Akaenda nae chumbani kwa bibi yake, Sabrina kufika
pale macho yake yakagongana na macho ya yule bibi
na kufanya ashtuke kwani alikuwa ni yule yule
mmama aliyempiga usiku.
Sabrina akaogopa sana na hakuweza kuzuia uoga wake kwani yule bibi alimkazia sana macho na kumfanya atetemeke na kutoka nje huku anakimbia.
Francis akamfata nyuma na kumuuliza,
"Kwani nini Sabrina?"
Kama kawaida yake ya kuropoka akajikuta akimwambia Francis
"Yule bibi ni mchawi"
Bila kujua kama kauli hiyo ingewezaje kumbadilisha Francis
"Unasemaje Sabrina?"
Sabrina akaongea kwa kujiumauma sasa na kujilaumu kuwa kwanini ameropoka vile
"Samahani Francis"
"Yani unamuita bibi yangu mchawi halafu unaniomba samahani kirahisi tu!"
"Naomba unisamehe Francis"
Francis alikuwa amechukia sana kwa kile kitendo cha bibi yake mpenzi kuitwa mchawi
"Yani siamini kabisa kama wewe Sabrina unaweza kumuita bibi yangu mchawi, siamini kwakweli"
"Nisamehe jamani"
"Usitake nitende dhambi Sabrina, tafadhari naomba uende. Kwa usalama wako nenda"
Kwa jinsi Francis alivyokuwa akiongea kwa ukali ilimbidi Sabrina aondoke huku moyo ukimuuma sana na kujilaumu kwa kuropoka kwake ingawa ilikuwa ni kweli ila ndio ilishamponza tayari.
Wakati Sabrina anatoka kwenye ile nyumba, akakutana na kijana aliyekuwa anataka kuingia mule ila alipomuona Sabrina akitoka huku machozi yakimbubujika alimuonea huruma na kumfata.
"Nini tatizo dada?"
"Hamna kitu"
"Mbona unalia sasa?"
Sabrina alizidi kutokwa na machozi tu, yule kijana akamshika Sabrina mkono na kumrudisha ndani ya geti la ile nyumba ili amuhoji vizuri kinachomliza.
Alipomrudisha tu, Francis nae alitoka nje na kuchukizwa kwa kuendelea kumuona Sabrina eneo lile, kisha akamwambia nduguye aliyemshika Sabrina mkono
"Fredy, mwache huyo malaya aende zake"
"Kwani amefanyaje?"
"Achana nae bhana"
Kile kitendo cha Sabrina kusikia kuwa yeye akiitwa malaya kilimuuma sana tena zaidi hata alivyoumia mwanzo kwani hakuamini kama Francis huyu aliyemwambia kuwa anampenda kwa vyovyote vile leo hii anamfukuza na kumuita malaya kisa tu kaongea ukweli, roho ilimuuma sana na kuondoka huku akilia zaidi ila Francis hakujali chochote.
Fredy, alimfata Francis ili kumuuliza vizuri
"Kwani kafanyeje yule?"
"Mwanamke fala sana yule, ndio kwanza leo namleta halafu anamuita bibi yangu mchawi! Na akafie mbele huko"
"Kwahiyo ni sababu hiyo tu iliyokufanya umfukuze?"
"Tena sio kumfukuza tu, yani hata kumuona sitaki yani sitaki kabisa"
"Mmh ulimpenda kweli yule mwanamke wewe?"
"Nilimpenda ndio ila siwezi kuvumilia upuuzi kama huu kwakweli"
Francis alionekana kuwa na hasira sana kupita maelezo ya kawaida na kuingia tena ndani.
Moyo wa Fredy bado ukamtuma kuwa amfate yule binti, kisha akatoka na kuanza kumfatilia.
Kwavile Sabrina alijihisi kuchanganyikiwa hadi akasahau njia waliyokuja nayo mwanzo na kujikuta akipita njia nyingine.
Isingekuwa Fredy kumfata basi angepotea leo.
Fredy alimuuliza,
"Kwani unaenda wapi?"
"Nataka kwenda kupanda daladala nirudi nyumbani"
"Dah huko uendako unapotea dada, twende nikupeleke stendi"
Kisha Sabrina akaanza kufatana pamoja na Fredy ambaye alipanda nae daladala hadi akamfikisha kwao kabisa.
