JE HAYA NI MAPENZI!! 82: - UHONDO KITANDANI

Hot

Post Top Ad

https://play.google.com/store/apps/details?id=chumba.cha.wakubwa

Wednesday, February 19, 2020

JE HAYA NI MAPENZI!! 82:





Hakuna aliyemjibu, Sam akasogea na kumshika
bega Sabrina kamavile mtu anayehitaji jibu.
Ila kabla ya yeyote kati yao kusema chochote,
wakashangaa kumuona Sam akianguka chini na
kuwa kimya kabisa.
Ikawa heka heka nyingine sasa ya kumuinua Sam pale chini huku wakitaka wampakize kwenye gari na wampeleke hospitali.
Ila Dorry akawapinga,
"Hapana, msimpeleke hospitali"
Mama wa Sabrina akauliza kwa mshangao,
"Kwanini?!"
"Mimi ndio nimekuja nae, tusaidiane kumuingiza ndani ila tusimpeleke hospitali."
Ikabidi wasaidiane nae pale na kumuingiza ndani, kisha kumlaza sehemu nzuri kidogo ambapo Dorry aliwataka wakamlaze kitandani kwa Sabrina nao wakafanya hivyo ila kila mmoja kati yao alimshangaa Dorry hata yule dereva wa gari za kukodi aliamua kuondoka tu ili kukwepa lingine la kuzuka.
Wote kwa wakati huo walisahau kabisa kuhusu mguu wa Sabrina na kukazana kujadili kuhusu Sam.

Muda kidogo wakamuona Sam akitoka chumbani, naye alifika na kuwashangaa.
"Jamani, nimefikaje hapa?"
Wote wakashtuka kwa kumuangalia Sam na hakuna aliyemjibu, Sam naye aliwatazama kwa zamu kisha akaangalia saa yake ya mkononi na kuona wazi kuwa muda umeenda sana.
"Aah! Mpaka muda huu, ni kitu gani kimenileta huku? Ngoja niende ofisini kwanza nikitoka nitapita ili mniambie vizuri"
Sam akatoka na kuondoka zake.
Dorry naye akainuka na kumuacha pale Sakina, Sabrina na mama Sabrina kisha yeye akaondoka.
Wote walibaki wameduwaa na kumfanya mama Sabrina aulize tena,
"Ni kitu gani hiki jamani?"
"Hata sielewi"
Wakapata na wazo la kuangalia mguu wa Sabrina, nao ulionekana kuwa mzima kabisa yani haukuvimba wala kuwa na jeraha lolote.
"Hivi haya ni maajabu, miujiza au ni kitu gani jamani? Au naota mimi mama Sabrina jamani"
Kila mmoja hakuelewa kabisa, ikabidi Sakina awaage pale na kwenda nyumbani kwake ili akamuulize vizuri Dorry kwani hata yeye alibaki njiapanda.
Kwahiyo pale akabaki Sabrina na mama yake,
"Vipi na maumivu ya mguu sasa?"
"Siyasikii kabisa mama, kwani ni mambo gani yanatendeka haya? Ila namshukuru Mungu  nimepona huu mguu maana ulikuwa unaniuma balaa"
"Pole sana, ila tutajua tu kisa na mkasa. Yani hadi sasa naona kamavile naota hata siamini haya yaliyotokea jamani"
Hakuna aliyeamini ila kila mmoja aliamua kuendelea na mambo mengine tu.

