoto, alimuona Sabrina upande wa kulia na Neema upande wa kushoto halafu yeye akiwa katikati yao, huku Sabrina akikazana kumuita ili aende upande wake ila hakuweza kwenda kwani alijikuta akiwa amejawa na penzi la Neema kisha akaelekea upande wa Neema.
Baada ya muda akaonyesha kumuhurumia Sabrina ila kabla hajasogea kwa Sabrina akaona kuna kijana akiondoka na Sabrina.
Sam akajikuta akishtuka usingizini huku akiongea,
"Usiende Sabrina"
Akajishangaa kuwa ilikuwa ni ndoto, akajiuliza inamaana gani katika maisha yake ila hakupata jibu lolote na kujikuta akiwa macho huku akimlinganisha Sabrina na Neema hadi panakucha.
Alfajiri na mapema Sakina kama alivyopanga akajihimu ile asubuhi ili kuwahi kwa yule mganga ambaye yeye anaona ndio anayefaa na huku akiamini kuwa atamwambia ukweli wa mambo yote.
Alitoka kwake na kumuaga Dorry kama kawaida kisha akaondoka.
Sam alitoka nyumbani kwake na kuelekea ofisini huku baadhi ya wafanyakazi wake wakitamani sana kumuuliza kuhusu Sabrina ila waliogopa kuwa inaweza kuhatarisha vibarua vyao.
Kwahiyo wengi walikuwa kimya tu.
Muda kidogo pale ofisini kwa Sam akafika Neema ambapo Sam alipomuona tu akamfata na kumkumbatia na kusahau kabisa kama jana yake alipopiga simu ilipokelewa na mwanaume.
Sam alifurahi tu kumuona Neema na muda huo huo wakatoka pale ofisini.
Muda wametoka ndipo wale wafanyakazi walipoanza kuwajadili kama kawaida yao,
"Jamani mnamuelewa bosi Sam siku hizi?"
"Mmh hata simuelewi kwa mimi, na huyu dada wa leo ndio nani?"
"Ingekuwa zamani nisingemshangaa ila bosi toka alipokuwa na Sabrina alikuwa ametulia sana. Hili kumbatio la leo hata sijalielewa, au nyie wenzangu mmelielewa?"
"Tulielewe wapi majanga tu"
Wakajadiliana pale na kucheka kwa umbea na unafki.
Sam alienda na Neema moja kwa moja kwenye hoteli kwa lengo la kupata supu.
Wakati wako pale wakafatwa na mtu ambaye anawafahamu vyema,
"Nimewaona wakati napita hapo ndio nikaona ni vyema nije niwasalimie"
Wakafurahiana pale, mtu huyo alikuwa ni Francis ambaye hakuelewa ni kwanini dada yake yupo na Sam kwa muda huo, ila akaona ni vyema kuulizia hali ya Sabrina,
"Vipi Sabrina hajambo?"
"Hajambo ndio"
"Basi msalimie ukirudi"
"Poa"
Francis hakutaka kuhoji zaidi ingawa majibu ya Sam yalimshangaza sababu alijibu kwa kifupi sana.
Kisha akawaaga pale na kuondoka zake.
Kisha wao kuendelea na mambo yao mengine mpaka muda wa Sam kurudi ofisini, akampeleka kwanza Neema nyumbani kwake kisha yeye kurudi ofisini tena bila hata ya kuuliza kuhusu simu ya usiku.
Sakina akiwa kwa yule mganga wake, kama kawaida akamueleza tatizo lililompeleka pale.
"Hebu niangalizie kwanza huyo Sam kapatwa na nini?"
"Huyu karogwa, tena aliyemroga alikuwa anamuonea wivu huyo mdogo wako"
"Na Sabrina je ule ugonjwa hajarogwa kweli?"
"Naye amerogwa"
"Sasa tufanyaje?"
"Hapa inatakiwa wapatikane ng'ombe wakubwa wawili, dume na jike hapo ndio itawezekana kuwazindua"
Sakina akapumua kidogo,
"Mmh mbona itakuwa gharama sana mtaalamu?"
"Ndio itakuwa gharama kwavile tatizo lao ni kubwa sana, tukitaka kuwasaidia lazima tufanye hivyo"
"Mmh khatari, haya nitajie basi aliyewaroga"
"Kumtaja huyo mtu inabidi apatikane kondoo mkubwa sana"
Sakina akaona sasa mambo yatamshinda na kuomba muda wa kwenda kujiandaa kisha akamuaga yule mtaalamu na kuondoka.
Akiwa njiani, akaona gari la Sam linakuja na kusimama karibu yake kisha Sam akamsalimia Sakina.
"Khabari dada"
"Nzuri shemeji, umepotea sana"
"Majukumu tu shemeji, nikija tutaongea vizuri"
Kisha Sam akawasha gari yake na kuondoka.
Sakina alimuangalia hadi alipotokomea huku akitafakari jinsi dawa zilivyofanya kazi kwa Sam.
"Mmh hata kuulizia hali ya Sabrina hakuna! Duh kweli aliyemroga amemroga sana"
Kisha akaendelea zake na kurudi kwake.
Sam alirudi nyumbani kwake huku akimuwaza Neema tu,
"Hata nimeshindwa kumuuliza kuwa kwanini jana simu yake imepokelewa na mwanaume mmh! Mapenzi yameniteka kwakweli"
Alijifikiria sana ila upendo wake kwa Neema nao uliongezeka mara dufu.
Sabrina akiwa nyumbani kwao na mama yao, akafika kaka yake ambaye ni James na akaonekana kukosa raha kabisa.
Mama wa Sabrina aliamua kumuuliza mwanae kwanini yupo vile.
"Unamatatizo gani mwanangu?"
"Mama, kichwa changu kimevurugika sana. Ila ningependa uniambie ukweli ili akili yangu iwe sawa"
"Kivipi?"
James akamvutia mama yake pembeni ili aongee naye kwa uhuru kabisa.
Muda wanaongea, kuna mtu alitokea nyuma yao.
"Mama niambie ukweli mimi baba yangu ni yupi?"
Yule mtu naye akazungumza,
"Na mimi niambie ukweli, mtoto wangu ni yupi?"
Mama wa Sabrina na mwanae wakajikuta wakigeuka na kumuangalia yule mtu.
Itaendelea
No comments:
Post a Comment