"Hivi hii ndoto inanijia mara kwa mara kwani
mume wangu ni nani?"
Akasikia sauti ya Jeff ikijibu kutoka mlangoni,
"Mimi hapa"
Sabrina akashtuka na kuuliza tena,
"Nani?"
Jeff akajibu tena,
"Mimi hapa Jeff"
Sabrina akainuka ili kuangalia kama kweli
anayemjibu ni Jeff.
Sabrina alipofungua mlango alimkuta ni Jeff kweli na kumshangaa kuwa kwanini ajibu kwamba yeye ndiye mumewe.
Akamuangalia kwa makini sana na kumuuliza,
"Ni wewe Jeff!!"
"Ndio ni mimi, kwani vipi?"
Sabrina akamzaba kibao Jeff na kumfanya Jeff ashangae na kumuuliza,
"Mbona unanipiga mamdogo! Kwani kosa langu ni lipi?"
"Ulikuwa unaniitikia nini hapa mlangoni? Je mimi ni mtani wako?"
"Sikuelewi mamdogo, kwani ni nini?"
"Inamaana hujui ulichokuwa unajibu hapa mlangoni au kiburi?"
"Kwakweli nakushangaa mamdogo, mi nilikuja mlangoni kwako kukugongea kuwa muda umeisha uamke uende kazini, ukauliza nani nikakujibu mimi, ukauliza tena nani nikakujibu ni mimi Jeff. Sasa hapo kosa langu ni lipi jamani?"
Sabrina alimuangalia Jeff kwa jicho la huruma na kumuomba msamaha, akajiona wazi kuwa mwenye makosa ni yeye na ndoto zake zisizoeleweka lakini yeye alichukua jukumu tu la kumpiga Jeff kibao bila hata ya kujiuliza au kumuuliza kwanza.
"Nisamehe sana Jeff toto yangu"
"Usijali mamy"
Jeff akaondoka na kumuacha Sabrina akiwa amesimama pale pale mlangoni.
Akasikia mtu akigonga mlango wao wa nje na kwenda kumfungulia, akashangaa kumuona kuwa ni Sam,
"Nimekupitia twende kazini"
"Nimesimamishwa kazi Sam"
"Mwenye uwezo huo pale ni mimi tu, haya kajiandae nakungoja twende"
Sabrina hakuamini masikio yake na kuamua kwenda kujiandaa haraka haraka ili aweze kuwahi kuondoka na huyo Sam.
Alipomaliza alitoka na kumkuta Sam akiwa bado anamngoja kwahiyo akatoka naye nje na kuondoka zao.
Ndani ya gari Sabrina akatamani sana kumwambia Sam kila kilichojiri juu yake wakati hayupo ila akajikuta akisita kwavile Sam alikuwa kimya sana hata tabasamu lake tu halikuonekana siku hiyo na kumfanya Sabrina nae akae kimya ili kuhofia kuharibu siku yake kabisa.
Walipofika ofisini, kila mmoja alikodoa macho kwa Sabrina huku wakiongea chini kwa chini, wakati huo Sabrina aliongoza moja kwa moja kwenye ofisi ya Sam.
"Nilijua tu kuwa atarudishwa"
"Ulidhani kuna mtu mwenye uwezo wa kumfukuzisha Sabrina kazi kwenye ofisi hii! Hakuna hata mmoja, na sie tukionekana tunachonga basi tutafukuzwa sisi"
Wakaangaliana na kugonga kwa mbali mbali kisha wakakaa kimya.
Sabrina alipokuwa kwenye ofisi ya Sam,
"Hebu nipe hiyo barua ya maelezo kuwa usimamishwe kazi"
Sabrina akatoa ile barua na kumkabidhi Sam, ambapo Sam aliisoma huku akitikisa kichwa na kumwambia Sabrina,
"Huwa simpendi mtu anayefanya kitu kinyume na maelezo yangu, sasa huyu atanijua vizuri kuwa Sam ni nani. Haya nenda ukaendelee na kazi zako"
Sabrina alikuwa kimya tu kwani hakuelewa hata kuwa Sam alitoa maelezo gani na kwanini waliopewa maelekezo walifanya kinyume.
