Fredy alitamani sana kujua kuwa ni kitu gani, wakati
wanaendelea na maongezi, Fredy akamfunua Sabrina
blauzi kwa kumshtukiza ili aone kile cha kiunoni.
Muda anakitazama tu ni muda huohuo Sabrina
akashtuka na ni muda huohuo Fredy nae akaanguka
chini kwenye mchanga huku damu zikimtoka
machoni.
Hofu ikampata Sabrina, alihisi kuchanganyikiwa kwa muda huo na hakujua ni kitu gani afanye ili kukabiliana na ile hali.
Aliangalia watu pale ufukweni kama kuna yeyote anayewatizama ila kila mmoja alikuwa akiendelea na mambo yake kanakwamba hawaoni kinachoendelea.
Sabrina alitamani hata akimbie na kumuacha Fredy pale ila moyo wake ulimsuta.
Akapata wazo la kumpigia simu Sakina, na hakutaka kupoteza muda kisha akachukua simu na kumpigia.
Wakati Sakina anapokea ile simu tena kabla hata ya Sabrina kuongea nae kitu chochote kile alishangaa kumuona Fredy akiinuka pale chini tena akiwa hana hata tone la damu kwenye macho wakati mwanzoni macho yake yalikuwa yakitoa damu.
Sabrina akashtuka sana na kushindwa kuongea chochote na Sakina hata Sakina mwenyewe alishangaa kwani alikazana kusema "Hallow, hallow" bila ya majibu ya aina yoyote ile hadi akaamua kuikata ile simu tu.
Sabrina alikuwa kama mtu aliyepigwa na butwaa, hakuelewa chochote kwa wakati ule.
Fredy nae alipoinuka pale akaanza kulalamika kuwa kichwa kinamuuma hivyobasi akamuomba Sabrina waondoke. Sabrina hakukataa kwani naye alishachanganyikiwa tayari na akaona kuwa labda waondoke mahali hapo na kurudi makwao tu.
Sabrina alirudi nyumbani kwao huku akiona akili yake kuwa imepagawa.
Moja kwa moja alienda kulala kwani alijihisi kuumwa kichwa pia kwa kutafakari kitu asichokielewa.
Usiku kwenye mida ya saa mbili alimsikia mama yake akimuita, alipotoka nje alishangaa kumuona baba yake.
Alifurahi sana ingawa baba yake alirudi bila ya kuwapa taarifa.
"Jamani baba, hata bila ya kusema!!"
"Nilitaka kuwafanyia surprise kama hivi mwanangu"
Wote walikuwa na furaha kwa ujio wa baba wa mwenye nyumba.
Hata Sabrina aliporudi kulala akawa amesahau yote yaliyomtokea kutokana na furaha aliyokuwa nayo kwa wakati huo wa usiku.
Kesho yake, asubuhi na mapema, Sabrina alipigiwa simu na Fredy
"Sabrina, kwanini umenifanyia hivi?"
"Nimekufanyia nini Fredy?"
"Inamaana hujui ulichokifanya!"
"Niambie Fredy, sijui chochote"
Fredy akakata ile simu na kumfanya Sabrina apatwe na mawazo kwavile hakujua kuwa ni kitu gani kimemtokea Fredy mpaka akasema vile tena asubuhi kabla bila hata ya salamu.
Sabrina akapata wazo la kwenda kwa Sakina ili amwambie yaliyojiri na pia aweze kupata ushauri kutoka kwake.
Alifika kwa Sakina na kumkuta kama kawaida yake, naye akamkaribisha vizuri sana na kama kawaida ya Sabrina hakutaka kupoteza wakati hivyobasi akamsimulia Sakina mambo yote yaliyojiri juu yake.
"Kheee mbona makubwa hivyo Sabrina!!"
"Ndio hivyo dada, yani hapa hata sijui cha kufanya dada yangu"
"Hayo mambo ni makubwa sana Sabrina, itabidi nimtafute mtu akakuulizie kuwa ni kitu gani"
"Itakuwa vizuri sana dada"
"Haya niambie, na huyo mwanaume kwani umemfanya nini hadi akakulalamikia?"
