James akamvutia mama yake pembeni ili aongee
naye kwa uhuru kabisa.
Muda wanaongea, kuna mtu alitokea nyuma yao.
"Mama niambie ukweli mimi baba yangu ni yupi?"
Yule mtu naye akazungumza,
"Na mimi niambie ukweli, mtoto wangu ni yupi?"
Mama wa Sabrina na mwanae wakajikuta wakigeuka
na kumuangalia yule mtu.
Alikuwa ni James, yule baba mkwe wa kaka wa Sabrina.
Mama wa Sabrina akamuangalia yule James mwalimu wake wa kwaya, kisha akamuangalia James mwanae na kuinamisha kichwa chini.
Akatafakari kidogo na kumuomba James mwanae akamsubiri kidogo ili azungumze na yule mwingine.
"Hapana mama, mi ndio nimewahi hapa. Unatakiwa kunisikiliza mimi kwanza"
"Tatizo nini James? Mbona umekuwa hivyo? Hutaki kunisikiliza mama yako kwanini? Kumbuka mama huwa hakosei, na kila kitu hukifanya kwa manufaa yako, yani leo hii unamthamini aliyekunywesha sumu ya uongo na kuacha kumthamini mama yako mzazi? Au umepata mama mwingine, nenda ukamuulize labda mimi sio mama yako"
James akapata uoga kidogo kwa maneno ya mama yake na kwenda kukaa ndani akimngoja amalize kwanza kuzungumza na yule mkwe wake.
Sasa mama wa Sabrina akamgeukia yule James mwalimu wake,
"Hivi ni nani kakwambia hayo maneno?"
"Joy, mimi ni mtu mzima, usidhani itakuwa rahisi kunitisha kwa maneno kama ulivyomtisha mwanao. Nimeambiwa na wifi yako, nataka unithibitishie sasa mwanangu ni yupi kati ya hao watatu?"
"Laiti ungekuwa mtu mzima kama unavyosema ni wazi ungefikiria maneno ya kuzungumza kabla ya kuzungumza. Eti mwanangu ni yupi? Huna hata aibu, jitu lenyewe ulinibaka sikuwa hata na mtoto kipindi hicho halafu unaniuliza mwanao ni yupi? Tumia akili yako changanya na akili ya aliyekwambia, sitaki maswali ya kijinga"
"Hivi Joy kwanini unifanyie hivi lakini? Najua nilitenda kosa lakini sikustahili adhabu hii jamani? Yani kunificha kuhusu mwanangu kwa miaka yote hiyo ni haki kweli? Na kwa maneno yako inamaana mwanangu ni huyu huyu James, hivi Joy kwanini kuniumiza hivi?"
Huyu James hakuweza kuvumilia kisha akamuita James kaka wa Sabrina ambapo James naye akatoka ndani.
Alipomuona tu akamsogelea na kumkumbatia,
"Mwanangu James, wewe ni damu yangu, wewe ni mwanangu"
James akawa anashangaa tu,
"Mbona sielewi?"
"Ndiomana wakakupa jina langu, ndiomana umefanana na mimi. Wewe ni damu yangu James"
"Bado sielewi"
"Mwambie mama yako akueleweshe."
Kisha akamuachia pale halafu yeye akaondoka bila hata ya kuaga.
James akiwa njiani, mawazo yote yalikuwa kwa mwanae,
"Inamaana mwanangu kamuoa mwanangu? Maana James kamuoa Joy mwanangu"
James akahisi kuchanganyikiwa kabisa, na kwa bahati mbaya hakuona gari mbele yake wala kusikia honi, alijikuta yupo chini kwani alipata ajali pale pale barabarani.
Wasamalia wema wakamchukua na kumpeleka hospitali kwani dereva wa gari lililomgonga alishakimbia na gari lake.
Huku nyumbani alibaki James na mama yake sasa, huku James akimtaka mama yake amwambie ukweli kwa kile alichokisikia.