Akatoka na kwenda kwenye ofisi yake, na kufanya baadhi ya watu kwenye zile ofisi kuishia kununa tu.
Wakati Sam yupo ofisini akifikiria namna ya kufanya na msaidizi wake ambaye alimpa barua hiyo Sabrina akapatwa na ugeni.
Alikuwa ni Joyce dada yake, mtoto wa mjomba ake.
Baada ya salamu, Joy akamwambia kaka yake
"Bora umerudi kaka, nina ujumbe wako mzito sana."
"Naomba badae tuonane nikwambie, maana nimejaribu simu zako hazipatikani ndiomana nikaona ni vyema nije moja kwa moja kama hivi"
Sam hakuwa na pingamizi na kumpa dada yake namba zingine alizokuwa anazitumia na kuagana nae huku wakipanga pa kuonana baada ya kazi.
"Basi usijali dada yangu nitakutafuta"
Joy akatoka kwenye ile ofisi na kupita kwenye ofisi ya Sabrina na kumsalimia kwa kugelesha kisha akamuaga na kuondoka.
Jioni yake Sam alimchukua Sabrina na kumrudisha nyumbani kwake kisha yeye akaamua kwenda kuonana na dada yake ili aweze kupewa ule ujumbe uliokusudiwa.
Walionana kama walivyopanga huku Sam akiwa na hamu ya kupata huo ujumbe.
Joy alianza kuongea kwa utulivu kabisa,
"Kwanza kaka samahani kwa nitakayo kwambia. Nimejitahidi kuvumilia lakini nimeshindwa na nimeona bora tu nikwambie halafu wewe mwenyewe ndio utaamua kula mbichi au iliyoiva"
"Usijali dada yangu, wee niambie tu"
"Ni kuhusu Sabrina"
Sam akashtuka sana na kumuuliza dada yake kwa mshangao,
"Kwani Sabrina kafanyeje!!"
Joy akapumua kwanza na kumuuliza kaka yake,
"Je! Una mahusiano yoyote ya kimapenzi na Sabrina?"
"Hapana, ila nampenda sana"
"Basi tahadhari kaka yangu, ule ni waya wa umeme. Ukikanyaga tu unanasa"
"Kivipi Joy? Mbona sikuelewi?"
Joy akaamua kumwambia Sam yale aliyoyasikia kumuhusu Sabrina kuwa ameathirika na chuo alichosoma wote wanatambua hilo na kumfanya Sam aishie kushangaa kwani hakufikiria hata kidogo kitu cha namna hiyo.
"Hivi Joy una uhakika na unayoyasema?"
"Ndio, nina uhakika kwa asilimia tisini na tisa pointi tisa kasoro sifuri pointi moja."
Sam akamuangalia sana Joy huku akijaribu kuyasoma mawazo yake na maneno yake, kisha akamwambia
"Asante kwa taarifa dada yangu, ila nitafanyia kazi hiyo taarifa yako ili niweze kujiridhisha na mimi mwenyewe"
"Sawa kaka, hakuna tatizo ila mi nimekupa ujumbe tu na kukuachia kazi wewe mwenyewe"
Wakaongea mawili matatu na kuagana.
Sam akiwa nyumbani kwake alijifikiria sana kuhusu Sabrina kama yale aliyoyasikia ni ya ukweli au la
"Kama ni kweli, basi Sabrina atakuwa amewaambukiza watu wengi sana kwa ule mtindo wake. Au ndiomana wakati mwingine anasema kuwa hataki mchumba! Mmh ananipa mashaka sasa"
Sam aliwaza sana bila ya kupata jibu la aina yoyote ile.
Sabrina alipokuwa nyumbani kwake, akagundua kuwa ana siku kama mbili tatu hajaingia kwenye mtandao wa kijamii
"Itakuwa kale kajamaa kamenimiss sana ila tatizo lake uongo mwingi, siku ile kamenigandisha pale hadi nikakutana na watu nisiowatarajia"
Ila akaamua kuingia kwenye mtandao ili kuona kama kweli Prince J amemkumbuka.