"Hata sielewi dada yangu, mi mwenyewe nimeshangaa tu akinilalamikia. Sijui ni kitu gani, itabidi nimuulize vizuri"
Sabrina akaongea mambo mengi sana na kushauriana vitu vingi sana huku wakipanga namna ya kukabiliana na matatizo yanayomzunguka Sabrina.
Baada ya kuridhika na mazungumzo yale, Sabrina aliamua kurudi kwao sasa.
Alipofika kwao, moja kwa moja akamkuta mama yake na baba yake wakiongea.
Ile alipotokea tu, mama yake akasema
"Umemuona mtoto wako! Basi ndio tabia yake siku hizi, pakikucha tu mwanao anaona miguu inamuwasha. Basi yuleee kiguu na njia kwa majirani"
"Anaendaga wapi kwani?"
"Wapi kwingine zaidi ya kwa Sakina! Yani huyo Sakina ndio amekuwa mama yake na baba yake hapo unapomuona, kila kitu anamueleza Sakina tu"
Bwana Deo akasikitika sana na kumuita Sabrina ili ajaribu kumuuliza vizuri, ila kama kawaida ya Sabrina maelezo yake yalipindapinda na kumfanya baba yake apate wazo la kufanya dhidi yake.
"Nenda tu, najua cha kufanya"
Sabrina akainuka na kwenda kuendelea na mambo yake mengine bila ya kujua kuwa baba yake ameamua kufanya kitu gani dhidi yake.
Usiku ulipofika aliamua kuwasiliana na Fredy ili kujua kuwa ni kitu gani alichomfanyia
"Ni kweli unataka kujua?"
"Ndio, nahitaji kujua Fredy"
"Kujua unajua ila tu unajipumbaza, ila kama unahitaji kujua kwa undani zaidi nakuomba kesho tuonane"
"Hilo halina tatizo Fredy, tutaonana tu"
Fredy akakubaliana na Sabrina mahali pa kukutaniana siku ya kesho ingawa hakumtajia kuwa wataenda kufanya kitu gani, na kumfanya Sabrina kuwa mgumu sana kuelewa juu ya hilo.
Sabrina alipokuwa amelala usiku, ikamjia njozi.
Alihisi kuna watu watatu wameingia kwenye chumba chake tena kwa staili zilezile ambazo wachawi huwa wanaingia, wale watu wakamnyanyua Sabrina pale kitandani kwa madawa yao kisha Sabrina akaanza kuwafata kama wanavyomuelekeza.
Yani ilikuwa kama roboti zinavyopelekwa na mashine ndivyo ilivyokuwa kwa Sabrina, akafikishwa mahali halafu akafanywa kama meza.
Wale watu walikuwa wakicheza na kula nyama, mara nyingine walimkalia kwa juu kama kiti, mara nyingine walimuwekea chakula juu yake kama meza na mara nyingine walimfanya kama punda au farasi, kwamaana kwamba walipanda juu yake kisha Sabrina akawa anawatembeza kama ambavyo farasi hufanya.
Mambo mengi yalifanyika ila kwa Sabrina ilikuwa kama njozi tu.
Muda ulifika wakaanza kumpa maelekezo mengine kama ya kumrudisha kwao, wakampeleka tena hadi chumbani kwake kitandani ila wakasahau kumuosha miguu.
Ila walipotaka kumchukua tena ili wakamnawishe, ndio hapo hapo Sabrina akashtuka kutoka kwenye ile njozi na ilikuwa ni alfajiri tayari.
Sabrina aliinuka kutoka usingizini na kukaa huku akiwaza ile ndoto kuwa ni ya aina gani! Ila alijihisi kuchoka sana kwa viungo vyake, haswaa mgongo ambao ulikuwa ukimuuma sana kwa wakati huo.
