Fredy akaamua kupapasa pale alipokaa Sabrina
ila hakugusa mtu, akashangaa kusikia mshindo na
kuashiria kuwa kuna mtu kaanguka.
Fredy akaamua kumuita Francis kwavile yeye alikuwa haoni chochote kile kinachoendelea mahali pale.
Francis alipofika akashangaa kumuona Sabrina akiwa chini ameanguka na kumfata pale chini huku akimtingisha na kumuita
"Sabrina, Sabrina"
Ila Sabrina hakutingishika wala kuitika.
Francis akamuuliza Fredy kwa mshangao,
"Kwani umemfanya nini huyu!!"
"Nimfanye kitu gani mie!! Hata mwenyewe nashangaa tu hapa, sielewi nini kinaendelea"
Francis akahisi huenda Sabrina amezimia na kuanza kumpepea ila hakuamka wala nini na kufanya Francis na Fredy wasiwasi uwapate vizuri sasa.
Baada ya muda kidogo Joy naye akaingia ndani kwake na kukutana na yale maswahibu yaliyompata binti yake.
"Nini tatizo hapa tamani!!"
"Hata sisi wenyewe tunashangaa maana ameanguka gafla tu"
Joy aliinama pale chini na kumuangalia vizuri mtoto wake huku na yeye akijaribu kumtingisha tingisha ili aweze kuzinduka.
Wali muamsha sana na kujikuta wakikata tamaa juu ya hilo.
Kabla Joy hajaendelea na kitu chochote cha zaidi, wakapatwa na ugeni mahali pale.
Kumuangalia vivuri yule mgeni akagundua kuwa ni wifi yake na kujikututa akimuita pale chini ili apate kumsaidia ila alipewa jibu ambalo huwa anapenda kulitoa iwapo akikutana na hali kama hiyo
"Inuka hapo na umuache kwanza"
"Jamani wifi!!"
"Hakuna cha jamani, nakuomba umuache hapo. Kisha wote tutoke nje"
Ikabidi wamsikilize alichosema, kisha wakatoka nje.
Walipotoka nje, baada ya kama dakika mbili hivi, Fredy alianza kulalamika kuwa macho yake yanawasha.
Fredy akawaomba maji kuwa labda ajaribu kunawa, ila mgeni huyu aliyejulikana kwa jina la Sabrina alimkataza Francis kwenda kumchukulia maji Fredy
"Ila macho yananiwasha sana jamani"
"Acha yakuwashe, ndio uzima wako huo"
Fredy aliendelea kulalamika kuwa macho yanamuwasha hadi machozi yakaanza kumtoka, akapewa ushauri kuwa aende kulala kidogo tu hata kwa dakika tano, naye hakupinga kisha Joy akamuongoza hadi chumbani kwa Sabrina kitandani na kumuacha huko.
Akakatisha pale sebleni na kumwangalia mtoto wake na kusikitika sana, kisha akatoka tena nje.
Hali hii iliyokuwa ikiendelea ilimfanya Francis ahisi kuwa huyu ndiye mdada aliyewapigia simu siku ile kwa madai kwamba anataka kumsaidia Fredy kwani jina alilojitambulisha siku ile ndio lilikuwa jina lile lile walilotambulishwa pale.
Akajiuliza kuwa kwanini yule dada anaongea vitu kama mganga wa jadi! Ila hakupata jibu kabisa.
Wakiwa pale nje wakaisikia sauti ya Sabrina ikikohoa ndani na kutambua kwamba Sabrina atakuwa amezinduka, kisha wakaamua kuingia ndani ambapo walimkuta Sabrina akiwa amekaa kwenye kiti, na alipomuona shangazi yake alifurahi sana na kuinuka kumsalimia
"Umekuja saa ngapi shangazi?"