Alikutana na jumbe nyingi sana kutoka kwa Prince J za kumkumbuka, ila ujumbe uliomshtua ulikuwa ni mmoja tu toka kwa huyo huyo,
"Ipo siku nitakuja na tutalala wote, siku hiyo itakuwa ya furaha kwako kwani utaburudika kwa penzi ambalo nitakupa. Ila kesho yake najua utachukia sana, ila penzi langu lazima liache doa kwako na kukufanya unikumbuke siku zote za maisha yako"
Sabrina akashtushwa sana na ujumbe huo, kwanza alimshangaa huyo Prince J kwani alijua kuwa hatoweza kuonana nae tena hata iweje.
Akajiuliza sana bila ya majibu,
"Ila kwanini aseme hivi? Kwanini aandike ujumbe kama huu? Anamaana gani huyu mtu? Eti ataniachia doa, doa gani hilo? Yani mijitu mingine hata sijui kwanini nilikuwa nikichat nalo shetani hili, ndiomana watu husema kuna majini humu"
Sabrina akafanya kitu kimoja juu ya Prince J, akamfuta kwenye orodha ya marafiki zake facebook ili awe huru sasa na kusahau kuwa alishawahi kumpa namba ya simu kwa mawasiliano.
Sabrina aliamua kulala kwani alijua hata kama ataamua kuwaza sana hawezi kupata jibu la kumridhisha au la moja kwa moja.
Kulipokucha kama kawaida Sabrina alijiandaa kwenda kazini na akapitiwa na Sam na kuondoka naye.
Ila kwenye gari kila mmoja alikuwa kimya, hakuna aliyemuongelesha mwenzie hadi wanafika ofisini.
Ila walipofika kwenye mlango wa ofisi, Sam akamwambia Sabrina
"Badae nina maongezi na wewe"
"Sawa, hakuna tatizo"
Sam akaingia kwenye ofisi yake na Sabrina pia akaingia ofisini.
Sabrina akatulia kwenye meza yake na kupatwa na ugeni asubuhi ile ile, ugeni ambao ulimshangaza sana kwani alikuwa ni binti mdogo na moja kwa moja alimuulizia Sabrina na kupelekwa kwenye meza ya Sabrina,
"Karibu, niambie shida yako nikusaidie"
"Asante, kuna mtu kanituma na kanipa ujumbe huu"
Yule binti akamuachia karatasi Sabrina kisha akamuaga na kuondoka.
Sabrina akafungua lile karatasi na kukutana na maandishi ya mtu kuwa anaomba waonane nae baada ya kazi kwakuwa ana ujumbe wake.
Sabrina hakujua pa kuanzia wala kuishia ukizingatia Sam ameshamwambia kuwa badae aonane nae, na vipi huyu mtu aliyemtumia ujumbe je itakuwaje! Alitamani kumjua kuwa ni nani ila alikuwa njiapanda.
Jioni ilipofika, akaona ni vyema kuanza kuonana na yule aliyemtumia barua kwanza kwahiyo aliamua kwenda kwa Sam ili amuage,
"Naomba ruhusa bosi kuna mahali nataka kwenda kidogo"
"Si nimekwambia nina maongezi na wewe!"
Sabrina akakaa kimya kwa muda na kumjibu,
"Natambua hilo, ila naomba nikaonane na huyu kwanza"
"Haya nenda"
Sam alijibu kama mtu mwenye hasira sana ila aliyezificha hasira zake.
Sabrina akaondoka pale ofisini na kwenda mahali ambako alielekezwa kwa ile barua kuwa aende.
Alipofika pale, akaangalia kushoto na kulia ili kujua ni nani aliyemuita ila alitokea mtu kwa nyuma na kumziba Sabrina kwa viganja vya mikono yake, Sabrina akauliza
"Nani wewe?"
Yule mtu akamjibu,
"Otea "
"Mmh! Kuotea siwezi kwakweli, wee niambie tu kuwa ni nani"
Akacheka na kumuacha Sabrina amuangalie mwenyewe,
"Kheee kumbe ni Francis!"
"Ndio ni mimi mpenzi, mwanaume nikupendaye kupita wote duniani"
Sabrina akamuangalia Francis, kisha Francis akamuomba Sabrina kuwa wakae na waweze kuzungumza mawili matatu.
