Wakati Sabrina akiwaza hayo, mara akatokea mtu
nyuma na kumsukuma Sabrina na kufanya
amwangukie yule dada mwenye mimba.
Sabrina alijishangaa tu akiwa juu ya tumbo la yule dada mjamzito huku yule dada akilalamika kuwa anaumia.
Sabrina akainuka upesi, akashangaa kuona watu wamejaa eneo lile kwa ule muda mfupi tu.
Wakatokea wadada wawili waliokuwa na jazba sana, tena walikuwa ni wadada wale wale waliopiga Sabrina alipokuwa kule kwa Japhet.
Akaona hapo akiendelea kusimama atapigwa hadi kufa, Sabrina alitumia sekunde tu kupata wazo la kukimbia.
Muda huo huo akawachoropoka wale watu na kuanza kukimbia, huku nyuma walikuwa wakimkimbiza pia.
Bahati nzuri ilitokea gari na kusimama, kisha mlango wa nyuma wa lile gari ukafunguliwa ili Sabrina aweze kuingia.
Naye Sabrina akaona wazi kuwa ule ndio utakuwa usalama wake na kuingia kwenye lile gari kisha dereva akaondoa lile gari.
Sabrina alikuwa anahema sana kwani hakuamini kama amesalimika eneo lile la tukio, na kuanza kuwashukuru wale watu wa kwenye lile gari,
"Asanteni jamani, asanteni sana hata siamini kama nimesalimika"
Alikuwa akitetemeka kabisa, akamsikia mmoja wa watu mule kwenye lile gari tena ni yule wa pembeni yake akimwambia,
"Nilikwambia Sabrina nikupeleke kwenu ukakataa, umeona faida ya ubishi sasa?"
Sabrina akamuangalia kwa makini, kumbe alikuwa ni John,
"Khee kumbe ni wewe John!!"
"Ndio ni mimi, pole sana kwani imekuwaje?"
"Hata sielewi, yani sielewi kabisa kabisa sielewi"
Sabrina alijihisi kama kuchanganyikiwa kabisa na hakuelewa kitu kingine zaidi ya kujishangaa tu.
Wakamuacha akili imtulie kwanza huku wakimpeleka kwao.
Walipofika kwao, John alishuka na kumfungulia mlango Sabrina.
"Pole sana Sabrina, hao wawili mbele ya gari ni rafiki zangu. Nimeshindwa hata kukutambulisha vizuri, ila nenda ukapumzike kisha nitapanga siku ya wewe kufahamiana nao"
Sabrina akaitikia na kuingia kwenye nyumba yao akiwa kajichokea kabisa, mama yake alimshangaa kwa ile hali aliyorudi nayo nyumbani,
"Mbona umenywea hivyo wakati uliondoka na furaha mwanangu?"
"Majanga yamenikuta njiani wakati narudi mama yangu"
"Majanga gani hayo mwanangu"
Sabrina akamsimulia alivyomuangukia yule dada mjamzito ila hakuthubutu kusema kama alishawahi kuonana nao kabla.
"Pole mwanangu, ila sio kosa lako. Ni kosa la huyo aliyekusukuma, usiwaze sana mwanangu. Sawa eeh!! Nenda ukapumzike tu kwasasa"
Kwavile kigiza kilishaingia, Sabrina akaenda kuoga na kulala kwani mawazo yalishamjaa tayari.
Akiwa usingizini, ikamjia ndoto akiwa amezungukwa na rafiki zake huku wakimsema kwa kupokezana maneno
"Yani Sabrina umeua! Tena umeua kiumbe cha Mungu kisichokuwa na hatia!"
"Nakwambia ukweli Sabrina, kwa kosa hili kamwe huwezi kusamehewa na Mungu"
"Umetia aibu Sabrina, yani mambo ya mapenzi unayapeleka kwenye mimba aliyobeba mwanamke mwenzio!"