"Muda sana, wewe si hutaki kuja kwangu"
"Nitakuja tu shangazi"
Sabrina alionekana kuwa sawa kabisa na hata hakuwa na kumbukumbu kama alikuwa ameanguka muda mfupi uliopita.
Baada ya muda kidogo, Fredy alitoka kwenye chumba cha Sabrina na wote wakamshangaa pale sebleni ila yeye alimfata nduguye Francis moja kwa moja na kumwambia
"Kaka, kaka naona mwenzio. Siamini kabisa eti naona jamani"
Francis alifurahi sana na kumfanya azidi kuamini kuwa huyu mdada ndiye aliyewapigia simu ingawa masharti aliyowapa leo ni tofauti na aliyowaambia kwenye simu.
Wote pale walifurahi kuona kuwa Fredy anaona tena, haswaa Sabrina alifurahi sana kwani siku zote alijilaumu kuwa yeye ndio chanzo cha Fredy kutokuona.
Wakafurahi na kuongea mambo mengi sana.
Francis uzalendo ukamshinda na kumfanya aulize kwanza kwani bado alijiuliza bila ya kupata majibu,
"Samahanini jamani, kuna kitu kinanitatiza sana hapo. Naomba kuuliza, haswaa nahitaji nikuulize shangazi"
"Uliza tu hakuna tatizo"
Francis akaanza kuelezea jinsi alivyopigiwa simu na yule mtu na jinsi alivyojitambulisha kwao na kuwapa maelezo ya kupona kwa Fredy,
"Ninachotaka kujua sasa, je mtu huyo ndio wewe shangazi? Na kama ndio wewe mbona masharti uliyotupa hapa ni tofauti na ulichotuambia kwenye simu?"
"Kwani kwenye simu mliambiwaje?"
Ikabidi Fredy aelezee kwavile yeye ndiye aliyeongea na yule dada kwenye simu
"Kwanza kabisa alisema kuwa, tukitoka nyumbani tupite karibu na mbuyu na kuchota mchanga, kisha tukifika hapa kwa wakina Sabrina tuumwage ule mchanga chini ili uchanganyike na ule wa kwenye mbuyu, kisha mimi nizungumze na Sabrina kuwa simtaki tena. Halafu wakati tunaondoka, tuchote mchanga hapo nje kwa wakina Sabrina na kwenda kuumwaga pale kwenye mbuyu aliotuelekeza halafu hapo hapo ndio ningeona. Na hayo mambo ilitakiwa tufanye kwa haraka, kwahiyo hapa hatukutakiwa kukaa sana"
"Eeeh na nyie mmeyafanya yote hayo?"
"Hapana, tulipotoka nyumbani tulisahau kupita kwenye ule mbuyu na kuchota mchanga hivyobasi tukaja moja kwa moja huku na hatukutaka kupoteza muda ndiomana nikamwambia Sabrina kuwa simtaki tena na mambo yakaharibikia hapo"
Sabrina mkubwa aliwasikiliza sana na kuamua kuwapa majibu ya maswali yao,
"Jamani aliyewapigia simu hakuwa mie kabisa kabisa kwanza namba zenu sina na hata nilikuwa siwajui"
Joy naye alishangaa kwa yale maelezo na kuuliza,
"Sasa alikuwa ni nani? Ana lengo gani? Na wewe umejuaje kuwa leo tuna matatizo huku?"
"Unajua jana usiku nimeota vibaya sana kuhusu huku na ndiomana nikaja moja kwa moja, ila hata sikujua chochote. Ila nilipomkuta Sabrina yupo chini huku wewe ukilia lia nikajua tu ni mambo yale yale kama kipindi kile na ndiomana nikawaambia twende nje na kumuacha mwenyewe ndani. Ila mtakuja kumjua tu kuwa ni nani na alikuwa ana lengo gani kwani hakuna kitu ambacho huwa kinajificha milele"
Walibaki kimya huku maswali kadhaa yakitembea kwenye vichwa vyao, tena maswali yasiyokuwa na majibu kabisa kwa wakati huo.
