JE HAYA NI MAPENZI!! 14: - UHONDO KITANDANI

Hot

Post Top Ad

https://play.google.com/store/apps/details?id=chumba.cha.wakubwa

Sunday, February 16, 2020

JE HAYA NI MAPENZI!! 14:





Fredy akafungua ule mkoba, kikatoka kitu kama
moshi na kuyakumba macho ya Fredy.
Fredy akaachia ule mkoba na kupiga ukelele wa
nguvu kisha akaanguka chini.
Sabrina akamuita mama yake aliyekuja mbio sana kutokana na ile kelele aliyoisikia kutoka ndani kwake.
Alipoingia alishangaa kumuona Fredy akiwa chini
"Imekuwaje Sabrina?"
"Sijui mama, ni gafla tu"
Mama huyu akaenda kuleta maji na kuanza kumwagia Fredy, hadi Fredy akazinduka.
Ila alipozinduka, alikuwa akifikicha macho yake na kudai kuwa yanamuwasha sana.
Joyce alichukua yale maji na kujaribu kumnawisha Fredy kwenye macho, lakini bado Fredy alilalamika kuwa macho yanamuwasha tena sana tu.
Aliyafikicha kwa muda, huku nao wakijaribu kuendelea kumpa huduma ya kwanza ambayo kwao ilikuwa ni kumuosha kwa maji.

Baada ya muda kidogo, muwasho ulipungua kwenye macho ya Fredy, naye akajaribu kuyafumbua ili aone lakini hakuona kitu chochote kile.
"Jamani sioni, sioni jamani"
Wakajaribu kufanya kila kitu walichoweza lakini bado Fredy aliendelea kulalamika kuwa hawezi kuona chochote.
Joyce aliamua kumbembeleza Fredy ili atulie na wajue cha kufanya kwa wakati huo.
Fredy akatulia kiasi na kumpa mama Sabrina nafasi ya kuongea
"Kwani imekuwaje Sabrina?"
"Hata mi mwenyewe sielewi mama, yani nashangaa tu hapa"
"Hebu nipe mlolongo mzuri wa matukio nikuelewe"
Sabrina akamwambia mama yake kuhusu  ilivyokuwa muda mfupi uliopita.
"Mbona sielewi? Kwani hiyo pochi ina nini?"
"Haina kitu mama"
Kisha Sabrina akachukua ile pochi na kubwaga vyote vilivyokuwemo ndani yake.
"Si unaona mwenyewe mama, hii pochi haina chochote yani hata mi mwenyewe nimeshangaa tu hapa"
"Mmh makubwa haya mwanangu"
Wakaanza kujadiliana jinsi ya kumrudisha Fredy kwao na jinsi ya kuwataarifu ndugu zake kuhusu yaliyotokea.
Basi Joy akainuka na kumuacha mwanae Sabrina ili amuulize vizuri namna watakavyomrudisha kwao.
"Kwakweli Fredy mi nimechanganyikiwa hapa, sasa tutakupelekaje kwenu?"
"Mpigie simu Francis ili aje kunichukua"
 Sabrina akakubaliana na hilo kwa Fredy, kisha akaenda kumwambia mama yake ambaye pia aliafikiana kuhusu hilo na kuamua kumpigia simu Francis ili aje kumfata ndugu yake.
"Kwani kuna nini Sabrina?"
"Njoo tu utaona hukuhuku, tafadhari njoo upesi"
Ingawa Francis hakujua anaitiwa kitu gani ila ile kauli ya kumwambia aende upesi ilimpa wasiwasi na kumfanya ajiandae haraka na kuianza safari.

Francis alipofika kwakina Sabrina, alikaribishwa ndani na kushangaa kumuona Fredy akiwa pale ndani.
Moja kwa moja Francis akauliza
"Vipi jamani!"
Fredy akajibu,
"Sioni Francis, sioni mwenzio"
"Imekuwaje kwani Fredy?"
"Nipeleke nyumbani tafadhari, nitakueleza tukifika nyumbani"
Ikabidi Francis asaidiane na Sabrina katika kumpeleka Fredy nyumbani kwao.