"Unadhani huyo mwanaume atakuwa na wewe kwa mtindo huo? Hakuna mwanaume anayependa kuoa mwanamke muuaji, hata kama alikupenda vipi hawezi kukutaka tena kwa kumuulia mtoto wake"
Wote walikuwa wakimshambulia kwa maneno, mara akatokea rafiki yake Sia na kuwaambia,
"Jamani, dawa ya mtu muuaji ni kuwa naye auawe tu. Kwahiyo huyu Sabrina tusimwache hivi hivi kwani ataendelea kusumbua watu"
Halafu likatokea kundi la watu wakiwa wamebeba silaha mbali mbali, wengine mawe, visu, mapanga, fimbo na wote wakitaka kumpiga Sabrina.
Akashtuka kwenye ile ndoto huku jasho jingi likimtoka, alikaa na kujiuliza maswali bila majibu.
"Inamaana mimba ya yule dada ikitoka, muhusika ni mimi? Lakini mimi kosa langu hapo ni lipi jamani? Eeh Mungu nisaidie mja wako"
Kisha akainuka na kwenda kujimwagia maji kwani joto kali lilitembea mwilini mwake na jasho jingi kumtoka.
Aliporudi kulala hakuweza kupata usingizi hadi panakucha, kwani mawazo yalimuandama zaidi na kumkosesha usingizi kabisa na kumfanya auone usiku ni mrefu.
Asubuhi alimuuliza mama yake kuhusu masomo yake.
"Hivi mama, mlisema nitaenda lini chuo?"
"Usiniambie umeshachoka kuwa hapa nyumbani!"
"Nimechoka ndio mama, nataka nikasome"
"Kama umeamua hivyo basi ni vizuri sana, nitamwambia baba yako kuwa upo tayari sasa"
"Ila mama, mfano yule dada niliyemuangukia jana, mimba yake ikatoka je wa kulaumiwa nitakuwa mimi?"
"Hakuna wa kulaumiwa hapo mwanangu, laiti kama ungemjua aliyekusukuma basi yeye ndiye aliyepaswa kulaumiwa ila sio wewe. Usiwaze sana mwanangu, yote muachie Mungu tu"
Sabrina alikubaliana na mama yake ila bado alikuwa na mawazo mengi sana.
Sabrina akiwa ametulia sasa, simu yake iliita. Alipoichukua na kuangalia akashtuka sana na moyo wake ukafanya paaa, kwani mpigaji alikuwa ni Japhet.
Moja kwa moja Sabrina alijiuliza kuwa Japhet alikuwa na nia gani.
Akapokea simu huku anatetemeka kwani ni muda mrefu hakuwasiliana na Japhet,
"Uko wapi Sabrina?"
"Nipo nyumbani"
"Nakuja"
Kisha akakata simu na kumfanya Sabrina apatwe na maswali mengi bila ya majibu ya kueleweka.
"Mmh anakuja kufanya nini? Au kuniuliza? Mmh naogopa"
Mawazo yakamzidi sasa.
Muda kidogo, mama wa Sabrina akamuaga Sabrina kuwa anatoka,
"Unaenda wapi kwani mama?"
"Naenda kwenye vikoba vya kinamama ila sitakawia sana kurudi"
Joy akaondoka na kumuacha binti yake mwenyewe pale nyumbani kwao.
Alipotoka tu, zikapita dakika chache Japhet nae akawasili pale kwakina Sabrina.
Sabrina akamkaribisha Japhet ndani kwao ila Japhet alionekana wazi kutokuwa na furaha. Na swali la kwanza kumuuliza Sabrina lilikuwa,
"Kwanini umenifanyia hivi Sabrina?"
"Kwani nimekufanyia nini Japhet?"
"Usiulize wakati unajua, umeniulia mwanangu Sabrina. Nilikupenda sana ila umeniumiza sana dah!"
Sabrina akajiona akikosa raha kabisa, akajaribu kumuelezea Japhet ilivyokuwa ila Japhet alikuwa akimpinga ukizingatia tayari kuna watu walishamueleza wanavyojua wao.