"Tafadhari James usitake kuvuruga akili yangu, usiivuruge kabisa. Kama alivyokwambia huyo mkweo ndio hivyo hivyo, mi msinivuruge"
Kisha akamuacha James pale nje na yeye kuelekea chumbani kwake.
James naye hakujielewa pale, akaona ni vyema aende kwa mkewe wakapeane ushauri wa hapa na pale.
Sam kwa kipindi hiki alikuwa akishughulika na Neema tu, mawazo kuhusu familia ya wakina Sabrina au Sabrina na mtoto hakuwa nayo kabisa.
Wazo pekee lililojaa kwakf ilikuwa ni Neema tu, kwani alipenda kumuona mbele ya macho yake kila siku na hakuchoka kumuona kabisa.
James alifika kwa mkewe Joy, na alipomuona tu akamkumbatia na kuanza kutoa machozi.
"Nini Mume wangu? Una tatizo gani?"
"Joy wewe ni dada yangu"
"Dada yako? Umepandwa na wazimu au? Dada yako ni Sabrina na sio mimi"
"Wewe ndio dada yangu, tena dada wa damu"
"Mbona sikuelewi James, na wewe umepoteza kumbukumbu jamani?"
James alikuwa akitokwa na machozi tu.
"Niambie basi, umepatwa na nini mume wangu jamani?"
"Siamini, siamini kabisa. Mwanamke ninayempenda kimapenzi, na kuamua kumuoa na kuzaa naye kumbe ni dada yangu wa damu? Kwakweli siamini, siamini Joy"
"Jamani James, mi unanichanganya ujue"
"Baba yako Joy, ni baba yangu mzazi"
"Kivipi? Nieleweshe"
James alikuwa amechanganyikiwa kabisa huku akilia, mara simu ya Joy ikaanza kuita akaipokea sababu mpigaji alikuwa ni mama yake,
"Joy, tupo hospitali huku. Baba amepata ajali"
"Nini?"
Mama yake akampa maelekezo tu ya hospitali waliyopo.
Joy akamwambia James alichoambiwa na mama yake, James alijikuta akilia zaidi tu,
"Ooh Mungu, kwanini unaniadhibu hivi? Sina kos mie"
James akamruhusu mkewe aende kisha yeye abaki nyumbani.
"Hapana James twende wote, siwezi kukuacha na hali hiyo. Tafadhari twende"
Ikabidi wampigie simu dereva wa gari za kukodi ili awapeleke huko hospitali.
Walipofika, Joy akamuona mama yake na baadhi ya ndugu zake pale nje, akamfata mama yake,
"Kwani mama ilikuwaje? Na baba yuko wapi?"
"Hata sisi bado hatujamuona. Kwakweli nimechanganyikiwa mwanangu. Nimepigiwa simu tu mimi na mtu hata simfahamu ndio akanipa khabari hii"
Ikabidi wakae wasubiri kwenda kumuona, muda wote huo James alikuwa kajikunyata kwenye benchi pale hospitali akiomba tu kwani hakujua hatma ya maisha yake na mkewe itakuwa ni nini.
Alikuwa akitafakari tu kuwa iweje amuoe dada yake? Tena dada yake wa damu. Ila hakuwa na jibu kabisa kwani alipomtazama mtoto wao aliyebebwa na mkewe, akiitazama na ile mimba ya mke wake ndio alikosa jibu kabisa.
Muda kidogo daktari akawaita na kisha kuwauliza,
"Kuna mtu anaitwa James hapo kati yenu?"
Ikabidi wamuite James kwani bado alikuwa amejiinamia pale kwenye benchi.
"Basi huyu ndio namuomba kwa muda huu"
Kisha yule daktari akaongozana na James.
Sakina alirudi nyumbani kwake, na moja kwa moja akaenda kwa wakina Sabrina huku akitamani kumwambia Sabrina ukweli kuhusu swala zima la kurogwa ila mashaka yake ni je Sabrina atamuelewa ukizingatia kumbukumbu hana.
