Sabrina akashtuka sana baada ya kumuona mtu mwingine aliyekuja na hao watu akiwa amevalia mavazi ya kipolisi.
Sabrina alikuwa kama mtu aliyepigwa na bumbuwazi kwani hakuelewa kabisa kuwa kwanini Sia aje na hao watu, na kwanini aje na polisi!
Wakati Sabrina akistaajabu hayo, Sia akasogea karibu na kuwaambia wale wenzie
"Sabrina ndio huyo hapo"
Yule polisi akamsogelea Sabrina na kumuuliza yule binti ambaye mimba ilitoka
"Msichana mwenyewe ndio huyu?"
Yule binti akajibu huku akiwa kama machozi yanamlenga lenga,
"Ndio huyo huyo"
Yule askari, akamshika Sabrina na kumwambia,
"Upo chini ya ulinzi, unahitajika kituoni"
Sabrina hakuelewa kitu kawani alikuwa anashangaa tu na kuona mambo yale kama ni ndoto tu kwake.
Alijikuta akiuliza,
"Kwani nimefanyaje jamani!"
Yule askari akamjibu kwa ukari,
"Utajua huko huko kituoni"
Joy nae muda wote alikuwa akishangaa tu kwani hakuelewa kabisa kuwa ni kitu gani kinaendelea, akazuia mwanae asipelekwe kituoni lakini ilishindikana.
Alihisi kuchanganyikiwa kwakweli, akamuangalia Sia na kumuuliza
"Yani wewe ndio unamfanyia hivi rafiki yako?"
Ila Sia hakumjibu chochote mama huyu na safari ya kwenda kituoni iliendelea.
Walipofika, moja kwa moja wakampeleka Sabrina rumande na kumfanya Joy azidi kuchanganyikiwa.
Akamfata askari mmoja na kumuuliza,
"Kwani binti yangu amefanya nini jamani?"
"Inamaana hujui kama mwanao ameua!"
"Ameua? Kamuua nani?"
Yule askari akacheka, kisha akanyoosha kidole huku akimuonyesha Joy yule msichana ambaye alikuwa mjamzito,
"Umemuona yule binti pale! Alikuwa na mimba yule, sasa inasemekana mwanao alikuwa na mahusiano na mchumba wa yule binti. Mwanao asivyokuwa na akili sasa, alimuibia mwenzie mwanaume halafu siku hiyo kamkuta mwenzie njiani nasikia akamsukuma na kumponda na kitu kizito tumboni kisha akakimbia. Ndio hapo mimba ya huyo binti ikatoka, je sio uuaji huo?"
Joy alitulia kimya huku machozi yakimlengalenga, alijisikia vibaya sana kusikia hivyo vitu ambavyo ni tofauti kabisa na alivyosimuliwa na mwanae kabla.
Joy akainuka pale na kuomba kuzungumza kidogo na mwanae, kwa bahati wakampa nafasi hiyo.
Sabrina alipoitwa kwa mama yake alikuwa akilia tu na kufanya ashindwe kabisa kuzungumza na mama yake hata pale walipomrudisha tena rumande alikuwa akilia tu.
Joy ilibidi ajikaze na kujipa moyo ili aweze kufanya kitu cha kumsaidia mtoto wake.
Akamfata yule binti inayesemekana kuwa mimba imetoka.
"Mwanangu, unauhakika kweli Sabrina alikusukuma na kukupiga na kitu kizito tumboni?"
"Ndio, Sabrina kaniulia mwanangu"
Huku akijiliza liza pale.
Joy alimuangalia tu huyu binti kisha akamwambia,
"Kama uyasemayo yana uongo ndani yake basi jua kwamba Mungu anatambua hilo naye ndiye atakayetoa hukumu"
Kisha Joy akaondoka eneo lile, akatafuta eneo la utulivu ili aweze kumpigia simu mumewe na kumwambia yaliyojiri.
Sabrina alikuwa akilia tu huku akiwaza yote yaliyotokea nyuma, hakuelewa kwanini rafiki yake Sia amegeuka kiasi kile na kuamini maneno ya watu kuwa rafiki anaweza kugeuka na kuwa adui kwa dakika moja tu.