Walipofika, walimpeleka Fredy chumbani akapumzike.
Ikabidi Sabrina amuage Fredy,
"Tafadhari usiniache Sabrina"
"Usijali Fredy, sitakuacha kamwe"
"Nakupenda sana Sabrina, tena sana"
Kisha Francis akamfata Sabrina kuwa watoke ili amsindikize.
Francis akamsikia Fredy akimwambia Sabrina
"Tafadhari Sabrina, nibusu kabla hujaenda"
Sabrina akainama na kumbusu Fredy, kisha akamuaga na kutoka nje na Francis.
Ila kile kitendo cha Sabrina kumbusu Fredy kilimuumiza sana na kujikuta akipatwa na wivu juu yao.

Walipotoka nje akamuuliza
"Kwani kuna nini kinaendelea kati yako na Fredy?"
Sabrina alishindwa kujibu kwavile hakuelewa ni kitu gani atamwambia Francis ili aweze kumuelewa.
"Naomba umuulize Fredy mwenyewe"
"Niambie vizuri Sabrina, si unajua kama nakupenda! Halafu Fredy ni ndugu yangu, ila kwanini unataka kunifanyia hivi Sabrina?"
Sabrina hakuwa na jibu na akajua wazi kama ataendelea kuongea kuhusu hilo na Francis basi lazima kuna ugomvi utatokea tu, hivyobasi alipoona gari inapita alisimamisha na kupanda ili tu kuweza kuepukana na marumbano na Francis ukizingatia usiku ulishakuwa mkubwa.

Sabrina akiwa kwenye lile gari, alikaa na kijana mmoja aliyemsikia kwa jina moja ambalo wenzie walikuwa wakimuita.
Kijana huyo alikuwa akiongea sana kwenye lile gari, na kila alipoongea aliwafurahisha watu wengi akiwemo na yeye mwenyewe Sabrina.
Na walipofika kwenye kituo, Sabrina alijikuta akishuka pamoja na yule kaka. Ikabidi amuongeleshe tu,
"John!"
"Kheee dada umenijuaje?"
"Nimesikia watu wakikuita hivyo kwenye gari, nimeyapenda sana maongezi yako"
"Kumbe eeh! Nipe namba zako basi"
Sabrina hakuona tatizo kumpa huyu kijana namba zake ili waweze kujadiliana zaidi na zaidi.
Kisha wakaagana na kuondoka.

Sabrina alipofika nyumbani kwao alimsikia mama yake akifanya maombi, haswaa alimsikia akimuombea pia na yeye kuwa arudi salama.
Alikaa pale nje na kumsikiliza mama yake kwa makini zaidi hadi alipomaliza yale maombi ndipo naye akaingia ndani.
"Sabrina, mgonjwa anaendeleaje?"
"Nimemuacha pale kwao amelala mama"
"Amegoma tena kuhusu hospitali?"
"Amekataa kabisa, anaamini kuwa atapona tu"
"Ndio, Mungu mkubwa hata mi naamini kuwa atapona tu"
"Basi vizuri mama, ngoja niende chumbani kwangu"
Sabrina aliingia chumbani kwake, ila kabla hajafanya chochote alipigiwa simu na yule John aliyekutana nae kwenye basi.
"Hivi jina lako unaitwa nani?"
"Naitwa Sabrina"
Basi John akaanza kumwambia Sabrina vitu vingi vya masikhara na kumfanya Sabrina acheke sana kutokana na kile ambacho John alikuwa anamwambia hadi pale alipokata simu, Sabrina alikuwa ameshacheka sana hadi machozi yakamtoka kwa kucheka na kujikuta akiongea peke yake
"Yani huyu kijana ana vituko sana dah, nimecheka hadi raha"
Kisha akaenda kuoga na kurudi kulala.