Wakaongea mambo mbali mbali kisha Francis na Fredy wakaaga kwani usiku ulishatawala ila siku hiyo Sabrina mkubwa hakuondoka na kulala hapohapo.
Kesho yake, walipoamka hakutaka kupoteza muda kisha Sabrina akamsindikiza shangazi yake, shangazi yake akamtahadharisha sana Sabrina
"Kuwa makini wee mtoto, mama yako alinisimulia mambo mengi sana juu yako. Wewe bado mtoto mdogo sana, mambo ya kishirikina ya nini? Hata sijui ulianzaje kwenda huko kwa waganga jamani! Wenzio hatukuwa hivyo, na hao
wanaume jamani hebu tulia usome mwanangu, mbona mi shangazi yako sikuwa hivyo jamani! Shauri yako, utapata mimba bure na usijue ni ya nani. Unatakiwa kwenda chuo, tulia uende chuo ukamalizie masomo yako sio kutangatanga tu na wanaume. Pata mmoja utulie naye"
"Sawa shangazi nimekuelewa"
Sabrina alikuwa makini sana kumsikiliza shangazi yake hadi pale alipopanda gari na kuondoka, kisha Sabrina akaanza safari ya kurudi kwao.
Njiani akakutana na John, kisha akasimama kwaajili ya kusalimiana nae
"Za siku nyingi Sabrina"
"Nzuri tu"
"Yani tangu siku ile ndiyo hukutaka tena kupokea simu yangu jamani! Lakini sio kosa langu Sabrina"
"Sio hivyo ila nilikuwa na matatizo tu"
"Hapana Sabrina, najua ulichukizwa sana. Ila yule mwanamke nimemuacha"
Sabrina akashangaa,
"Umemuacha! Kwanini umemuacha?"
"Kwasababu yako Sabrina, sikupenda alivyokujibu"
"Acha masikhara John, yani umemuacha kweli kwasababu yangu!!"
"Ndio Sabrina, sikupenda ule ujinga aliokufanyia. Hajui jinsi gani wewe ni mtu wa muhimu sana kwangu"
"Khee wa muhimu kushinda yeye!!"
"Yeye kitu gani bhana, yani nilichukia sana. Nisamehe Sabrina, naomba usinichukie wewe ni mtu muhimu sana kwangu, bila wewe mimi si chochote"
Maneno hayo yakaingia kwenye akili ya Sabrina na kufanya kazi yake ipasavyo.
"Usijali John, mi nilishakusamehe kitambo sana"
"Asante sana Sabrina"
Kisha John akamkumbatia Sabrina na kuzidi kuichanganya akili yake, akaomba wapange siku ili wapate muda wa kuongea zaidi.
Sabrina akakubali na kupanga siku ya kukutana tena kisha wakaagana na Sabrina kuendelea na safari yake ya kurudi kwao.
Sabrina aliingia ndani kwao huku akiwa amejawa na tabasamu usoni na kujiambia,
"Huyu John atakuwa ananipenda sana yani hadi kafikia hatua ya kumuacha mpenzi wake kwasababu yangu! Mmh huyu ndio ananipenda huyu"
Alikuwa anatabasamu tu hadi mama yake akamuuliza
"Shangazi yako amekwambia maneno mazuri nini huko?"
"Ndio mama, Shangazi ana vituko sana. Leo nimemfaidi na maneno yake kwakweli"
"Na pia uyasikie na maonyo yake na kuyatendea kazi"
"Hapana shaka mama, mimi tena! Lazima niyatendee kazi"
Aliingia chumbani kwake huku mawazo yake yote yakiwa juu ya John, hakumuwaza mwanaume mwingine yeyote kwa wakati huo zaidi ya John tu aliyetawala akili yake.
Usiku ulipofika, John akampigia simu Sabrina na kuzungumza nae mawili matatu na kumfanya Sabrina azidi kufurahia kupendwa na kijana John.