Sabrina hakuweza kukaukwa na machozi, alikumbuka hadi jinsi Fredy alivyokuwa akimzuia kuwa asiende ila kwa kiburi chake akaenda na kukutana na hayo yaliyomkuta sasa.
Alitamani siku zirudishwe nyuma ili awe Sabrina mpya ila ndio hivyo tena alikuwa rumande tena kwa kosa asilohusika nalo.
Alijikuta akiyachukia mapenzi, na kujiapia kule rumande kuwa hatokuja kupenda tena katika maisha yake yote yaliyobaki.
Khabari ya mwanae kupelekwa rumande ilimsikitisha sana Deo, na vile alivyoambiwa kuwa dhamana imeshindikana kwahiyo mtoto wake atalala rumande kulimfanya aombe likizo ya dharura ili aweze kwenda kumsaidia mtoto wake aliyejua wazi kuwa hana hatia.
Sakina nae alisikitishwa sana na khabari hii, alijua wazi kuwa Sabrina amesingiziwa tu.
Alikuwa akijisemea tu,
"Maskini Sabrina sijui ana damu ya kuchukiwa jamani!! Wachawi wamemfatilia wee hadi basi, saivi kaanza kufatiliwa na watu wa kawaida hadi kufikia hatua ya kumsingizia mmh!"
Kumbe Joy alikuwa akimsikiliza Sakina kwa makini na kujikuta akisema,
"Umeona eeh! Mwanangu anaonewa jamani hata sijui amewakosea nini watu hawa hadi wanafikia kumfanyia hivi mtoto wangu!!"
Wote wakajikuta wakisikitika kwa pamoja kwani jitihada zote walizokuwa wakizifanya kwaajili ya dhamana ziligonga mwamba na kufanya siku hiyo Sabrina alale rumande.
Joy aliumia sana tena sana hata hakutamani kurudi nyumbani kwake, alitaka alale pale pale polisi ila Sakina ndiye aliyefanya kazi ya kumpooza na kumbembeleza.
Sabrina alizidi kuumia kuona vile anakandamizwa kwa kosa ambalo hakulitenda hata kidogo na wakizidi kumwambia kuwa amelitenda.
"Ila ni Mungu pekee anayejua hatma yangu, ni Mungu pekee atakayenihukumu kwa haki juu ya hili"
Moyo ulimuuma zaidi pale alipogundua kwamba siku hiyo atapaswa kulala hapo rumande sababu dhamana yake imekataliwa.
Sabrina alilia muda wote, hakujisikia kunyamaza kwani moyo ulikuwa ukimuuma tu na kujiona kama mtu mwenye mkosi katika maisha yake, ukizingatia kile chumba kilikuwa na mbu na harufu ya mikojo ndiyo ilitawala mule ndani na kumfanya Sabrina ajisikie vibaya zaidi.
Deo hakutaka kupoteza muda na kuamua kuchukua gari yake na kusafiri siku hiyo hiyo ili aweze kuwahi hata kwa kesho na kumsaidia mtoto wake.
Wakati yupo njiani, kuna jamaa mmoja alionekana kupatwa na matatizo kwenye gari yake njiani na kuliweka pembeni, alionekana kusimamisha kila gari inayopita ili kuweza kupata msaada ila gari zote zilimpita kwenye eneo lile, kwahiyo lilipopita gari la Deo nalo akalisimamisha.
Deo alitamani kutokusimama kwani aliona kuwa anacheleweshwa tu, ila huruma ikampata na kusimama, kisha akamuuliza yule mtu
"Nini shida hapo kaka?"
"Nina tatizo bhana na gari yangu hapa, sijui kama utaweza kunisaidia"
"Tatizo ni kitu gani?"
"Tairi langu la mbele limepata pancha, ubaya ni kuwa sina hata tairi la ziada"
Deo akaenda kwenye buti la gari yake na kutoa tairi, kisha akamwambia yule bibi
"Mimi ninalo, chukua hili"
Kwakweli yule baba hakuamini kupata msaada kiurahisi kiasi kile,
"Dah, nashukuru sana na Mungu akubariki. Ngoja nijaribu kuliweka, ila unaweza kwenda sasa usije ukachelewa zaidi"
"Usijali, ngoja tusaidiane kuliweka ili tuondoke kwa pamoja. Eneo sio zuri hili, nisije nikafika mbele na kusikia mengine bure"
Kisha Deo akaanza kumsaidia yule jamaa, yani alijikuta tu akipatwa na moyo wa kumsaidia.