"Asante sana"
"Usijali, mimi ni kati ya wanaume walioumbwa na moyo wa huruma katika dunia hii. Nimekuhurumia sana ndiomana nikafanya haya"
"Nashukuru sana kaka"
"Naitwa Fredy, vipi wewe jina lako!"
"Naitwa Sabrina"
"Sawa Sabrina tutawasiliana basi"
Kisha Fredy akampa namba zake Sabrina na kumuaga pale halafu akaondoka.
Sabrina aliingia ndani kwao ila mama yake hakuwepo na kumfanya apate muda muafaka wa kuwaza yanayomsibu.
"Mmh sijui nikamuhadithie dada Sakina! Lakini ataniona ni mpumbavu. Ngoja nijaribu kukaa nalo moyoni huku nikiombea Francis anisamehe jamani"
Alikuwa akiwaza sana huku akiumia moyoni mwake.
Baada ya masaa kupita akajaribu kumpigia simu Francis lakini simu yake haikupokelewa na kumfanya aumie zaidi na zaidi.
Muda kidogo alifika mgeni nyumbani kwao na mgeni huyo alikuwa ni Sakina
"Kheee Sabrina, umerudi saa ngapi?"
"Muda tu, karibu"
"Mi nimemfata mama yako"
"Na hata hayupo"
Ila Sakina alimgundua Sabrina kuwa hayupo sawa ingawa kila alipomdadisi kuhusu alipotoka hakusema ukweli na kuishia kujibu kuwa ni nzuri tu.
"Niambie ukweli Sabrina, najua una matatizo niambie tafadhari"
Baada ya kumbana sana, Sabrina akaamua kusema ukweli kwa Sakina kwa yale yaliyojiri
"Mungu wangu Sabrina, kheee kwani wewe ulimchapa viboko vingapi jana"
Napo ilibidi aseme ukweli kuwa alimchapa viboko vinne tofauti na alivyoambiwa
"Hayo majanga mdogo wangu, kwanini ulifanya tofauti na nilivyokwambia? Haya swali jingine sasa, kama huyo bibi ni bibi yake huyo Francis kwanini alikufata wewe kukuwangia?"
"Hata mi mwenyewe sielewi dada yani sielewi kabisa na hata sijui cha kufanya maana Francis nampenda ila sijui itakuwaje. Sijui kama ataendelea na mimi kwa jinsi alivyonifukuza"
Sakina alimuhurumia sana Sabrina na kumpa moyo
"Usijali, atakusamehe tu wala usiwe na wasiwasi"
Muda mwingi Sabrina alijilaumu mdomo wake kwa kuropoka mambo yasiyotakiwa kuropokwa kama hili linalompa mawazo kwasasa na kumkosesha raha ya maisha na kumfanya akose furaha.
Usiku ulipofika alimkumbuka sana Francis lakini kila alipojaribu kumpigia simu, simu yake haikupokelewa. Hata alipojaribu kumtumia ujumbe, jumbe zake hazikujibiwa na kumfanya azidi kupatwa na mawazo yasiyo rasmi.
Akaamua kuitafuta ile namba aliyopewa na Fredy ili amuulizie Francis kwa Fredy
"Unaongea na Sabrina hapa"
"Ooh! Kumbe Sabrina, nipe khabari"
"Namuulizia Francis, anaendeleaje?"
"Yuko poa, ila acha kujiumiza kichwa kwa hayo mambo wangu. Utaumia bure, kesho kama unamuda basi tuonane. Sawa?"
"Hakuna tatizo basi"
Akamuaga na kukata simu huku akiamini kuwa huyu Fredy ndiye atakayemsaidia yeye kuwa na mahusiano tena na Francis.
Kesho yake alimuaga mama yake na kwenda kuonana na Fredy kama ambavyo walipanga kwenye simu.
"Kwani Francis mlifahamiana vipi?"
Sabrina alimueleza Fredy kwa kifupi tu.
"Nimekuelewa, sasa una mpango upi baada ya yote"
"Nampenda Francis, nahitaji anisamehe ili niwe nae tena"
"Poa usijali, ila kama akikataa kukusamehe usiwe na shaka. Wengine tupo hapa"
Aliongea kwa utani lakini ndio alikuwa akimaanisha hivyo kwani nae alijikuta akimpenda Sabrina na kuvutiwa nae.
