JE HAYA NI MAPENZI!! 17: - UHONDO KITANDANI

Hot

Post Top Ad

https://play.google.com/store/apps/details?id=chumba.cha.wakubwa

Sunday, February 16, 2020

JE HAYA NI MAPENZI!! 17:






Alipomaliza tu kujiandaa, akasikia mtu akibisha
hodi pale kwao. Moja kwa moja akahisi ni huyo
Japhet kaja kumpitia, ila alipoto kufungua alimkuta
Francis na Fredy, hakuwa na cha kufanya zaidi ya
kuwakaribisha tu.
Ile wanaingia ndani tu, Japhet naye akawasili.
Sabrina akamtazama Japhet na kujiuliza kama aondoke na Japhet na kuwaacha pale Francis na Fredy au abakie nao na kumuacha Japhet aende zake.
Yote akayaona si mazuri kuyatenda kwa muda huo ukizingatia Fredy aliletwa na Francis pale akiwa vilevile haoni, ni wazi alihitaji sana kuongea na Sabrina baada ya kusikia yote yaliyompata. Japhet nae alimkawiza sana siku ya nyuma, ila leo alimwambia ni ahadi ya kweli na ndio amekuja kumfata.
Ilibidi akili ya Sabrina ifanye kazi kwa haraka sana, akamvuta mkono Japhet na kutoka nae nje kisha akamwambia kitu
"Nisubiri hapo nje ya geti dakika mbili, natoka sasa hivi"
Kwavile Japhet hakujua kinachoendelea ikambidi tu akubaliane na Sabrina na kwenda nje ya geti kumngoja.
Kisha Sabrina akaingia ndani na kuwafata Francis na Fredy kisha akawaambia
"Natoka kidogo tu, naenda hapo duka la mbele kidogo ila nitarudi muda sio mrefu"
Na kutaka kuondoka ila Fredy akamshika mkono Sabrina na kumwambia
"Unatuongopea Sabrina, najua kama huendi dukani"
"Siwadanganyi, huo ndio ukweli"
Francis nae akamuuliza
"Na mbona umependeza sana?"
"Kupendeza ni kawaida yangu kwahiyo usiwe na shaka, narudi sasa hivi"
Ila Fredy hakutaka kuuachia mkono wa Sabrina na kuzidi kumuomba kuwa asiende
"Nakuomba usiende huko unapotaka kwenda Sabrina"
"Usijali Fredy, ni hapo dukani tu"
"Si salama kwako Sabrina, sipendi ujutie badae. Uendako si dukani, uendako napajua sababu usiku nimeota juu yako. Tafadhari Sabrina usiende huko kwani si salama kwako tafadhari nakuomba"
Sabrina akaona Fredy anamletea longolongo na vitisho tu ingawa Fredy alionekana akiongea kwa uchungu sana.
Ila mwisho wa siku Sabrina aling'ang'ania na kuamua kumuacha aende tu kisha Fredy akasema
"Mtoto akililia wembe mpe, nenda Sabrina, nenda mama, sie tuache hapa ila ukirudi tutakuwa tumeshaondoka"
Sabrina hakujali hilo na kujitokea zake nje.

Akamkuta Japhet akiwa na sura ya hasira kiasi,
"Umeniuzisha sura sana hapa Sabrina"
"Naomba unisamehe Japhet, nipo tayari sasa tunaweza tukaondoka"
Japhet akamuangalia vizuri Sabrina kisha akapanda kwende pikipiki yake aliyokuja nayo halafu Sabrina akapanda nyuma yake na safari yao ikaanza.
Moja kwa moja walienda ufukweni kupunga upepo na kubadilishana maongezi kwanza.

