Muda ulipofika Sabrina alijiandaa ili kwenda
kuonana na Prince J.
Alipofika eneo la tukio, akaangaza macho ili
aweze kumuona Prince J.
Macho yake yakagongana na watu wawili mbele
yake, Sam na Jeff.
Sabrina akawashangaa na kujiuliza kuwa ni nani anayemchezea akili kati yao, alihisi labda kuna mchezo unaendelea pale
"Inawezekana Prince J ni Jeff kweli! Hapana Jeff hawezi kunichezea mchezo kama huo, na je inawezekana ni Sam kweli! Mmh inamaana Sam ameshindwa kunitongoza kawaida hadi atumie njia ya facebook kweli! Hapana, ila nitajua ukweli tu"
Alisimama kamavile anayengoja kuwaona wote wawili wakisogea eneo alilokuwepo, na kweli wote wawili wakasogea eneo lile.
Sabrina alianza kwa kumuhoji Jeff,
"Umefata nini huku?"
"Nina maagizo yako toka kwa mama na ndiomana nimekufata"
Sabrina akamuangalia Jeff kwa jicho kali sana na kumuuliza tena,
"Eeh umejuaje kama nipo huku?"
"Ulinitumia ujumbe kuwa unatoka kidogo na kusema unakuja huku, kwahiyo mi nikaja kukubahatisha tu"
"Kwanini usingenisubiria nyumbani?"
"Jamani mamdogo, kama nimekosea kukufata basi unisamehe kisha Jeff akaondoka zake"
Sabrina alimuangalia Jeff hadi alipoishia, na kujisemea
"Haka katoto hakana akili kwakweli"
Akamuangalia Sam sasa na kumuuliza,
"Eeh nawe umejuaje kama nipo hapa?"
Ila Sam alikuwa na hasira sana, alimuangalia Sabrina kwa jicho kali na kumwambia,
"Nimekuja kumuona huyo Prince J wako"
Sabrina akashtuka na kumuangalia vizuri Sam, kisha akamuuliza
"Umejuaje kuhusu Prince J?"
"Kwakweli sikuweza kuamini kama wewe Sabrina ungeweza kufanya upuuzi wa namna hii, yani unachat na watu kwenye facebook! Aah umenisononesha sana"
Sabrina bado hakumuelewa Sam na kuendelea kumuangalia tu,
"Sam, sikuelewi lakini"
"Hunielewi eeh!! Angalia uchafu wako sasa"
Sam akamfungulia Sabrina mtandao wa facebook kwenye simu yake na kumfanya Sabrina atambue kosa alilolifanya ni kuwa alisahau kutoka kwenye mtandao alipotumia simu ya Sam.
"Angalia sasa, na huyo mpuuzi wako wa kuitwa Prince J amekutumia ujumbe tena angalia vizuri"
Sabrina akaona ujumbe toka kwa Prince J uliosema,
"Samahani mpenzi, nimepatwa na dharura kidogo kwahiyo sitaweza kufika eneo la tukio ila nakupenda sana Sabrina mpenzi wangu"
Sam alikuwa akimuangalia Sabrina kwa jicho la hasira sana huku akifoka,
"Nilikuthamini Sabrina, nilikuheshimu na kukuona ni mwanamke wa pekee kwenye hii sayari. Sikuamini wala kufikiria kama ungeweza kufanya upuuzi wa namna hii na ndiomana nikaamua kuja ili niweze kujionea mwenyewe kwa macho. Na huyo Prince J wako ana bahati sana kwamaana ningemkuta ningemfumua ubongo wake, na leo nimetembea na bastola kabisa kwaajili yake"
Akainua shati lake vizuri na kumfanya Sabrina aione ile bastola na kutetemeka.
"Haya twende kwenye gari nikurudishe kwako"
Sabrina hakuweza kusema chochote kwani uoga ulimshika na alikuwa akitetemeka tu.
Alienda kupanda gari na safari ya kurudishwa nyumbani kwake ilianza.
Alipofika kwake, moja kwa moja Sabrina akaenda chumbani kwake na kuiona siku hiyo kuwa mbaya sana kwake.
Alijiuliza maswali mengi sana,
"Mbona huyu Sam simuelewi jamani, ana lengo gani na mimi? Ndio kusema ananipenda au ni kitu gani? Mbona simuelewi, na kwanini achukie kiasi kile?"
Sabrina hakupata jibu, akatamani aingie facebook ili amseme Prince J ila alishindwa kwani alijua wazi atakapoingia tu basi Sam ataona tena kila kitu, ikabidi atulie na kutafuta usingizi tu ili apoteze yale mawazo yanayomtatiza.
Kesho yake asubuhi na mapema Sabrina akajiandaa kwaajili ya kwenda kazini, na kwajinsi Sam alivyochukia jana yake Sabrina akajua kuwa hawezi kuja kumchukua tena kwenda nae kazini.
Ila Sabrina alipotoka, alimkuta Sam akiwa nje anamngoja.
