Ila kabla Sabrina hajafanya chochote cha zaidi, yule
bibi ambaye alimfunga kamba hiyo Sabrina alitokea
mbele yao.
Sabrina akashtuka sana kumuona yule bibi sababu alishakufa kwa muda mrefu.
Muda huo, Fredy alikuwa kama mtu aliyepitiwa na usingizi mzito kwani alikuwa hadi akikoroma kwa muda mfupi tu.
Yule bibi alikuwa akimtazama tu Sabrina, kisha akainua mkono wake na kunyoosha kidole chake mpaka kwenye kiuno cha Fredy kisha ile kamba ikatoka kwenye kiuno cha Fredy na kuhamia kwenye kiuno cha Sabrina.
Muda huo Sabrina alijikuta akiongea kwa nguvu
"Naomba unitoe hii kamba"
Yule bibi akajibu,
"Siwezi kukutoa kwani ukiitoa hiyo kamba utateseka sana kama usiku wa jana. Ila kuna sharti moja sikukupa"
"Lipi hilo?"
"Hutakiwi kukutana kimwili na kijana yoyote yule"
Kisha yule bibi akatoweka na kumfanya Sabrina ashtuke sana.
Sabrina akajishika kiunoni na kujikuta na ile kamba ambayo hakuitaka siku zote.
Akamuangalia Fredy pale kitandani ambaye aliamka na kuwa kama mtu anayeshangaa kisha akamuuliza Sabrina
"Kwani kimetokea nini Sabrina?"
"Sijui na siwezi kuelezea"
Sabrina akatoka nje na kuondoka kwavile hakujielewa kabisa, hakuielewa akili yake kabisa.
Alipofika kwao, alimkuta mama yake akiongea na Sakina.
Akawasalimia, kisha akataka kumuuliza kuhusu kutokupatikana kwake ila alijiona akisita kuongea chochote, na badala yake akajikuta akiamua kwenda chumbani kwake tu.
Fredy akiwa kwenye kile chumba cha kulala wageni bado alijishangaa na kujiuliza maswali mengi bila ya majibu yoyote, akakumbuka maneno ya bibi yao alipokuwa akimwambia Francis kuwa yule Sabrina sio mwanamke wa kuwa naye
"Inawezekana bibi aliongea maneno ya ukweli, najuta kumfahamu huyu mwanamke kwakweli ingawa moyo wangu bado unampenda sana"
Fredy aliinuka naye na kutoka kwenye kile chumba walichokuwa na Sabrina.
Wakati Fredy anaondoka, akashangaa gafla akiitwa na yule muhudumu wa ile nyumba ya kulala wageni
"Kaka samahani, nakuomba mara moja"
Ikabidi Fredy arudi na kusikiliza wanachomuitia.
Alipofika karibu, yule muhudumu alikuwa amebeba mkoba wa kike na kumkabidhi Fredy
"Mmesahau mkoba wenu kaka"
Fredy akauangalia kwa makini na kugundua kuwa ule ni mkoba wa Sabrina, hivyobasi akauchukua na kwenda nao kwao ili ajipange siku ya kuupeleka huo mkoba kwa muhusika.
"Nitampelekea kesho huu mkoba"
Ila Fredy hakuelewa imekuwaje hadi Sabrina asahau mkoba wako.
Sabrina alipokuwa chumbani kwake, akakumbuka kuhusu mkoba wake na kuamua kumpigia simu Fredy ili kujua kama aliuacha kule au ni vipi.
"Fredy, eti niliacha mkoba wangu kule"
"Ndio, ila nitakuletea kesho Sabrina usijari"
"Naomba unitunzie Fredy, huo mkoba ni wa muhimu sana kwangu"
"Usijali Sabrina nitautunza"
Walipomaliza mazungumzo, bibi yake Fredy alikuwa pembeni na alisikia kila kitu ambacho Fredy alikuwa akikizungumza.
"Mkoaa gani huo Fredy?"
"Ni mkoba wa Sabrina, kuna mahali aliusahau"
"Basi nipe mie niutunze mpaka hiyo kesho kwamaana nyie wanaume huwa hampo makini sana"
Fredy akampa bibi yake ule mkoba na kuondoka.
Sabrina hakujisikia hata kula kwa siku hiyo zaidi ya kulala tu ili aweze kupunguza mawazo aliyokuwa nayo juu ya mambo yaliyomtokea na kile alichoambiwa na na yule bibi alipowatokea.
Muda mwingi taswira ya yule bibi ilicheza katika akili yake, akatamani hata siku zirudishwe nyuma ili iwe ile siku aliyopelekwa kwa yule bibi na kufungwa kamba kiunoni ili aweze kuikataa siku hiyo katika maisha yake. Ila kama ilivyo, maji yakishamwagika hayazoleki. Siku nayo ikipita imepita, ndiyo iliyomtesa katika maisha yake ya sasa.
Usingizi ulimpata kwa shida sana kwani muda mwingi alikuwa na mawazo.