Sabrina hakukataa zaidi ya kukaa na kumsikiliza Francis,
"Siku zote nilikuwa natafuta siku nzuri na muda muafaka wa kuzungumza na wewe Sabrina, kiukweli bado nakupenda tena nakupenda sana"
Sabrina alimuangalia Francis bila ya kumjibu chochote kwavile alikuwa anajiuliza kuwa kati ya Francis na Fredy ni nani aliyekuwa anampenda kweli? Kwavile hakuelewa kwanini wote wanamwambia kuwa wanampenda sana.
Francis aliendelea kuongea tena kwa hisia kabisa,
"Sema chochote juu ya penzi letu Sabrina. Mi mwenzio bado nakupenda sana, nakuhitaji katika maisha yangu. Napenda uwe nami siku zote."
"Sawa Francis nimekuelewa tena sana tu ila tafadhari nipe muda ili niweze kutafakari"
"Kumbuka Sabrina, mi ni mwanaume pekee ninayekupenda toka kipindi kile. Yale yote niliyokuwa nikiongea zamani ilikuwa ni sababu ya hasira tu mpenzi. Tena usipende kumsikiliza Fredy, hana lengo zuri na wewe ila nia yake ni kuona kuwa penzi letu linaporomoka"
Francis aliongea mambo mengi sana na kumfanya Sabrina awe kimya kabisa akimsikikiza hoja zake.
"Natumaini una nielewa Sabrina, nakuombea yaliyo mema. Fanya uchaguzi sahihi katika maisha yako, wakati ni huu na hakuna wakati mwingine usije kujutia badae. Ushakuwa mtu mzima sasa, unatakiwa kuolewa na kuwa na familia yako. Najua majibu yanakuwa magumu kwangu kwavile ni wengi wanaokwambia kuwa wanakupenda, ila angalia kwa makini ni nani anayekupenda kweli ili badae usijutie tena"
"Nashukuru Francis, nimekuelewa sana tena sana hakuna haja ya kurudia maelezo"
Kisha wakaongea mengine kati ya yale, na muda nao ulikuwa umeenda hivyo Francis akamuomba Sabrina ampeleke nyumbani kwake kwa usafiri wake wa pikipiki ili aweze na kupafahamu pia.
Sabrina akakubali kwavile muda ulishaenda tayari.
Francis alimfikisha Sabrina nyumbani kwake na kumuaga kwavile muda ulikuwa tayari umeshaenda sana.
Aliingia ndani na kwenda kukaa karibu na Jeff ambapo akabambana na maswali ya Jeff.
"Mbona umechelewa sana leo mamy?"
"Kuna mtu nilikuwa nazungumza naye, yani mwanangu mapenzi haya mi yataniua jamani"
"Kwanini unasema hivyo mamy?"
"Kwakweli sielewi yani sielewi kabisa, sijui nani ananipenda kweli sijui nani ananidanganya. Yani wale wale waliofanya niyachukie mapenzi eti leo wanakuja na kusema kuwa wananipenda sana. Hata sijui ni nani wa kuwa nae kati yao!"
"Nikwambie kitu mamdogo?"
"Niambie mwanangu."
"Kati ya hao watu usimkubali hata mmoja mamy"
"Kwanini unasema hivyo?"
"Watakuona mjinga halafu wao ndio washindi wakati washakuumiza sana. Huu ni muda wa wewe kuwaumiza wao"
"Kuwaumiza wao kivipi?"
"Unatakiwa uwe na mtu mwingine kabisa, mtu ambaye atakusahaulisha kila kitu kuhusu wao. Unatakiwa kuanza upya maisha yako, sitapenda kuona ukilia au ukiteseka sababu ya mapenzi mama angu"
"Sasa nitafanyeje hapo?"
"Unatakiwa uwe na mtu mwingine"
"Mwingine yupi?"
"Kesho nitakuonyesha mamy"
"Aaah sitaki kesho, nataka uniambie leo"
"Kweli unataka leo?"
"Ndio niambie leo"
"Haya inuka nikakuonyeshe"
Jeff alimshika mkono Sabrina mpaka chumbani kwa Sabrina, kisha akamwambia
"Nenda ukakae pale kwenye kitanda chako nikuonyeshe"
Sabrina akamuangalia Jeff kwa mshangao na jicho la hasira.
Itaendelea
No comments:
Post a Comment