Sakina alifika nyumbani kwake na kumkuta Dorry akiwa amejiinamia tu.
Akamfata kwa karibu na kumuuliza,
"Hivi imekuwaje Dorry, hebu niambie maana sielewi kabisa"
"Hata mimi sielewi ila sina budi kukueleza mama"
Sakina akatulia kwa makini akingoja kuelezwa na Dorry, naye akamueleza yote toka alivyopigiwa simu na maelekezo aliyopewa,
"Kwahiyo yote niliyoyafanya leo ni maelekezo niliyopewa na Jeff kwenye simu"
"Unauhakika ni Jeff amekupa maelekezo hayo?"
"Ndio ni Jeff mama"
"Mmh! Mbona hayo maelekezo kamavile umepewa na mganga wa kienyeji? Hivi Jeff mwanangu na mambo hayo ya utaalamu wapi na wapi?"
"Kama huamini mama mpigie simu umsikie mwenyewe, maana hata mimi nimeshangaa   ukizingatia haya mambo ni mageni kabisa kwangu"
Sakina alijikuta akiguna na kuchukua simu yake, akaangalia salio kwanza alipoona lipo la kutosha akampigia simu mwanae kumuuliza.
Baada ya salamu akaamua kumuuliza,
"Mwanangu kwani siku hizi umekuwa mganga wa kienyeji?"
"Kwanini mama?"
"Ila twashukuru sababu mgonjwa amepona, ila niambie ulivyo sasa mwanangu?"
"Kwani vipi mama? Mbona sikuelewi?"
"Jana umempigia simu Dorry hapa, umempa maelekezo ya kiganga kabisa ila yamesaidia"
"Nimempigia simu Dorry? Kwanza Dorry yupi?"
"Si huyu Dorry mchumba wako mwanangu"
"Kwanza kabisa mama huyo Dorry sio mchumba wangu, pili sijampigia simu kwani hata namba yake sina nilishaifutaga zamani sana"
"Khee wewe Jeff una wazimu au? Dorry sio mchumba wako wakati ana mimba yako hapa!"
Dorry naye akaishiwa pozi kwa yale mazungumzo kwani aliona wazi mamamkwe wake akizidi kuharibu kwa kusema kuwa Dorry ana mimba.
Muda huo Jeff naye  alikuwa akimshangaa mama yake.
"Mama jamani mama yangu, sijawahi kuwa na mahusiano na huyo Dorry. Kwakifupi sio mchumba wangu wala mpenzi wangu. Sasa hiyo mimba unayosema imetokea wapi jamani mama....."
Simu ikakatika kwani vocha nayo ilishakata.
Sakina akamuangalia Dorry na kujikuta wakitazamana,
"Mbona maajabu haya, Jeff anasema hajakupigia simu na wala haitambui hiyo....."
Kabla hajamaliza, Dorry alidakia kwa kushika simu yake,
"Kama hajanipigia mbona namba yake ipo humu kwenye simu kuwa alinipigia"
Huku akijaribu kuipekua ili amuonyeshe Sakina.
Cha kushangaza ile namba hakuiona na kumfanya ajishangae mwenyewe.
"Sasa namba imeenda wapi?"
"Unaniuliza mimi wakati simu yako unayo mwenyewe muda wote"
"Ndio, ila namba siioni humu. Mbona mauzauza haya!!"
Dorry hakuelewa kabisa, akaingia chumbani na kutoka nje na begi lake kisha kumuaga mama mkwe wake.
"Sasa unaenda wapi?"
"Naenda nyumbani mama, acha nikatafakari haya nyumbani kwetu kwamaana nashindwa kuelewa kabisa mama yangu yani sielewi kitu hapa."
"Sasa kuondoka ndio suluhisho jamani?"
"Mama acha tu, akili ikikaa sawa nitarudi hata kesho"
Dorry aliogopa kuulizwa tena kuhusu ile mimba yake na kuamua kuondoka kwanza.
Sakina nae akaona kwake hapakaliki na kuamua kwenda kwakina Sabrina kwa muda.