Kulipokucha, Sabrina alikuwa wa kwanza kuamka katika nyumba yao na moja kwa moja alienda kukaa sebleni na kujiinamia kwa mawazo aliyokuwa nayo.
Mama yake alimkuta na kujaribu kumuuliza tena
"Una tatizo gani mwanangu?"
"Sina tatizo mama"
"Hivi kwanini huwa hutaki kusema? Unajua kukaa na mawazo sana ni dhambi? Kwanini hutaki kuniambia mama yako ili niweze kukushauri mwanangu jamani!"
Sabrina alimuangalia mama yake kwa huruma, huku akitamani kumwambia ukweli wa mambo ila mara zote alihisi kama atasema ukweli basi mama yake anaweza kumfikiria kwa mabaya.
Bibi yao na wakina Fredy, alimuita Francis na kumwambia
"Mkoba huu ni wa Sabrina"
"Umeutoa wapi bibi?"
"Alikuwa nao Fredy, kuna mahali Sabrina aliusahau. Sasa mimi nataka wewe ndio ukampelekee Sabrina"
"Kwanini mimi bibi? Na mbona umemjua Sabrina kiasi hicho wakati ulimuona mara moja tu tena ukiwa mgonjwa!"
"Wewe mpelekee huu mkoba, ukirudi nitakwambia kila kitu. Ila ufate nitakacho kwambia wakati unaenda"
Francis akakubali, kwani cdo alikuwa anampenda Sabrina ingawa mara ya mwisho alimfukuza kama mbwa na ubaya ni kwamba hakujua chochote kilichoendelea kati ya Fredy na Sabrina.
Hakujua kama walifahamiana zaidi kwa siku zote hizi ambazo yeye ameshindwa kuwasiliana na Sabrina.
Francis alijiandaa na kuianza safari ya kwenda kwa wakina Sabrina kwa lengo la kumpelekea ule mkoba na vilevile kwa lengo la kumuona kuwa anaendeleaje ingawa alishaambiwa na bibi yake kuwa mwanamke huyo hafai kuwa naye, na ndiomana Francis huwa anamshangaa bibi yake kuwa anamjua vipi Sabrina.
Francis alienda mpaka kwakina Sabrina, na mtu wa kwanza kuonana naye ilikuwa ni mama wa Sabrina.
Alishangaa kuona yule mama akimkumbuka
"Khee mbona ulipotea wewe kijana?"
"Majukumu mama, je Sabrina nimemkuta?"
"Yupo ndani ndio, ngoja nikuitie"
Joy alimuita binti yake, na moja kwa moja Sabrina akatoka nje ili tu kujua ni kwanini anaitwa.
Sabrina akashangaa kumuona Francis mbele ya macho yake, akajikuta akitamani kumkumbatia.
Wakati yeye akitamani hivyo, hata Francis naye alikuwa akitamani hivyo hivyo na kujikuta wamekaribiana na kukumbatiana, kisha maongezi mengine yakaendelea
"Nimekuletea mkoba wako Sabrina"
Sabrina akashtuka kwani hakujua kama Fredy angempa Francis ule mkoba aulete.
Francis alimpa Sabrina mkoba ukiwa ndani ya mfuko wa plastick, Sabrina alipokea na kumshukuru Francis
"Asante sana"
"Ila unajua nilipoutoa?"
Sabrina alinyamaza kimya kwa muda, kisha akamjibu
"Sijui, niambie umeutoa wapi?"
Francis akacheka na kusema
"Najua unanizuga tu hapa, ngoja niende ila badae nitakutafuta Sabrina nina shida sana na wewe"
"Poa, hakuna tatizo karibu sana"
Kisha wakaagana na Francis akaondoka.
Sabrina alienda chumbani kwake na kuweka ule mkoba, mawazo yakamuhama sasa.
Yakahamia kwa Francis, alijiona wazi akimpenda Francis zaidi ya alivyojihisi kumpenda Fredy.
Alikaa na kujiuliza,
"Hivi ni nani nimpendaye kati ya Francis na Fredy? Inawezekana hawa ni ndugu, itakuwaje sasa? Ila kama Francis akiamua kuwa na mimi tena basi ni bora nikawa mbali na Fredy kwavile Fredy alishanikuta nikiwa na mahusiano na Francis tayari."
Mapenzi yalionekana kumchanganya sasa baina ya watu hawa wawili, ila kila alipoikumbuka ile sauti ya yule bibi kuwa haruhusiwi kulala na mwanaume yeyote yule, alinyong'onyea.
Jioni ya siku hiyo alienda mahali na kukutana na Francis ambaye alimuomba msamaha kwa yale aliyomwambia.
"Nisamehe Sabrina, bado nakupenda"
"Hata na mimi nisamehe, kwani bado nakupenda"
Wakakumbatiana kwa furaha bila ya kujali ni kwanini waligombana.
Kisha wakaagana huku wakiwa na nyuso za furaha, ambazo zimejaa mapenzi.