Alimkuta Sabrina akicheza na mwanae, kisha akamuuliza
"Hivi Sabrina unajisikiaje kulea mtoto mwenyewe wakati mume wako yupo tena tajiri tu"
"Kwani mimi nina mume?"
"Ndio, Sam ni mume wako Sabrina. Kwanini ukae bila kuelewa kuhusu mumeo?"
"Kama nina mume mbona simjui?"
"Alikujaga hospitali kukuona pale mwanzoni"
"Aaah ndio yule kaka mzuri?"
"Ndio huyo huyo, anaitwa Sam. Tena huyo mtoto umezaa nae na hiyo mimba uliyonayo ni yake, inamaana mama yako hajakueleza?"
"Mmh hajaniambia kabisa, na mbona huyo mume haji huku kwetu?"
"Subiri kesho twende nyumbani kwake labda utakumbuka vizuri kuhusu yeye"
Sakina akaona ni vyema aweze kumfanya Sabrina akumbuke hata kidogo tu ili iwe rahisi kuhusu swala zima la kwenda nae kwa mtaalamu.
Kwahiyo akapanga nae kwa siku ya kesho kwenda nyumbani kwa Sam ambapo Sabrina alikubali tu bila kinyongo.
James alipelekwa moja kwa moja alipolazwa baba mkwe wake ambaye ndiye baba yake mzazi.
Akasogea karibu yake, daktari naye akamwambia
"Ongea naye kwa ustaarabu, maana amekutaja sana hapo"
James akatikisa kichwa na kuanza kwa kumpa pole pale kitandani ambapo baba yake huyo alikuwa akiongea kwa shida sana kutokana na maumivu yake.
Alianza kwa kumwambia James,
"Nisamehe mwanangu, natamani ningepata hata fursa ya kukubeba kwenye mikono yangu ulipokuwa mdogo. Roho inaniuma sana, umeoana na dada yako. Nitaiweka wapi sura yangu mimi kwa aibu hii, kwanini Joy kanifanyia hivi?"
Machozi yakamtoka, muda huo James naye akatokwa na machozi huku akijaribu kumtuliza baba yake huyo.
"Tulia baba usilie, ngoja upone kwanza tutawekana sawa kuhusu hili"
"Sitamani kupona James, natamani kufa hata muda huu. Moyo unaniuma sana, wewe ni damu yangu. Iweje leo uwe na dada yako? Aibu kwangu, nitajilaumu maisha yangu yote. Natamani kufa kwakweli"
"Usiseme hivyo baba, bado natamani uwepo wako katika maisha yangu. Tafadhari nitazame mwanao, utaniacha katika hali gani? Utanifanya nijute kuzaliwa. Kila siku nilikuwa najiuliza kuwa kwanini baba hayupo karibu sana na mimi? Labda hajui ila damu zetu haziendani. Tafadhari usiniache, kuwa nami japo kwa muda mfupi wa maisha yangu"
Maneno haya yalimuingia vilivyo baba huyu pale kitandani, na kujikuta akiumia zaidi ya mwanzo.
Daktari akamuomba James amuache baba huyu apumzike kwanza, kisha akamchoma sindano ya usingizi.
Kwahiyo hata mkewe na baadhi ya ndugu walimuona akiwa amelala huku wengi wakimshangaa James kwa kutokwa na machozi ambapo aliamua tu kuondoka eneo lile.
Joy alipoona James katoka akaamua kumfata kwa nyuma,
"Kwani leo una tatizo gani? Na baba alipokuita alikuwa anakwambia nini?"
"Aah hamna kitu ila mi naenda nyumbani"
"Mbona hueleweki James?"
Joy hakuwa na jinsi zaidi ya kuamua kufatana nae na kurudi nyumbani kwao tu.
Sabrina kwa jioni ya siku hiyo aliamua kumuuliza mama yake kuhusu huyo mume wake aliyeambiwa na Sakina.
"Mbona mama hukunieleza tena kuhusu huyo mume wangu?"