Akamsalimia na kupanda kwenye gari halafu safari ikaendelea.
Sabrina akatamani kumuuliza Sam swali moja tu kuwa "je unanipenda!"
Ila kila alipotaka kumuuliza mdomo wake ukasita na kuona kamavile atajibiwa vibaya kwahiyo akakaa kimya hadi walipofika ofisini.
Sabrina alipokuwa ndani ya ofisi, na leo akapata ugeni pia.
Mgeni wake alikuwa ni kaka yake James.
Sabrina akafurahi sana kutembelewa na ndugu yake pale ofisini.
Wakaongea kiasi kisha James akaaga na kumfanya Sabrina amtoe kidogo kaka yake hadi nje ya ofisi.
Kufika pale nje wakakutana na ndugu wa Sam ambaye naye alikuwa anakuja pale ofisini, Sabrina akamkaribisha kwa furaha kabisa
"Karibu Joy"
Joy naye akatabasamu kiasi na kuendelea kwenda kwenye ofisi ya Sam.
Kisha Sabrina akamuangalia kaka yake na kumwambia,
"Kaka umemuona yule mdada?"
"Si yule uliyemuita Joy hapa"
"Ndio huyo huyo"
"Kafanyaje kwani?"
"Yani yule mdada, ana baba yake unafanana nae huyo balaa halafu na yeye anaitwa James, nitawakutanisha siku moja"
"Itakuwa vizuri, si unajua duniani wawili wawili tena"
Kisha James akamuaga Sabrina na kuondoka zake.
Walivyotoka ofisini kama kawaida Sam alimrudisha Sabrina nyumbani kwake, ila leo Sabrina leo hakutaka kukaa ndani kwake bali alitaka kujua ukweli japo kwa kifupi tu kumuhusu Sam, na aliona mtu pekee wa kumwambia ni yule muhudumu wa baa ambaye amewahi kumdokeza Sabrina kuhusu Sam.
Kwahiyo Sam alipoondoka, Sabrina akaitumia nafasi hiyo kwenda kwenye ile baa ili amuhoji yule muhudumu kiasi.
Sabrina alipofika kwenye ile baa aliangaza kila mahali ili aweze kumuona yule muhudumu na kwa bahati akamuona.
"Samahani dada, unanikumbuka?"
"Mmh! Sura yako sio ngeni sana ila sikumbuki nimekuona wapi"
Sabrina akaamua kumuelezea kuhusu siku aliyoenda kwenye ile baa na Sam, na jinsi huyu dada alivyomwambia mwanzo.
"Aah! Nimekukumbuka dada, si ndio ulikuja na yule kibosile"
"Ndio, niambie ulichokuwa unataka kuniambia"
Yule muhudumu akawa anasita sita, Sabrina akagundua anachotaka yule dada.
Kisha akafungua pochi yake na kutoa elfu tano na kumpa ili amueleze vizuri.
"Ni hivi dada yangu, yule kaka huwa ana michezo michafu"
"Michezo michafu! kivipi?"
"Yani akikuchukua na kukupeleka ndani kulala naye, atakachokufanyia humo ndani hakifai"
"Anakufanyia mambo gani kwani?"
Yule dada akaitwa na kuamua kumuaga Sabrina,
"Umekuja muda mbaya, siku ukiwahi mapema nitakusimulia vizuri"
Kisha akaondoka na kumfanya Sabrina atafakari bila hata ya majibu na kuamua kurudi nyumbani kwake.
Alipoingia ndani kwake alimkuta Jeff akiangalia video, moja kwa moja Sabrina akamwambia Jeff
"Najua wewe ni mtundu sana, nataka unisaidie kitu"
"Kitu gani hiko?"
"Mfano niliingia facebook kwa simu ya mtu mwingine na nikasahau kutoka, halafu sitaki yule mtu aone meseji zangu. Je nifanyeje?"
"Kitu kidogo sana hicho, nipe simu yako"
Sabrina akampa Jeff simu ili aweze kumrekebishia, baada ya dakika mbili Jeff alimrudishia Sabrina simu
"Tatizo lako limeshaisha hapo"
"Yani bila hata kubadili neno la siri?"
"Wewe usijali, tatizo hapo limeisha niamini mimi"
Sabrina akaingia chumbani kwake na kumtumia ujumbe Prince J huku akingoja kuona kama Sam naye atazipata.
Baada ya muda kidogo simu yake ikaita, mpigaji alikuwa ni Sam na kumfanya Sabrina aogope kwani alihisi Sam kaona huku akimlaumu Jeff kuwa amemdanganya.
Ila alipopokea simu ya Sam aliulizwa swali moja tu,
"Kwanini umeifunga facebook yako kwangu nisiione?"
"Sijaifunga mbona, labda matatizo ya mtandao tu"
Sam hakujibu kitu zaidi ya kukata simu na kumfanya Sabrina acheke na kufurahia ushindi wake.