Waliongea mambo mengi sana, kisha wakaagana na kuondoka.
Sabrina alirudi kwao huku akiwa na imani kwamba atasaidiwa na Fredy kuweza kurudiana na Francis bila kujua kwamba Fredy nae kashampenda tayari na hatoweza kufanya kitu hiko cha kumsaidia.
Maisha yao nayo yakaendelea kwa mtindo huo huku Fredy akidumisha mawasiliano na Sabrina.
Toka lile sakata la Sabrina kumpiga yule mchawi usiku, hakuweza tena kufatwa na hao wachawi kwa kipindi hiko na bado hakujua kwanini bibi yake Francis alimfata.
Alitamani sana kujua ni kwanini ila hakuweza kujua kabisa.
Mawasiliano baina yake na Fredy yalishamiri sana.
"Naomba kesho nikutembelee kwenu hapo Sabrina"
"Karibu tu hata usijali, wee njoo tu"
Fredy alifurahi kwani alijua ndio sehemu ya kwenda kubwaga ya moyo wake.
Kesho yake Fredy alienda kwa wakina Sabrina na kumkuta, ile leo hakumkuta mama yake na Sabrina kwavile alitoka.
"Eeh niambie Francis anaendeleaje, maana hapokei simu zangu wala hajibu meseji zangu"
"Francis kanipa ujumbe kuwa usimsumbue tena, na hivi ninavyokwambia ana mwanamke mwingine. Kwakweli nimekuhurumia sana Sabrina kwa kung'ang'ania sehemu usiyotakiwa wakati wapo watu wa maana tu wanaokuhitaji kushinda hata huyo Francis"
"Wakina nani hao?"
"Mimi hapa, kwakweli nakupenda sana Sabrina. Siku zote hizi nimekuwa nikikupenda sema tu sikujua nianzie wapi kukwambia"
"Mmmh Fredy!"
"Sikutanii Sabrina, mi ni msema kweli na huo ndio ukweli kutoka moyoni mwangu"
"Wewe si ndugu yake na Francis! Halafu si unamwanamke wewe!"
"Sina mwanamke mie, nakupenda wewe Sabrina. Ni kweli Francis ni ndugu yangu ila yeye alikutamani, mimi ndiye ninayekupenda. Mungu alifanya makusudi kukukutanisha wewe na Francis ili uweze kukutana na mimi mwenye mapenzi ya dhati na wewe. Sina nia mbaya naye zaidi ya upendo wa dhati"
Maneno ambayo Fredy alikuwa akiyaongea yalimuingia akilini Sabrina na kujikuta akivutiwa nae huku akiwaza kuwa anayoyasema yanaweza kuwa yana ukweli ndani yake.
"Basi tutaongea vizuri kwenye simu badae"
Hakutaka kumjibu kwa muda huo kwavile bado alimpenda Francis ingawa maneno ya Fredy nayo yalimuingia kichwani.
Wakaongea mengi kisha Fredy akaaga na kuondoka halafu Sabrina akamsindikiza.
Wakati Sabrina anarudi kutoka kituoni alipotoka kumsindikiza Fredy.
Njiani alijikwaa kwenye jiwe na kuanguka, alipojitahidi kuinuka aliona damu zikimtoka kwenye kidole, alikuwa amechunika ngozi kwenye dole gumba la mguu wa kushoto na damu kiasi zilimwagika pale.
Alijikongoja hadi nyumbani kwa Sakina kwavile hapakuwa mbali sana na alipojikwaa.
Sakina alipomuona alimshangaa
"Vipi mbona unachechemea Sabrina?"
Sabrina akamuonyesha kile kidole na kumueleza alivyojikwaa.
Sakina akachukua pamba na kumfuta Sabrina kisha akamfunga pale kwenye kidole.
Wakati anamalizia kumfunga ikawa kama mtu aliyekumbuka kitu na kumuuliza
"Umejikwaa sehemu gani?"
"Pale karibia na kiwanja, pale kwenye njiapanda"
"Mmmh!!"
"Mbona unaguna?"
Akamfunga haraka haraka na kumwambia
"Hebu twende ukanionyeshe"
Wakainuka na kwenda mahali alipojikwaa Sabrina.