Akajaribu kujinyoosha lakini bado maumivu aliyasikia mwilini na kumfanya atafakari vizuri zaidi kuwa ile ni ndoto au ni kweli.
"Mbona sijielewi sasa! Hivi nilikuwa naota au ni kweli ilikuwa vile usiku!!"
Hakupata jibu, ila alipojitazama miguuni alishtuka zaidi baada ya kuona miguu yake imejaa vumbi
"Mungu wangu, inamaana ni kweli? Inamaana wachawi walikuja kunibeba usiku!"
Hofu ikamjaa na kumfanya palipokucha vizuri tu aende kwa Sakina kumuelezea yale mambo.
Alipofika kwa Sakina hakumkuta na kumfanya ajiulize kuwa asubuhi ile amekwenda wapi, na alipojaribu kupiga simu yake haikupatikana. Ilikuwa ni ajabu sana kwa Sabrina na kumfanya apatwe na mawazo zaidi na kuamua kurudi kwao tu.
Alimkuta baba yake akiwa amekaa sebleni na kumsalimia
"Kumbe ni kweli mwanangu kuwa ikifika asubuhi miguu inakuwasha!"
"Hapana baba, nilikuwa hapo nje tu"
"Hapo nje kwetu ndio siku hizi kuna vumbi kiasi hicho mwanangu!!"
Sabrina akajitazama tena miguuni, akatamani kumwambia baba yake ukweli kuhusu mambo yaliyojiri na ndoto aliyoota usiku lakini midomo yake ilikuwa mizito kusema na kujikuta akimuangalia tu baba yake bila ya kumwambia kitu cha aina yoyote ile.
Deo alimtazama sana binti yake na kujaribu kuitafakari akili ya mwanae bila ya majibu yoyote yale, kisha akamruhusu kuwa aende akaendelee na shughuli nyingine.
Sabrina alienda kuoga moja kwa moja.
Alipokuwa anaoga alijishika kiunoni na kuona hali sio ya kawaida kwani ile kamba haikuwepo tena kwenye kiuno chake.
Sabrina alijaribu kutafakari bila majibu,
"Imeenda wapi ile kamba? Mbona maajabu haya! Au yule bibi alinihurumia akaitoa?"
Sabrina hakupata jibu zaidi ya kujiongezea maswali na mawazo katika kichwa chake.
"Sijielewi kwakweli, kitu gani kimetokea kwangu? Na kimetokeaje? Na kwanini kimetokea? Mbona sipati jibu?"
Hakuwa na raha kabisa, hata alipomaliza kuoga bado alikuwa na mawazo na kumfanya ashindwe kufanya kitu cha aina yoyote ile.
Mchana akapigiwa simu na Fredy
"Sabrina, kama tulivyoongea usiku. Tukutane pale Mitini guest house"
"Sawa hakuna tatizo ila hujaniambia kuwa tunaenda kufanya nini hapo"
"Nimekwambia utajua huko huko"
"Poa, hakuna tatizo"
Fredy akashangaa kwa Sabrina kuitikia haraka hivyo wakati usiku wa jana yake tu alikuwa akipinga swala hilo ingawa badae alikubali kwa kusitasita ila leo alikubali moja kwa moja bila mashaka ya aina yoyote ile.
Mawazo ya Sabrina yalimpelekea kwamba Fredy anahitaji kulala nae na ndiomana kamwambia wakutane huko kwenye nyumba za kulala wageni.
"Mmh nitaweza kweli kulala na mwanaume? Sijui itakuwaje, nitajua hukohuko ila bora kamba imetoka"
Sabrina hakuwahi kukutana kimwili na mwanaume yeyote yule na ile kamba ndiyo iliyokuwa ikimpa mashaka zaidi kuwa hakuna mwanaume atakayeweza kumuelewa ukizingatia kamba yenyewe ilikuwa na muonekano wa hirizi.
Kwavile sasa ile kamba haikuwepo tena kiunoni mwake, akaona sasa ni wakati muafaka kwake kwenda kujaribu ukizingatia Fredy mwenyewe ndiye aliyetaka na kumuita.