Walipomaliza pale, ikabidi wafahamiane na kupeana mawasiliano yao
"Naitwa Deo"
"Nami naitwa James, itabidi unipe namba zako Deo yani hapa hata simu yangu haipo hewani sababu haina chaji na namba zake sijazishika"
Ikabidi Deo amuandikie yule James namba zake kwaajili ya kufahamiana zaidi.
Kisha kila mmoja akapanda kwenye gari yake na safari kuendelea.
Hali ya Sabrina kwenye kale kachumba haikuwa nzuri kwakweli, bado alikuwa na matatizo mule ndani na kila kilichoendelea hadi palipokucha.
Alimsikia mama yake akizungumza nje ya kile kituo cha polisi na kugundua kwamba mama yake alikuwa mtu wa kwanza kufika pale kushinda hata watu wote.
"Naombeni jamani hata nimuone mtoto wangu"
"Hairuhusiwi mama, subiri muda ufike"
"Msinifanyie hivyo jamani, mwanangu anahitaji uwepo wangu kwasasa. Naomba nimuone tu"
Malalamiko hayo ya mama yake yalimfanya Sabrina azidi kuumia moyo mule kwenye kile kichumba.
Joy alizidi kuwaomba lakini walimkatalia kabisa, yote hayo yalifanywa kwa lengo la kumtesa Sabrina tu ukizingatia ndugu wa yule binti ambaye mimba ilitoka walishafanya mambo yao pale kwenye kituo na Kuhonga baadhi ya askari ili kumfanya Sabrina ateseke na ndiomana Joy hakusikilizwa kabisa.
Joy aliona itakuwa vyema kama ataenda kumtafutia mwanae chakula kwanza, kwa kifupi Joy alikuwa amechanganyikiwa kabisa.
Njiani wakati anaenda kumtafutia mwanae chakula akakutana na Sakina.
"Najua umeshachanganyikiwa dada yangu, ila usijali chakula mie nimekibeba"
"Ni kweli nimechanganyikiwa, tena nimechanganyikiwa kabisa kabisa"
Wakaenda tena pale kwenye kituo cha polisi na kuanza kumuomba askari ili awatolee Sabrina waweze kumpa kile chakula,
"Hairuhusiwi, labda mnipe hiko chakula nimpelekee. Kesi ya mtoto wenu ni kubwa sana. Sitaki kufanya makosa tena"
Wakamuomba sana, ila yule askari alikataa na kuamua kumpa kile chakula ili akampe Sabrina.
Yule askari akachukua kile chakula na kumpelekea Sabrina kwenye kale kachumba ambapo alikuwa na watuhumiwa wengine kama watatu hivi, hao watuhumiwa wengine ndio waliokula kile chakula.
Joy na Sakina wakajaribu kufatilia ili wajue hatma ya ile kesi ya Sabrina,
"Mtoto wenu ana hatia sana, na ushahidi upo wa kutosha. Kwanza kabisa alikimbia eneo la tukio baada ya kulitenda, huo ni ushahidi tosha kuwa alitenda. Halafu kila tukitaka kumuhoji analia tu, inaonyesha wazi anajutia kosa alilolifanya ila tu hataki kukubali ukweli kuwa amelifanya"
Ndivyo walivyojibiwa na yule askari, akaendelea kuongea
"Hapa ni moja kwa moja segerea, tena kesi ya mauaji hiyo ataenda kufungwa huko maisha"
Joy alihisi kama moyo wake ukitaka kupasuka kabisa, ikiwa ameshindwa kukabiliana na hali ya mwanae kulala pale polisi kwa usiku mmoja je ataweza kukabiliana na hiko kifungo cha maisha kwa mwanae!!
Joy alihisi kama hiyo hukumu itatolewa kwa mtoto wake basi na yeye ndio itakuwa mwisho wa maisha yake.