Kufika pale, walikuta ile sehemu ambayo damu ya kwenye kidole cha Sabrina imemwagika ikawa kama mtu kaja kuichota na mchanga wake na kuacha kijishimo.
"Umeona Sabrina?"
"Nimeona"
"Inamaana hapa kuna mtu kaichota damu yako"
"Sasa kwanini kaichota?"
"Unafatiliwa Sabrina, yani ni bora tungekumbuka muda ule ule ila bado hatujachelewa sana. Nisubiri kidogo tena hapa hapa usiondoke"
Sakina akaondoka na kumuacha Sabrina mahali pale.
Baada ya muda kidogo akarejea na kimfuko kidogo, ndani yake alibeba majivu na kipande cha mkaa, kisha akamwambia Sabrina
"Kwavile yeye alisahau kufukia hiki kishimo wakati anachukua damu yako basi tutakifukia sie"
Akachukua kale kamkaa kadogo na kuweka kwenye kale kashimo halafu akaweka majivu juu yake kisha akasawazisha na mchanga pale juu na kumwambia Sabrina kuwa waondoke.
Waliporudi nyumbani, Sakina akamuonya tena Sabrina
"Usimwambie mama yako"
"Ila dada leo hebu niambie kwanini hutaki nimwambie mama?"
"Mama yako yule ni mtu wa maombi kwahiyo ataharibu kila kitu ndiomana sipendi umwambie"
"Hapo nimekuelewa sasa"
Kisha akarudi nyumbani kwao na kumkuta mama yake akiwa ndani.
"Haya niambie, pale njiani mlikuwa mnafanya nini na Sakina wako?"
Sabrina akashtuka kugundua kwamba mama yake aliwaona, ikabidi amdanganye
"Tulikuwa tunaongea tu mama, kuna mgeni tulimsindikiza"
"Endelea kunificha mwanangu ila ipo siku kila kitu kitakuwa peupe"
Joy alihisi tu kuwa kuna vitu mtoto wake anamficha ila hakutaka kumlazimisha sana kuwa amwambie kwani alijua ipo siku lazima atasema yeye mwenyewe bila hata ya kushurutishwa.
Siku hiyo ikapita, hata usiku wake ukapita vizuri kabisa bila ya tatizo lolote.
Kitu kimoja tu kilichomtatiza Sabrina ni kamba yake ya kiunoni na ilikuwa ni siri yake yeye na Sakina, hakutaka mtu mwingine ajue hiyo siri haswaa Fredy.
Wakati akiwaza kuhusu huyo Fredy na kukiambia kichwa chake kiamue moja kama kumsubiri Francis arudishe moyo au kuwa na Fredy.
Muda huo huo akapigiwa simu na huyo Fredy
"Naomba tuonane Sabrina"
Sabrina hakukataa na wakapanga mahali pa kwenda kukutana, ambapo waliona kuwa sehemu nzuri ni ufukweni ili waweze kufikia muafaka wa swala lao.
Muda wa kuonana ulifika, wote wawili waliwahi kufika eneo la tukio.
Walikaa kwenye mchanga na kupeana habari mbalimbali.
Wakati wakizungumza, Fredy alijikuta akipatwa na matamanio zaidi juu ya Sabrina na kumfanya awe nae karibu zaidi hata aweze kumshikashika ili aridhike.
Wakati yupo karibu vile, akazungusha mkono wake kwenye kiuno cha Sabrina na kujikuta akiishika ile kamba.
Bila uvumilivu akamuuliza Sabrina
"Unavaaga shanga?"
Sabrina nae akashtuka na kujibu
"Hapana, sivaagi"
"Sasa hii naishika kwenye kiuno chako ni nini"
Sabrina akaogopa kujibu na kuutoa mkono wa Fredy kwenye kiuno chake.
"Niambie Sabrina, kitu gani hicho?"
"Sio kitu"
Fredy alitamani sana kujua kuwa ni kitu gani, wakati wanaendelea na maongezi, Fredy akamfunua Sabrina blauzi kwa kumshtukiza ili aone kile cha kiunoni.
Muda anakitazama tu ni muda huohuo Sabrina akashtuka na ni muda huohuo Fredy nae akaanguka chini kwenye mchanga huku damu zikimtoka machoni.
Itaendelea
No comments:
Post a Comment