"Sasa unanituhumu bure Japhet, mi nimejulia wapi kama huyo ni mwanamke wako? Walikuja kweli siku ile kwako na kunipiga"
Japhet akasimama na kuanza kufoka,
"Hebu acha uongo Sabrina, siku ile ulipatwa na alama za kugongwa unasema ulipigwa eti! Na aliyekugonga nampongeza sana, sababu wewe ni mwanamke malaya na ni wazi ulikuwa unakimbilia kwa bwana zako"
Sabrina akaumizwa sana na hayo maneno, naye akaamua kuinuka kisha akafungua mlango na kumwambia Japhet
"Nakuomba uende"
"Kwenda nitaenda ila umeniumiza sana kwa kuniulia kiumbe changu"
Sabrina alikuwa na hasira kwa muda huu na kumfanya aongee vitu kwa hasira,
"Usinibabaishe bhana, kiumbe kiumbe hata panya nae ni kiumbe"
"Unasemaje Sabrina?"
"Kama ulivyosikia"
Japhet akajikuta akipandwa na hasira na kuanza kumpiga Sabrina mule ndani, kwa bahati nzuri Fredy na Francis walitokea na kumsaidia Sabrina kisha Japhet akaondoka zake.
Sabrina alikuwa analia tu kwani Japhet alimpiga vya kutosha, kwahiyo Francis na Fredy wakapata kazi ya kumbembeleza.
Ila Sabrina bado alikuwa na hasira sana na hata hakujisikia kubembelezwa alitamani tu nao waondoke mahali hapo ili alie na moyo wake tu kwani kuzungukwa na watu wa aina ile hakutaka kabisa.
Francis na Fredy walijitahidi kumtuliza ila ilishindikana, Francis akamwambia Sabrina
"Ila na wewe Sabrina mambo mengine haya unajitakia mwenyewe"
Huyu ndio alikuwa anamzidishia hasira zaidi,
"Najitakia kitu gani? Kitu gani najitakia?"
Francis naye akatoa yake ya moyoni,
"Mwanamke gani bhana wewe hujui kukataa, kila mwanaume unamkubali tu. Ona sasa, mimi ulinikubali na Fredy pia ukamkubali. Haya ukiulizwa mpenzi wako ni nani kati yetu utajibu nini, uwe unajifikiria wakati mwingine. Inamaana wewe una moyo wa penda penda, yani kila mtu wewe unampenda. Mwanamke wa aina gani wewe? Ndiomana unapigwa hivyo, wote tukitaka haki yetu itakuwaje! Si utakuwa na shimo wewe! Mwanamke gani hujiheshimu bhana!"
Sabrina hakuamini masikio yake kama yale maneno yote yanatokea kwenye kinywa cha Francis, hakuamini kabisa na kumfanya azidi kulia zaidi na zaidi.
"Naomba na nyie muondoke, ondokeni kwetu tafadhari"
"Kuondoka tunaondoka ndio ila niliyokwambia yaweke kwenye akili yako. Na kwa mtindo huo kitu ndoa utakuwa ukisikia kwa wenzio tu kwani hakuna mwanaume hata mmoja anayependa kuwa na uchafu"
Kisha Francis akamwambia Fredy kuwa waondoke na kumuacha Sabrina akilia sana na kujiuliza maswali bila ya majibu ya aina yoyote.
Joy aliporudi alishangaa kumkuta mwanae akiwa analia kiasi kile tena akiwa na alama za kupigwa kwenye mwili wake.
"Sabrina mwanangu nini tatizo?"
Sabrina hakuweza kuelezea kwa wakati huo na kujikuta akizidi kulia tu,
"Nyamaza mwanangu, kichwa kitakuuma jamani. Nyamaza dada"
Joy alijitahidi pale kumtuliza mwanae na kumbembeleza hadi Sabrina akatulia kabisa ila bado alishindwa kuelezea anavyojisikia kwenye moyo wake kwani alihisi kama kuna kitu kimemkaa kooni na kumfanya ashindwe kusema.
Macho yake yalivimba sababu ya kulia sana.