Huku nyumbani kwao mama wa Sabrina alirudi na kuwakuta Francis na Fredy tu mule ndani kwake.
Baada ya salamu ilibidi awaulize,
"Kwani huyu Sabrina yuko wapi?"
Wakamueleza alivyowaaga kuwa anaenda dukani, Joy  akachukia sana,
"Yani hapa mtoto sina jamani, sina kabisa yani. Kavizia nimetoka kidogo tu naye akatokomea pa kutokomea. Mmh hapa mtoto sina."
Fredy na Francis nao hawakutaka kukaa zaidi hivyo basi wakaaga ili waweze kuondoka na kurudi kwao ukizingatia Fredy bado alikuwa haoni kitu, yani macho yake bado yalikuwa na upofu.
Wakati wanaondoka, Fredy akamwambia Joy,
"Ila mama, kuwa makini sana na Sabrina"
"Usijali mwanangu, huyu Sabrina ni kiburi tu kinamsumbua. Ila msijali nipo makini naye, na ngoja arudi leo ili anieleze alipokuwa mtoto huyu loh"
Francis na Fredy wakaaga tena na kuanza safari ya kurudi kwao

Sabrina na Japhet waliongea mambo mengi sana kule ufukweni, na ni dhahiri kila mmoja alifurahia maongezi ya mwenzie kwani nyuso zao zilijawa na furaha kweli kweli.
"Ila Japhet kweli huna mwanamke wewe!!"
"Nimpeleke wapi huyo mwanamke wakati nakupenda wewe Sabrina jamani!! Kisura wangu nakupenda sana"
Sabrina alikuwa akitabasamu tu muda wote na ukizingatia ni mtu anayependa kusifiwa na kusikia kuwa anapendwa.
Japhet aliendelea kumwambia Sabrina,
"Na ili kukudhihirishia kuwa kwangu upo peke yako, naomba leo leo nikupeleke ninapoishi. Tafadhari Sabrina usikatae nakuomba"
Sabrina akaendelea kutabasamu tu na kuwa kama wale watu wa sitaki nataka, ila mwisho wa siku akakubali na kusahau kuwa hata mama yake hakumuaga siku hiyo na pia nyumbani kwao aliacha wageni.
Wakaendelea na maongezi kidogo kisha wakanyanyuka na kuanza safari ya kwenda kwa Japhet.

Japhet alimpeleka Sabrina mpaka nyumbani kwake, kisha wakaingia ndani huku sura ya Sabrina ikiwa imejawa na furaha tu
"Karibu Sabrina, hapa ndio nyumbani kwangu na kwako pia kwani mimi lazima nikuoe kwahiyo utakuwa mke wangu na changu kitakuwa chako"
"Kweli nimeamini Japhet unanipenda jamani"
"Ndio, nakupenda sana naomba ujisikie huru tafadhari"
Wakati  wanaendelea kubadilishana mawazo huku Japhet akiwa na hamu kubwa ya kuwa karibu na Sabrina, mara simu ya Japhet ikaita na kisha akaipokea na kusikika akijibu
"Nani?..... Unataka nini?...... Usije tafadhari...... Mbona unakuwa hivyo bhana...... Poa ningoje hapo hapo dakika sifuri."
Kisha akaikata ile simu na kumuangalia Sabrina, ila kabla hajasema chochote Sabrina akamwambia,
"Unataka kutoka?"
"Aaah kuna mtu mmoja namfata hapo tu ila sasa hivi narudi"
"Basi usichelewe"
"Sitachelewa, ila akija mtu na kugonga mlango hapa kwangu usimfungulie hadi nirudi"
Kisha Japhet akatoka na kwenda alikopigiwa ile simu.

Sabrina akiwa kabaki mwenyewe mule ndani ya nyumba ya Japhet, akawa anajisemea sasa,
"Huyu ndio mwanaume bhana anaishi kwake, sio Francis na Fredy wanaoishi kwao bado"
Wakati akijisemea hayo, kuna mtu akabisha hodi kwenye nyumba ile ya Japhet.
Ila kwakuwa Sabrina huwa anapenda kujua mambo akaona akamfungulie tu ingawa alikatazwa na mwenye nyumba.
Waliingia wadada watatu walioonekana kuwa na jazba sana ila mmoja kati yao alikuwa na tumbo kubwa, inaonyesha wazi alikuwa na ujauzito.