"Achana nae huyo mwanangu, atakuumiza kichwa tu"
"Kwanini mama?"
"Hafai yule, akijisikia atarudi tu mwenyewe"
Sabrina hakutaka kumuhoji zaidi mama yake kwani alishapanga na Sakina tayari.
James alirudi nyumbani na mke wake huku mkewe akikazana kumuuliza kuhusu tatizo lake kwa siku hiyo ila bado James hakuweza kumueleza kwa uwazi kuhusu yanayomsibu kwani alijua ni lazima atachanganyikiwa tu na yeye.
Ingawa alimlazimisha sana ila bado hakumwambia.
Muda kidogo James akapigiwa simu na mama yake,
"Wee James mbona nakupigia simu muda wote hupokei?"
"Samahani mama, nilitoka halafu simu niliacha nyumbani"
"Sawa, ila uwe makini kwa yaliyotokea leo. Nakuomba urudi nyumbani ili tuweze kuzungumza"
"Hapana mama sitaweza, na hivi ninavyokwambia ni kwamba baba yupo hospitali alipata ajali mchana ule"
"Nani kapata ajali? Unamuongelea yupi?"
"Namuongelea baba yangu mzazi"
"Nani?"
"Unayemjua wewe mama"
James akamkatia mama yake simu kwani hakutaka kuendelea kuongea nae zaidi.
Ndipo Joy alipomuuliza kwa karibu zaidi mumewe ili amueleze hali halisi ilivyo.
James akamuahidi kumueleza kesho yake,
"Nakuahidi Joy, nitakueleza kila kitu kesho ila kwavile muda umeenda saizi ni bora tulale tu"
Joy hakubishana nae kwavile kashamuahidi mwenyewe kumueleza kila kitu kesho yake.
Sam alishinda kwa Neema siku hiyo hadi usiku ule ndio akarudi nyumbani kwako, ambapo nyumba yake ilikuwa imepoa vilevile kama zamani kipindi ambacho alikuwa bado hajaoa.
Aliingia na kuchukua albamu yake ya picha za harusi ya yeye na Sabrina.
Akaona na picha za mtoto mdogo Cherry, roho ya huruma ikamshika sana moyoni mwake.
"Itabidi kesho niende kuwaona, hata kwa kumsalimia tu huyu mtoto"
Alijawa na roho ya huruma sana moyoni mwake kwa muda huo hadi alipolala.
Kesho yake, kama ambavyo Sakina alipanga.
Akaenda kumchukua Sabrina ambapo alimkuta kashamuandaa na mtoto,
"Mmh Sabrina, me naona mtoto tumuache"
"Hapana, sitamuacha mwanangu. Sitaki kumsahau tena, nitaenda nae popote pale ili nilipo awepo"
Sakina hakutaka kumfanya Sabrina ajisikie vibaya ila alishamgundua kuwa akili yake ya sasa ipo tofauti na akili yake ya mwanzoni.
Kwavile mama wa Sabrina alionekana kuwa na kazi nyingi kwahiyo wakamuaga juu juu na kuondoka.
Ila Sakina ndio akambeba mtoto wa Sabrina kwa kumuhurumia na mimba ile nyingine.
Walifika nyumbani kwa Sam kama kawaida wakamkuta yule mlinzi wa Sam ambapo alimkaribisha Sabrina kwa furaha sana.
"Aah mama umerudi! Pole sana kwa matatizo, ila baba hakuniambia kama utarudi leo, hata funguo hajaniachia"
Alimshangaa Sabrina akimtazama tu kamavile ni mtu asiye mfahamu yani ambaye hajawahi kumuona kabisa.
Yule mlinzi hakuchoka na kukazana kuwakaribisha ndani ila Sabrina na Sakina walisimama pale pale nje ya geti.
Muda mfupi tu, Sabrina akasikika akipiga kelele na kuanguka, wakashangaa kuona nyoka akikimbia na damu zikimtoka Sabrina mguuni.
Itaendelea
No comments:
Post a Comment