Sabrina alirudi nyumbani kwao, alipofika nje alikutana na mama yake aliyemwambia
"Tena afadhari, kuna mgeni wako ndani huko"
"Mgeni gani? Kwani baba yupo?"
"Baba yako hayupo, kasafiri tena ila kwavile wewe una mambo mengi akashindwa kukuaga. Kuhusu mgeni, ingia mwenyewe ndani utamuona"
Sabrina alisononeka kuona baba yake ameondoka bila ya kumuaga, kwahiyo akaingia ndani kwa msononeko.
Akamkuta Fredy akiwa ndani kwao, na kumshangaa
"Kheee Fredy!"
"Nini sasa Sabrina jamani!"
"Huogopi kuja kwetu bila taarifa?"
"Niogope nini kwa mkwe wangu?"
Sabrina akamuangalia tu Fredy, kisha akamfata alipokaa.
Akatamani kumwambia ukweli kuhusu yeye na Francis, ila alishindwa kwani alijua lazima Fredy angejisikia vibaya.
"Sabrina, unafanya mambo mengi sana yasiyoeleweka. Ila mi sijali sababu nakupenda sana Sabrina, jana uliondoka bila hata ya kuniaga hadi ukasahau mkoba wako mule ndani. Ila kwa mapenzi yangu, nikauchukua na kwenda kukutunzia nyumbani....."
Sabrina akamkatisha Fredy hapo na kumwambia
"Na kwa mapenzi yako, ukaamua kumpa Francis aniletee"
Fredy akashangaa sana, ila akili yake ikamwambia kuwa ni bibi yao tu ndio aliyefanya hivyo.
"Kwahiyo, Francis ndiye aliyekuletea mkoba?"
"Inamaana hujui au?"
"Sijui ndio"
"Hebu niambie kwanza, je kuna undugu kati yako wewe na Francis?"
"Hayo nitakwambia tu, ila naomba uniletee huo mkoba wako mara moja nione"
Sabrina hakusita, moja kwa moja akaenda chumbani kwake kwa lengo la kuutoa ule mkoba ili akampe Fredy aweze kuuona.
Francis nae aliporudi kwao ile jioni, moja kwa moja bibi yake alimuita na kumuuliza
"Ule mkoba uliufikisha kwa Sabrina?"
"Ndio bibi"
"Hukuufungua kweli wewe!"
"Siwezi kufanya kitu ambacho umenikataza tayari, siwezi kabisa bibi yangu. Ila nimerudiana na Sabrina"
"Kwanini umerudiana nae? Yani ndio hapo unaponikera wewe mtoto"
"Bibi, nampenda sana Sabrina. Alikosea ndio ila nimemsamehe, nampenda kwakweli"
"Hakuna shida, je unaweza kuwa na mahusiano na mwanamke asiyeona?"
"Kivipi bibi?"
"Namaanisha kipofu"
"Mmmh! Mie sitaki mwanamke asiyeona bibi, na ndiomana nikampenda Sabrina"
"Kwasababu anaona, si ndio!"
"Ndio bibi, na macho yake yanavutia sana"
"Ila weka akilini jambo hili, hata binadamu anayeona anaweza kuwa kipofu kwa sekunde chache tu"
"Mbona sijakuelewa bibi?"
"Ndiomana nikakutuma wewe, kwavile ningemtuma Fredy angeharibu kila kitu yule na huwa hajielewi kabisa"
"Kwani angefanyaje?"
"Angechungulia ule mkoba wa Sabrina"
"Kwani ulikuwa na nini?"
"Ulikuwa na vitu vya kike ambavyo hairuhusiwi mwanaume kuviona. Usipende sana kudadisi mambo, unaweza ukawa kichaa bure"
Francis alichukua muda mrefu kuyatafakari maneno ya bibi yake bila ya jibu la aina yoyote ile.
Mwisho wa siku aliacha kama mambo yalivyo na kuendelea na mambo yake mengine.
Sabrina, alichukua ule mkoba wake na kwenda kumpa Fredy.
"Kheee ndio alikuwekea kwenye rambo kabisa!"
"Ndio, hivyo hivyo alivyouleta"
Fredy akautoa ule mkoba kwenye rambo na kuupakata, kisha akataka kuufungua.
Sabrina akamzuia,
"Sasa unataka kitu gani humo Fredy?"
"Lazima nione, labda Francis kakuwekea vibarua vyake humu"
"Mmmh Fredy acha wivu bhana"
"Siwezi hadi nione kilichopo ndani"
Ikabidi Sabrina amuachie Fredy ule mkoba aangalie sababu alijua wazi kuwa hakuna chochote cha ajabu kwenye mkoba wake.
Fredy akafungua ule mkoba, kikatoka kitu kama moshi na kuyakumbuka macho ya Fredy.
Fredy akaachia ule mkoba na kupiga ukelele wa nguvu kisha akaanguka chini.
Itaendelea
No comments:
Post a Comment