Akiwa usingizini, akamuona yule bibi wa wakina Francis akiwa ameushika ule mkoba wake aliousahau katika nyumba ya kulala wageni.
Kisha akaifungua na kuweka vitu vyenye asili ya ungaunga halafu akawa kama ananenea vitu fulani kwenye ule mkoba.
Kisha Sabrina akajiona akishika ule mkoba, vikatoka vitu kama moshi kwenye ule mkoba na kuelekea kwenye macho yake, kisha akahisi macho yakimuwasha sana na alipokuja kufumbua alikuwa ni kipofu tayari.
Sabrina akanza kulia bila ya kujua kama anaota, hadi mama yake akakimbilia chumbani kwa Sabrina huku akijua kuwa binti yake kapatwa na matatizo.
Alimkuta akiwa kalala chali huku machozi yakimbubujika
"Wee Sabrina, wee Sabrina"
Sabrina akashtuka na kujifikicha macho,
"Una matatizo gani wewe mtoto?"
"Kumbe naona mama!"
"Kwani ulikuwa huoni! Mbona una mambo ya ajabu wewe mtoto?"
Alitafakari ndio akagundua kwamba alikuwa anaota.
"Samahani mama, ni ndoto tu"
"Aaah! Una kichaa sana wewe mtoto wangu, muone na akili zake zilivyofupi. Ngoja nikamalizie usingizi wangu mie"
Akatoka na kwenda chumbani kwake huku akijisemea
"Najuta kumpa mwanangu jina la shangazi yake"

Kulipokucha, Sabrina akaamka na mawazo mapya kichwani mwake kwani ile ndoto aliona kama vile imempa mjibu ya maswali kadhaa katika akili yake.
"Inawezekana ule mkoba wangu ulifika kwa yule bibi na ndiomana nimeletewa na Francis, ni lazima yule bibi alifanya kitu kibaya kwenye ule mkoba ili aweze kunidhuru mimi, sasa kamdhuru mjukuu wake mwenyewe! Mmh sijui itakuwaje sasa. Inamaana Fredy kawa kipofu badala yangu! Lazima nifanye kitu cha kumsaidia"
Sabrina alijiona kuwa yupo njiapanda kwasasa na haya mambo kwani hakuyatarajia.

Mchana wake alienda kwa Sakina, alikuwa na mengi ya kumueleza ukizingatia ni siku kadhaa zimepita bila ya wao kuongea chochote.
"Bora umekuja Sabrina mdogo wangu"
"Kuna nini dada?"
"Nina khabari mbaya kuhusu hiyo kamba yako ya kiunoni"
"Mmh! Hebu niambie vizuri dada, maana hata sielewi kitu hapa."
"Ni hivi, mimi niliondoka hapa kwenda kuulizia kuhusu hiyo kamba yako kwa watu wenye uzoefu nazo"
"Eeh wamesemaje?"
"Ni hivi mdogo wangu, kwavile aliyekufunga hiyo kamba alishakufa na hakuna wa kukufungua tena basi lazima wewe uliyefungwa hiyo kamba upate madhara"
"Mmh yapi hayo, niambie dada jamani"
Huku moyo wa Sabrina ukienda kwa kasi sana, Sakina aliendelea kumueleza
"Kwanza kabisa, hutakiwi kukutana kimwili na mwanaume yoyote yule. Hairuhusiwi mwanaume yoyote kuiona hiyo kamba yako, na siku ile yule mkaka aliamka ni kwa bahati tu. Pia, hiyo kamba haitakiwi kukatwa na mtu yeyote yule labda kama itatokea siku ikakatika yenyewe huo ndio utakuwa uzima  "
"Jamani dada, naishije mimi sasa kwa mtindo huo? Kwahiyo sitakiwi kuwa na mchumba? Kwahiyo mimi sitaolewa wala kuwa na watoto?"
"Ndio hivyo Sabrina, kwahiyo kuwa makini sana. Na ikitokea mtu akakukata hiyo kamba jua kwamba mtu huyo atapata madhara makubwa sana, vilevile kila mwanaume utakayelala nae atakufa na ukibeba mimba lazima itatoka"
Sabrina aliogopa sana na kutetemeka huku machozi yakimtoka, hakutaka kuwa na hali ya namna hiyo katika maisha yake kwani alipenda kuwa kama wanawake wengine duniani.
"Sasa nitafanyaje dada?"
"Cha msingi ni kuombea hiyo kamba ikatike yenyewe ili uwe huru"
"Itabidi niende tena kwenye lile kaburi la yule bibi ili nimuombe anipunguzie adhabu hii au hata aikate kimiujiza"
"Labda tufanye hivyo mdogo wangu, basi kesho asubuhi na mapema twende huko"
"Sawa dada"
"Ila kuwa makini sana na hiyo kamba, jihadhari mtu yeyote asije akaiona hiyo kamba Sabrina. Sawa eeh!"
"Hata hivyo nipo makini sana, hata mama tu ndani kwetu hajui kama nipo hivi"
Sabrina akakubaliana na Sakina juu ya mpango wao wa siku ya kesho wa kwenda kwenye kaburi la yule bibi.