Mida ilipofika, Sabrina alijiandaa na kwenda kumuaga mama yake
"Haya wapi sasa?"
"Naenda kwa rafiki yangu mama"
"Sabrina, Sabrina. Kuwa makini mwanangu na hizo safari zako zisizoeleweka"
"Usijali mama, niko makini"
Kisha akamuaga na kuondoka.
Safari ilikuwa ni moja kwa moja alikopanga kukutana na Fredy.
Njiani akakutana na mmama mmoja, yule mmama alipita karibu na Sabrina kisha akacheka.
Sabrina akamuangalia yule mmama na kumshangaa kuwa kilichomchekesha ni kitu gani, kisha yule mmama akamwambia Sabrina
"Na bado"
Halafu akaondoka, Sabrina alikuwa na mshangao tu pale aliposimama kwani hakumuelewa kabisa yule mmama.
Wakati anaendelea na safari, wazo likamjia. Taswira ya yule mmama ikamji kuwa ni kati ya wale watatu aliowaona ndotoni ambapo bado anamashaka kuwa ni ndoto au ni ukweli. Ila kwa ile hali ilivyoonekana akapata jibu kuwa ile haikuwa ndoto tu bali ni ukweli mtupu.
Akaamua kuendelea na safari yake ingawa mawazo yaliendelea kuitafuna akili yake.
Alifika mahali walikopanga kukutana na Fredy, kisha Sabrina akampigia simu Fredy ili ajue alipo
"Nishafika Fredy uko wapi?"
"Ingia moja kwa moja ndani, chumba namba tano"
Sabrina hakujishauri sana, alipokata simu tu akaelekea ndani hadi kwenye chumba alichoelekezwa na Fredy.
Alipofika alifungua mlango na kumkuta Fredy amejilaza kitandani.
Moja kwa moja Sabrina alimuuliza Fredy,
"Mbona umejilaza hivyo?"
"Wee njoo tu"
Sabrina akasogea hadi alipo Fredy na kukaa huku mapigo yake ya moyo yakienda kwa kasi sana, hata Fredy aligundua hiko kitu kutoka kwa Sabrina.
Fredy akainuka na kwenda mlangoni kisha akafunga vizuri ule mlango kwa funguo na kurudi kukaa karibu na Sabrina, kila alipomsogelea ndivyo mapigo ya moyo ya Sabrina yalivyozidi kwenda kwa kasi ya ajabu.
Fredy akainua mkono wake na kumshika Sabrina kwenye kifua chake, karibia na mapigo ya moyo.
"Mbona moyo wako unadundadunda sana?"
Sabrina hakujibu chochote zaidi ya kumtazama tu Fredy.
Kisha Fredy akajilaza tena chali na kumwambia Sabrina
"Jilaze kama mimi"
Sabrina bila kubisha nae akajilaza chali, halafu Fredy akakaa na kumfunua Sabrina blauzi yake na kuanza kushika kiuno chake, Sabrina alijihisi kusisimka mwili mzima kwavile alivyokuwa akishikwa.
Gafla Fredy aliacha kumshika Sabrina na kumuuliza
"Kamba yako ya kiunoni iko wapi?"
Sabrina akashtuka baada ya kugundua kwamba Fredy anakumbukumbu juu ya ile kamba ya kiunoni mwake.
Sabrina alikaa na kumuangalia Fredy kisha akamjibu
"Sijui"
Fredy nae akamwambia Sabrina
"Ila mi najua"
Kisha Fredy akajilaza chali na kumwambia tena Sabrina
"Nifanye kama nilivyokufanya wewe"
Sabrina akaogopa, ila akajaribu na kumfunua shati Fredy.
Hapo Sabrina alishtuka sana kwani ile kamba ilionekana kwenye kiuno cha Fredy.
Ila kabla Sabrina hajafanya chochote cha zaidi, yule bibi ambaye alimfunga kamba hiyo Sabrina alitokea mbele yao.
Itaendelea
No comments:
Post a Comment