Sam akiwa ofisini, wafanyakazi wake walimshangaa kwani alionekana ni mtu mwenye mawazo halafu shati lake lilionekana kuwa na vumbi baadhi ya sehemu ila waliogopa kumuuliza.
Muda kidogo Sam akafatwa na Rose yule rafiki wa Neema,
"Shemeji, kuna tatizo kidogo nakuomba twende tafadhari"
"Wapi tena?"
"Nyumbani kwa Neema"
Sam aliamua kutoka pale ofisini na kuondoka na Rose hadi nyumbani kwa Neema ambapo walimkuta Neema akiwa hoi kabisa.
"Sasa mtu anaumwa hivyo unashindwa kumpeleka hospitali kweli Rose? Kwanini sasa?"
"Tatizo sio ugonjwa wa hospitali"
"Ni ugonjwa wa wapi sasa?"
"Subiri"
Rose akachukua kikombe na kuweka maji, alikuwa na karatasi mkononi akafungua na kutoa kitu kama ungaunga akachanganya na maji, kisha akagawa yale maji kwenye vikombe viwili.
"Shemeji, hii ni dawa inatakiwa unywe wewe na Neema, yani kunywa kwako hii dawa ndio kuokoa maisha ya Neema."
"Mmh! Mambo gani haya? Ndio wanaita ushirikina au ni vitu gani hivi?"
"Sio ushirikina shemeji, kuna bibi yetu ndio kanipa hii dawa. Yani Neema anaumwa hivi sababu ya kukupenda wewe sana shemeji"
"Mmh hebu mpe kwanza Neema hiyo dawa halafu mi ndio nitakunywa"
Rose akampa Neema ile dawa na kuinywa yote huku akiumwa sana, kisha Sam naye akainywa ile dawa na muda huo huo Neema akawa mzima.
Sam alijikuta akistaajabu ila alishindwa kuuliza kuwa kwanini inakuwa vile.
Walikaa pale hadi jioni kabisa kisha Sam akawaaga na kuondoka zake.

Sakina nae akaenda kumueleza mama wa Sabrina alichoambiwa na Dorry na jinsi alivyojibiwa na Jeff baada ya kumuuliza.
"Khee sasa mbona haya ni mauzauza?"
"Ni mauzauza kweli mmh!"
"Ila bora mwanangu ni mzima, mengine tumuachie Mungu tu. Kwahiyo Dorry yuko wapi?"
"Mmh kaondoka hata sijui kwanini? Labda anaogopa mauzauza"
"Mmh mnanikumbusha mauzauza ya wifi yangu Sabrina leo"
"Yalikuwaje kwani"
"Mmh ni historia ndefu na sipendi ijirudie kwenye maisha yetu maana yalikuwa majanga tena majanga haswaaa"
Sakina akatamani kuyajua hayo majanga ila kwavile mama wa Sabrina aliyakatishia njiani hakuweza kumuuliza zaidi.
Ila bado aliendelea kuwepo pale kwakina Sabrina,
"Yani leo sijisikii hata kurudi kwangu"
"Kwanini uhangaike Sakina? Vyumba vipo hapa vya kutosha tu, leo lala hapa kwetu"
Wakakubaliana hivyo.

Sam alipofika nyumbani kwake akajaribu kutafakari matukio bila ya kupata jibu la aina yoyote.
"Niliondoka hapa asubuhi nikielekea kazini. Sasa niliendaje kwakina Sabrina? Na iweje  nikajikuta nimelala mule ndani kwao? Mbona sielewi, eti Neema kaumwa yani dawa ninywe mimi halafu apone yeye. Mbona nimekuwa mpumbavu kiasi hiki! Kwani nina matatizo gani?"
Sam alijihoji bila ya kupata jibu la maswali yake kabisa.
Na kuamua kulala tu.

Kesho yake, Neema na rafiki yake Rose waliamua kujadiliana juu ya hali halisi.
"Kwakweli Rose nimechoka yani nimechoka kabisa, ipo siku nitakufa najiona jamani"
"Unachokaje mapema hivyo Neema? Bado hata hatujavuna matunda unachokaje kwa mfano? Dawa ni kupata mimba ya Sam tu halafu ndio tuachane na hizi dawa sababu lazima atalea mtoto wake"
"Hivi kwa unavyomuona huyu Sam kuna hata dalili ya kulala nae kweli? Mi naona tunamtesa bure tu Sabrina. Ila mi nimechoka shoga yangu, maana huyo Sam akienda tu kuonana na huyo Sabrina mi nakuwa hoi. Unajua nitakufa mimi bila sababu!"
"Maji tumeshayavulia nguo shoga yangu hatunabudi kuyaoga tu. Hapa hakuna la kufanya, ndiomana mimi nilipoona jana hali imekuchachia nikaamua kukimbilia kwa yule mganga ndio akanipa ile dawa"
"Kwahiyo ndio ilitakiwa tunywe wote mi na Sam?"
"Ndio, unadhani ningempa peke yake angekubali? Yule mganga kiboko. Ila leo hebu twende akatueleze vizuri maana kama mambo yenyewe haya wakionana tu unakuwa hoi hata mimi yatanishinda"
Wakakubaliana pale kuwa waende wote kwa mganga ili awaelekeze vizuri.
Kisha wakajiandaa na kuondoka.