Mchana aliokutana na John walipanga kuonana keshokutwa ila kwa maongezi yao ya kwenye simu kwa usiku huo, waliona keshokutwa ni mbali sana na kuamua kupanga kukutana kesho yake ili waweze kuzungumza.
Wote wawili waliafikiana juu ya maamuzi hayo ya kukutana kesho yake badala ya keshokutwa.
Sabrina alilala huku sura yake ikiwa imetawaliwa na tabasamu tu usoni mwake.
Kulipokucha, Sabrina aliamka na kufanya kazi zake kwa haraka zaidi ili aweze kwenda kwenye safari yake bila ya kipingamizi cha aina yoyote ile kutoka kwa mama yake.
"Leo umekuwa mtoto mzuri kweli mwanangu Sabrina jamani"
"Sipendi kukuchukiza mama yangu, nataka ufurahie mimi kuwa mtoto wako mama"
"Kweli kabisa"
Joy alifurahi sana kuona mwanae kabadilika kwani kupigishana nae kelele kila siku alishachoka kwakweli.
Jioni ilipofika, Sabrina alijiandaa na kumuaga mama yake.
Joy hakuwa na kipingamizi kwakweli ukizingatia mtoto wake alishafanya kazi zake zote tayari.
Sabrina akaianza safari yake ya kwenda kuonana na John.
Alipofika eneo alilopanga kukutana na John, alimkuta John amewasili kitambo tu na akafurahi kumuona Sabrina.
"Yani Sabrina, nina furaha hapa kupita maelezo ya kawaida kwa kukuona tu. Halafu umependeza sana, yani kama malkia vile"
Sabrina akajitazama na kutabasamu kisha akakaa na kuanza kumsikiliza John.
Mwanaume huyu alijua sana kumsifia mwanamke, na kutokana na hilo ikawa rahisi sana kuiteka akili ya Sabrina ambaye muda mwingi alipenda kusifiwa.
"Kwakweli Sabrina nakupenda, sijui nikueleze vipi ila nakupenda jamani. Mimi bila wewe Sabrina sijiwezi, tafadhari nielewe Sabrina. Nikikukosa wewe nitampata wapi tena binti mrembo kama wewe! Hakuna Sabrina, niamini kwa hilo"
Sabrina alikuwa makini kabisa kumsikiliza John, kwakweli maneno ya John yalijua kuiteka akili ya Sabrina na kumfanya awe kimya kabisa katika kumsikiliza,
"Napenda uwe malkia wangu, nitafanya chochote juu yako Sabrina. Simtaki mwingine mimi, nakutaka wewe tu ndio wa kupoza mtima wangu"
Sabrina akatabasamu kuashiria kwamba yale maneno ameyaelewa na yamemuingia vizuri.
Kisha John akamwambia,
"Napenda upate muda wa kutosha kuyatafakari maneno yangu Sabrina ili tuwe pamoja kwa mapenzi ya dhati"
Halafu John akamuomba Sabrina amsindikize nyumbani kwao, Sabrina akamzuia John na kumwambia kuwa asijali ataenda tu mwenyewe.
Ingawa John alisisitiza kumsindikiza ila bado Sabrina alisisitiza kwenda mwenyewe.
John hakuwa na budi zaidi ya kumruhusu kwenda mwenyewe.
Sabrina alipokuwa anarudi kwao, njiani akakutana na mdada mjamzito.
Sura ya yule mdada ikamjia Sabrina kichwani na kumjulisha kuwa ni mdada yuleyule ambaye alikuja na wenzie kule kwa Japhet na kumpiga Sabrina.
Wakati Sabrina akiwaza hayo, mara akatokea mtu nyuma na kumsukuma Sabrina na kufanya amwangukie yule dada mwenye mimba.
Itaendelea
No comments:
Post a Comment