Wakati akifurahia hayo, ujumbe ukaingia toka kwa Prince J
"Mpenzi umekula?"
Sabrina akafurahi kwani aliona kuwa Prince J ni mtu anayemjali sana,
"Bado sijala, ila sijisikii kula leo"
"Tafadhari mpenzi nakuomba ule, usipokula wewe unaniumiza mimi. Nakuomba mpenzi wangu, au nikuandalie chakula mpenzi?"
Sabrina akatabasamu na kujikuta akiinuka pale kitandani na kwenda sebleni ambako alimkuta Jeff akiwa makini na simu yake tu.
Sabrina akapitiliza moja kwa moja jikoni ambako Jeff alimfata na kumuuliza
"Unataka kufanya nini mamy?"
"Nataka kupika chai"
"Acha nikupikie mie mamy"
Sabrina akamuangalia Jeff kisha akamuacha mule jikoni na kurudi sebleni.
Jeff alipomaliza, alimuandalia Sabrina ile chai ili aweze kunywa kama alivyohitaji.
Alipomaliza kunywa alirudi chumbani kwake, na moja kwa moja aliingia kwenye mtandao apate kumuaga Price J, akakutana na ujumbe toka kwake
"Uwe unaniambia mapema mpenzi ili nikuandalie chukula kizuri zaidi"
"Usijali, nina mwanangu hapa naye ananiandalia vizuri sana"
"Kuna kitu hujui Sabrina"
"Kitu gani?"
Prince J akatoweka hewani na kumfanya Sabrina akose jibu na kuamua kulala tu.
Kulipokucha, Sabrina aliamka na kujiandaa kwaajili ya kwenda kazini.
Kama kawaida Sam alikuwa pale kwaajili ya kwenda nae kazini.
Walisalimiana na kuianza safari, lakini Sabrina hakuthubutu kumuuliza Sam kuhusiana na yote aliyoyasikia.
Sam akavunja ukimya na kumwambia kitu Sabrina,
"Nimepata safari ya gafla Sabrina kwahiyo kesho natarajia kusafiri, naenda Nairobi"
"Sawa bosi, ila kweli ni safari ya gafla hiyo"
Wakaendelea na maongezi mengine mpaka pale walipofika ofisini. Halafu kila mmoja akaendelea na kazi zake.
Mchana wa siku hiyo, Sabrina alijihisi vibaya na kuomba ruhusa ya kurudi nyumbani kwake.
Ingawa Sam hakuwepo mchana huo lakini Sabrina hakukataliwa kuondoka na kwenda kupumzika.
Alifika nyumbani kwake na kujilaza kwenye kiti, Jeff akamfata pale karibu
"Nini tatizo mamy?"
"Kichwa kinaniuma sana"
"Punguza mawazo mama angu, ni mawazo hayo ndio yanakuumiza kichwa hiko"
Kisha Jeff akainuka na kwenda kumletea maji Sabrina ili apate kutuliza maumivu kiasi.
Sabrina alikunywa yale maji na kwenda kulala.
Muda kidogo akafika mgeni wa Sabrina pale nyumbani na kumkuta Jeff,
"Samahani, eti Sabrina yupo?"
"Hata hayupo"
"Mmh mbona nimeongea nae muda si mrefu akasema yupo nyumbani na yeye ndio kanielekeza hapa"
"Basi alichanganya mada tu ila hata hayupo"
Yule mgeni alisita kidogo na kuondoka zake.
Jioni ilipofika Sabrina alitoka ndani na kumuuliza Jeff,
"Hakuna mtu wa kuitwa Fredy aliyekuja hapa kuniulizia leo?"
"Mmh hata sijamuona mtu yeyote"
"Basi kanidanganya, alisema atakuja kumbe hana lolote. Kashanikera tayari"
Jeff alikaa kimya tu na kuendelea na mambo mengine mpaka pale usiku ulipoingia na kila mmoja kwenda kulala akiwa na mawazo anayoyajua yeye.
Siku ya leo Sabrina aliamka asubuhi na mapema ili kuwahi kujiandaa kwani alijua wazi kuwa siku hiyo lifti haipo kwavile Sam alimwambia jana kuwa atasafiri.
Alipomaliza kujiandaa akatoka nje, akashangaa kuona kuna gari imepaki pale nje kwake, halafu dereva akashuka baada ya kumuona.
"Nimetumwa na Bosi Sam kuwa nije nikuchukue nikupeleke kazini"
Sabrina alifurahi sana na kupanda kwenye lile gari na safari kuanza.
Wakiwa wanaendelea na safari, Sabrina akashangaa kuona lile gari halielekei njia ya ofisini kwao.
Akamshtua yule dereva na kumuuliza,
"Mbona hunipeleli huko ofisini?"
"Hatuendi ofisini ndio, kuna mahali nakupeleka"
"Ni wapi huko?"
Yule dereva hakujibu ila alianza kucheka.
Itaendelea
No comments:
Post a Comment