Walifika kwa yule mtaalamu wao ili waweze kupata maelezo zaidi.
Yule mganga aliwaangalia kwa jicho kali sana,
"Jamani hapa tunacheza na moto, jana nilikupa tu dawa kuepusha ya mbali ila cha msingi mnatakiwa kumdhibiti yule mwanaume asiende kabisa kule. Jitahidi umuwekee ile dawa tena kwenye chakula"
"Ila kwanini unasema tunacheza na moto?"
"Kuna kitu nakiona kwa huyu dada tunayemfatilia, nadhani kuna kitu kinamlinda na ndio kilichopelekea yule kijana aende na alipofika   kauvuta ugonjwa wote na kuja kwako"
Yule mganga akawaonyesha kwenye kioo chake ambapo ilionekana kama video.
Walimuona Sam alipofika kwakina Sabrina na kumgusa Sabrina kisha akaanguka na kumpeleka chumbani.
Neema na Rose walishangaa na kuduwaa,
"Khee ni wachawi nini?"
"Bado sijajua ila kuna kitu nitachunguza ili nijue ilikuwaje mpaka kuwa hivi. Ila kwasasa hivi mkawe makini sana."
Walimalizana nae pale na kuamua kuondoka.
Wakiwa njiani walijidadisi sana,
"Ila huyu mganga ni noma, unajua Sabrina hatakiwi kabisa kukanyaga nyumbani kwa Sam ndiomana akang'atwa na nyoka!"
"Naelewa hilo Rose, ila kama hawa wakina Sabrina ni wachawi hapa kazi ipo sababu itakuwa tunavutana kwa kumpa madawa Sam"
Rose akacheka,
"Ndiomana wanaume wanakuwaga vichaa jamani. Ila usiwe na shaka Neema sababu Sabrina pale alipo bado hana kumbukumbu"
Walijikuta wakimuongelea Sabrina njia nzima.
Nyuma yao alikuwepo Francis na kuwaita, nao wakashtuka sana kwani hawakutegemea uwepo wa mtu anayewafahamu nyuma yao.
"Mbona mmeshtuka hivyo?"
Wakacheka na kusalimiana nae.
"Nimewasikia kama mkimtaja Sabrina, je ni huyu ninayemjua mimi au ni Sabrina yupi?"
"Francis, dunia hii ni kubwa sana na Sabrina huyupo mmoja duniani. Halafu tumtaje huyo Sabrina unayemjua wewe kwa lipi? Hapa ni mambo yetu tu"
Francis hakutaka kubishana na hawa wadada kwahiyo alichokifanya ni kuwaaga na kuendelea na safari yake tu.

Sakina bado alikuwa nyumbani kwa wakina Sabrina kwa siku hiyo pia kwani hakujisikia kabisa kurudi nyumbani kwake ukizingatia akirudi anakuwa peke yake nyumba nzima.
Akiwa pale akapigiwa simu na mtoto wake Jeff kwa siku hiyo ambapo Jeff alikuwa na hoja yake ile ile ya jana.
"Yani mama kama huyo Dorry alikwambia mimi nilimpigia simu ujue ni muongo tena muongo hafai"
"Ila Jeff mwanangu sikuelewi na hata sijui umepatwa na nini huko."
"Sijapatwa na   chochote mama ila ndio hivyo. Na wala sina mahusiano na huyo msichana"
"Na ile mimba je?"
"Mimba? Mimba gani? Mama huyo msichana atakuchanganya akili tu mi simtambui. Ila nimemkumbuka sana mamdogo Sabrina naomba umsalimie sana"
"Nipo nae hapa, ngoja nimpe umsalimie"
"Wow, itakuwa vizuri sana maana simpati hewani siku hizi"
Sakina akachukua ile simu na kumkabidhi Sabrina ili aongee na Jeff.
Sabrina aliichukua ile simu na kuanza kuongea, mara gafla akaanza kulia na kumfanya Sakina ashtuke.

Itaendelea



No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

https://play.google.com/store/apps/details?id=chumba.cha.wakubwa