Kisha Joy akamshauri mwanae kwenda kupumzika ili kuweza kupoteza yale mawazo ambayo yanamsumbua na kumtesa kwa wakati huo.
Sabrina akainuka na kwenda kulala.
Kwenye mida ya saa tatu usiku alienda kuamshwa na mama yake ili aweze kwenda kula.
Alitoka ndio na kula kwa kiasi kidogo sana kwani mawazo bado yalimsumbua.
Aliporudi chumbani kwake ili alale, alikuta ujumbe mfupi umetumwa kwenye simu yake kutoka kwa John,
"Kumbe yule mwanamke wa jana alikuwa ni mwanamke wa mpenzi wako, nasikia mimba yake imetoka. Najua utakuwa na mawazo kama hukukusudia ila kama ulikusudia utakuwa na furaha ila hukufanya vyema kwakweli. Kumbuka yule hana kosa lolote, ni mwanamke tu kama wewe. Yakupasa ukamuombe msamaha, yangu ni hayo tu Sabrina. Usiku mwema, ila ulivyo na mambo uliyoyafanya havifanani"
Sabrina aliumia tena kuona kila mtu akimpa lawama kwa jambo ambalo sio kosa lake kabisa, alijisikia vibaya sana.
Hakuweza kulala tena, na alikuwa akijizungusha tu usiku kucha kwani kila upande aliogeuka alijiwa na mawazo yale yale ukizingatia hakutaka mama yake aujue ukweli kuhusu Japhet wala yule mwanamke ambaye mimba ilitoka.
Kulipokucha, Sabrina aliamka na kuoga huku akili yake bado ikiwa na mawazo yasiyo na majibu wala mwisho.
Akapigiwa simu na rafiki yake Sia, akajua wazi kuwa mambo ni yale yale tu. Akatamani asipokee ila aliamua kupokea ili asikie naye atakavyomponda,
"Pole sana Sabrina, nimesikia yaliyotokea. Ila sijaamini kwakweli, na siwezi kuamini kabisa. Sabrina nakufahamu rafiki yangu, najua wazi huwezi kufanya haya niliyoyasikia"
"Ndio hivyo Sia, hata mi mwenyewe sielewi. Kila mtu ananichukia kwa kosa ambalo sio langu"
"Usijali, nitakuja ili tuongee vizuri. Najua wazi huwezi kufanya hivyo Sabrina, utakuwepo kwenu lini ili nije?"
"Nipo Sia, saa yoyote ile ukija utanikuta"
"Sawa nakuja kwenye mida ya saa kumi rafiki yangu"
Huyu akamfanya Sabrina ajisikie vizuri kiasi kwni hali yake ilikuwa mbaya sana mwanzoni,
"Nashukuru Mungu, rafiki yangu Sia ananielewa jamani"
Kidogo muda huu Sabrina akapata nguvu ya kufanya baadhi ya mambo yake huku akimngoja huyo Sia ili aweze kumueleza yote yaliyopo kwenye moyo wake.
Sabrina alikaa na mama yake kuzungumza mawili matatu,
"Nimeongea na baba yako kasema amechelewa kutupa taarifa, ila wiki ijayo unatakiwa kuanza chuo. Kwahiyo mwishoni mwa wiki hii utasafiri mwanangu. Sawa!"
"Sawa mama, hiyo ni khabari njema kwangu na nimefurahi sana mama"
"Usijali mwanangu, kwahiyo hao mashoga zako sijui wakina nani nani huko uwaage kabisa. Sio siku inafika, nawe uanze porojo zako"
"Hakuna tatizo mama"
Mara mlango wao ukagongwa, moja kwa moja Sabrina akajua kuwa ni Sia tu anayegonga mlango na kwenda kumfungulia.
Ni kweli Sia alikuwa mbele, nyuma yake walikuwepo wale wadada wawili waliompiga Sabrina na yule aliyekuwa mjamzito siku mbili zilizopita.
Sabrina akashtuka sana baada ya kumuona mtu mwingine aliyekuja na hao watu akiwa amevalia mavazi ya kipolisi.
Itaendelea
No comments:
Post a Comment