Sabrina alikuwa akiwashangaa tu kwani hakuelewa walitaka kitu gani, mmoja akamuuliza Sabrina
"Upo humu ndani kama nani?"
"Kwani vipi jamani?"
"Tueleze tujue, upo hapa kama dada wa Japhet au kitu gani!"
"Hapana, mi ni mpenzi wake....."
Hawakutaka Sabrina amalizie maneno kwani walimvamia mwilini gafla na kuanza kumpiga hovyohovyo, huku wakisema
"Umetusumbua sana wee mbwa, ngoja leo tukufunze adabu ili usirudie tena"
Sabrina alipiga kelele lakini hazikusaidia kwani wale wadada walimpiga sana na kumuacha akiwa ameumia sana kisha wakaondoka zao.
Sabrina alibaki na maumivu pale chini huku akilia kwani hakujua kosa lake kuwa ni kitu gani hadi wale wadada kumshambulia kiasi kile.
Sabrina hasira ikampata na kumfanya ajikongoje kuinuka pale kisha akafanya uamuzi wa kuondoka kwa hasira tena bila hata ya kumuaga Japhet.
Akatoka nje na kuanza kuondoka huku amejawa na hasira tupu moyoni mwake.
Akiwa anajaribu kutafuta usafiri huku anaenda hovyohovyo, ikatokea baiskeli upande mwingine na kumvamia, kisha akaanguka chini na kupoteza fahamu.

Wasamalia wema wakamzingira ili kumsaidia, kwa bahati Japhet nae alikuwa anakatisha eneo lile. Alishangaa kuona watu wamezingira kwenye lile eneo, akaamua naye kwenda kushuhudia.
Alishangaa sana na kustaajabu kuwa ni Sabrina pale chini.
Wakasaidiana na baadhi ya watu na kumuwaisha Sabrina  hospitali. Hata mwendesha baskeli mwenyewe alishangaa kuwa amemgonga vipi Sabrina hadi kuzimia vile.

Japhet ikabidi ampigie simu mama wa Sabrina na kumjulisha kuhusu ajali aliyoipata binti yake.
Joy alihisi kuchanganyikiwa kabisa, bahati nzuri kwa muda huo Sakina naye alikuwepo pale kwa Joy na kumsaidia kumpa matumaini kisha kufunga hospitali na kwenda alipolazwa Sabrina.

Walipofika walimkuta Sabrina bado amezimia, ila baada ya muda kidogo akazinduka na kuanza kulia.
Mama yake alikuwa pembeni akimbembeleza huku akishangaa kuwa ni kitu gani kinamliza.
Japhet nae akasogea karibu, ila Sabrina alipomuona Japhet akazidisha kulia hadi daktari akaamua kumtoa Japhet nje. Kisha yule daktari akamchoma Sabrina sindano ya usingizi ili alale kwanza na kupotezea lengo la kulia kwake.
Walipotoka nje ya wodi, Joy alimfata Japhet na kwenda kumuuliza
"Hivi umemfanya nini mwanangu wee kijana?"
"Mi sijui mama"
"Hujui nini na wakati alilia zaidi kukuona wewe!!"
Ikabidi Sakina asogee karibu na kumtuliza Joy aliyemuona kuwa na jazba ya haswaa dhidi ya mwanae.

Wakati Francis na Fredy wamerudi nyumbani kwao, kuna mtu alimpigia simu Francis na kujitambulisha kwa jina la Sabrina kisha akaomba kuzungumza na Fredy.
Francis hakusita kwa hilo na kumkabidhi Fredy ile simu, upande wa pili ukaongea
"Najua huoni"
"Ndio, kwani wewe ni nani?"
"Nishajitambulisha tayari, mimi naitwa Sabrina pia napenda kukusaidia. Je upo tayari?"
Fredy akasita kidogo, kisha akakubali
"Ndio nipo tayari"
Yule dada akampa maelekezo Fredy, akamwambia mambo ya kufanya kisha akakata simu.
Fredy aliishikilia ile simu na kumuuliza Francis
"Eti ni Sabrina gani huyu?"
"Hata mi simjui kwakweli, kwani sauti yake ni ngeni masikioni mwangu. Hata sio Sabrina tuliyemzoea, haya niambie alichokwambia"
Fredy akaanza kumwambia Francis kile alichoambiwa na huyo mdada kuhusu kupona kwake.
"Usijali Fredy nitakusaidia"
Fredy akafurahi na kumshukuru nduguye Francis.