Walishinda pale pale kituo cha polisi huku wakiwangoja ndugu wa yule dada ambaye mimba ilitoka kujua hitimisho la ile kesi inayomkabili Sabrina.
Deo alirudi nyumbani kwake na kushangaa kukuta hakuna mtu ila milango yote iko wazi,
"Kweli huyu mke wangu ameshachanganyikiwa jamani mmh!"
Na yeye hakutaka kupoteza muda, nia yake ilikuwa ni kujiandaa kidogo na kwenda huko kituoni.
Wakati anajiandaa, akapigiwa simu na namba ngeni. Akaipokea,
"James anaongea hapa, yule mtu uleyemsaidia njiani"
"Aah kumbe ni wewe, nipe khabari ndugu yangu"
"Salama tu, nishafika nyumbani kwangu. Najiandaa hapa kwenda kazini kidogo ila naomba jioni nikutafute"
"Sawa hakuna tatizo"
Kisha akakata ile simu na kumalizia mambo yake kisha kuanza safari ya kwenda kwenye kituo cha polisi alichoambiwa na mkewe jana.
Alipofika hakuwakuta, ikabidi aulize.
Akajaribu kumpigia mkewe simu lakini hakupatikana, ikabidi awafate askari wa pale na kuwaeleza kisha wakamwambia,
"Ile kesi imehamishwa na kupelekwa kituo cha kati kule"
Deo, akaondoka eneo lile na kwenda alipoelekezwa.
Alipofika, aliwaona Joy na Sakina wakiwa wamekaa chini ya mti pale kituoni, ikabidi awafate.
Joy alipomuona mume wake, akapata nguvu kiasi huku machozi yakiendelea kumtoka.
"Hebu nielezeni kwanza ili nijue pa kuanzia"
Joy akamuelezea mume wake kila kitu hadi vile alivyoelezewa na mwanae wakati wapo nyumbani.
Deo akawa amepata picha kichwani kuwa ni wapi waanzie na wapi waishie.
"Ngoja nikamuulizie mkubwa wa kituo kwanza"
"Mkubwa wao hayupo, kuna msaidizi tu. Ila huyo naye hataki hata kutusikiliza"
"Na ilikuwaje mkaamishiwa huku?"
"Nahisi ni njama tu Deo, yani kule hata hatukukaa sana ile jana wakatuhamishia huku utafikiri mwanangu ndio muharifu wa kwanza duniani. Hata dhamana wakatukatalia"
Deo kuna kitu kikawa kinajengeka katika akili yake, alijua wazi kuwa mkewe alisahau kumwambia kama walihamishwa kituo ile jana sababu ya kuchanganyikiwa.
Deo akawaacha pale na kuanza kushughulikia kesi ya mwanae, alitaka kuhakikisha kwamba siku hiyo mwanae anapata mdhamana hata kama siku inakaribia kuisha sababu alichelewa kufika.
Alienda kwenye ofisi ya mkuu wa kituo na kuambiwa angoje nje, baada ya muda aliruhusiwa kuingia.
Alishtuka sana kumuona mkuu wa kituo ni mtu waliyeonana naye kabla,
"Kheee bwana Deo, umejuaje kuwa nipo huku? Maana hapa nikakumbuka ile ahadi yangu na kutaka nimalize nikupigie"
"Tatizo mwanangu bhan"
"Kafanyaje!!"
Deo akamuelezea vile alivyoelezewa na mke wake.
"Dah! Vijana wetu hawa wanamatatizo kwakweli, ni ujana tu unawasumbua. Ngoja waniitie hapa huyo binti yako nimuhoji mwenyewe. Sababu maelezo unayonipa na niliyopewa ni tofauti kabisa"
Yule mkuu wa kituo akaamuru Sabrina apelekwe ofisini kwake, kwahiyo askari akaenda kumtoa Sabrina.
Sabrina alikutwa hajitambui kwenye kile kichumba, inaonyesha wazi kuwa alilia sana hadi kupoteza fahamu kwahiyo walimtoa kama mzoga.
Itaendelea
No comments:
Post a Comment