Sabrina alirudi nyumbani kwao akiwa amepunguza kiasi kidogo cha mawazo na kuongeza kiasi kingine ambacho hakujua kitaishia wapi.
Hakujua hatma yake na ile kamba yake ya kiunoni, kwavile alikuwa na mawazo mengi sana, akama ni vyema ampigie simu yule John mwenye vituko ili aweze kucheka na kufurahi.
Akaipiga ile simu, ila haikupokelewa na John kama alivyotarajia bali ilipokelewa na sauti ya kike
"Samahani, John yupo?"
"Unamuulizia John wewe kama nani?"
Sabrina akaona kuwa itazuka shari pale na kuamua kukata ile simu huku akijisemea
"Kumbe huyu John ana mwanamke, kwanini hakuniambia sasa?"
Alihisi kama moyo ukimuuma vile na kujigundua kuwa ameingiliwa na mdudu wivu kwa John wakati si mpenzi wake.
"Ngoja niachane na mawazo ya kijinga  ilihali najua wazi kwamba siwezi kuwa na mpenzi kutokana na matatizo niliyonayo, hata najishangaa kuwa naanzaje kupenda jamani"
Hali ya kuwa hivi ilimsumbua sana Sabrina na kujikuta akitamani kesho yake ifike na waweze kwenda huko makaburini na pengine ukawa ndio ukombozi wake kwenye maisha.

Usiku wa siku hiyo alikuwa akiwaza tu kuhusu kamba yake ya kiunoni
"Ni kweli inanisaidia kuona wachawi, na pia inanisaidia kupambana nao lakini kwanini initese hivi!! Na mbona kabla sijawa nayo hao wachawi hawakunisumbua?"
Alikuwa akiwaza tu muda wote huku akiamini kwamba akienda kule makaburini kulia na kumuomba yule bibi basi atasalimika na kusahau kwamba ameshawahi kufanya hivyo kabla lakini tatizo bado liliendelea tena kwa makubwa zaidi kila kukicha.
Usingizi ulimpitia akiwa bado na mawazo.

Wakati yupo usingizini, alikuja yule mmama waliyekutana nae mchana. Kama kawaida Sabrina alishtuka na kuanza kuangaliana nae,
"Kwani mnataka nini kwangu nyie?"
"Tunataka uwe mshirika mwenzetu"
"Sitaki, na muondoke"
"Nimekuja peke yangu leo, sina nia mbaya ila nataka uwe mshirika mwenzetu"
Sabrina akainuka huku akitetemeka, akachukua maji yaliyokuwepo pembeni yake na kumwagia yule mchawi, muda huo huo yule mchawi akatoweka.
Sabrina akashangaa kuona kuwa hata maji nayo ni dawa, ila hakuweza kulala tena hadi palipokucha.

Aliamka na kwenda kuoga ili kujiandaa kwaajili ya safari aliyopanga na Sakina.
Wakati anaanza kujiandaa tu, mama yake akaingia gafla chumbani kwake bila ya hodi na moja kwa moja alimshangaa Sabrina kiunoni
"Nini hiko cheusi kwenye kiuno chako Sabrina?"
Sabrina akashtuka sana na kuchukua khanga ili kujifunika.
Kama kawaida ya Joy, hakutaka kukubaliana na kujifunika kwa mwanae.
Hivyo basi akamfata na kuitoa ile khanga kwa nguvu,
"Khee una kamba kiunoni Sabrina! Tena nyeusi! Mambo gani hayo ya kishirikina Unayaleta ndani kwangu!"
Akamfata karibu, kisha akachukua mkasi uliokuwepo kwenye meza ya Sabrina na kuikata ile kamba.

Itaendelea   l



No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

https://play.google.com/store/apps/details?id=chumba.cha.wakubwa