Baada ya siku mbili Sabrina alikuwa katika hali nzuri na kuruhusiwa kurudi kwao, kwahiyo wakarudi naye nyumbani huku akiwa na hali nzuri kiasi.
Joy hakutaka kumsema mtoto wake kuhusu kitu chochote kile kwani hakutaka kumkumbusha yaliyopita na hakutaka hali yake iwe mbaya zaidi.
Sabrina alitulia tu nyumbani kwao bila ya kuwasiliana na mtu yeyote yule hata Fredy na Francis nao hawakuja kumuona na kumfanya ajihisi vibaya,
"Najua walichukia siku ile nilipoondoka na kuwaacha hapa ndani peke yao"
Mama yake alimsikia akijilalamisha na kumuuliza,
"Ni wakina nani hao?"
"Sio kitu mama"
Kisha Sabrina akaenda kupumzika.

Usiku wa siku hiyo alijikuta akipatwa na njozi za kila aina ambazo hakuelewa zinamaana gani katika maisha yake.
Aliota kuwa ana mtoto mchanga anamnyonyesha, ila baba wa mtoto huyo hakumfahamu na kushtuka toka kwenye ule usingizi kisha akajiangalia kwa makini na kujiuliza kuwa ile ndoto inamaana gani kwake! Kisha akakumbuka maneno ya yule bibi kuwa ile kamba ikikatwa basi hatobeba mimba wala hatoweza kuzaa, sasa ndoto ya kuwa na mtoto mchanga ilikuwa na maana gani kwake, hakuelewa kabisa.

Kulipokucha bado alikuwa na mawazo ya ndoto aliyoota usiku wake bila ya majibu.
Alianza kuwawaza wanaume waliowahi kumwambia kuwa wanampenda na mapungufu yao, kisha akajiambia
"Kati ya wote, nadhani Fredy ndiye anayenipenda kiukweli. Najua yeye atanivumilia katika hii hali niliyokuwa nayo, natakiwa kuwa na Fredy tu"
Moyo wake sasa uliona kuwa umefanya maamuzi sahihi ya kuwa na Fredy, akangoja apone vizuri ili aende kumuona Fredy na kumwambia ya moyoni.

Mchana wa siku hiyo, Sabrina alitembelewa na watu wawili ambao aliwaona ni wa muhimu sana katika maisha yake.
Alikuwa ni Francis na Fredy, Sabrina alifurahi sana kuwaona ingawa hawakwenda hospitali kumuona.

Baada ya muda kidogo, Fredy akamuomba Sabrina kuwa anahitaji kuzungumza naye.
Hivyobasi Francis akawaachia nafasi ili waweze kuzungumza.
"Sabrina, kuna jambo la muhimu sana nahitaji kuzungumza na wewe"
"Niambie tu, Fredy hata usiwe na shaka"
"Ila nakuomba unisamehe kwa haya nitakayokwambia"
"Mbona unanitisha Fredy, niambie tu"
"Kuanzia leo Sabrina, sitakuwa na wewe"
"Mbona sikuelewi Fredy!!"
"Yani sikutaki tena"
Kimya kikatawala kwa muda huo, Fredy akajaribu kumuita Sabrina ili ajue kama yupo anamsikiliza ila kimya kikatawala.
Fredy akaamua kupapasa pale alipokaa Sabrina ila hakugusa mtu, akashangaa kusikia mshindo na kuashiria kuwa kuna mtu kaanguka.

Itaendelea



No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

https://play.google.com/store/apps/details?id=chumba.cha.wakubwa