JE HAYA NI MAPENZI!! 81: - UHONDO KITANDANI

Hot

Post Top Ad

https://play.google.com/store/apps/details?id=chumba.cha.wakubwa

Wednesday, February 19, 2020

JE HAYA NI MAPENZI!! 81:



Yule mlinzi hakuchoka na kukazana kuwakaribisha
ndani ila Sabrina na Sakina walisimama pale pale
nje ya geti.
Muda mfupi tu, Sabrina akasikika akipiga kelele na
kuanguka, wakashangaa kuona nyoka akikimbia na
damu zikimtoka Sabrina mguuni.
Sakina naye akapiga kelele baada ya kumuona yule nyoka,
"Ni nyoka yule, uwiiiii"
Yule mlinzi alijaribu hata kutaka kumtupia jiwe yule nyoka ila alienda kwa kasi sana na haikujulikana ni wapi alipotokomea.
Wakaanza kumpa huduma ya kwanza Sabrina kwa kumfunga na kumkimbizia hospitali.

Sam alifika nyumbani kwa wakina Sabrina na kumkuta mama wa Sabrina ambapo alianza kushambuliwa na maneno tu.
"Mtoto mbaya sana wewe, hivi kweli kabisa mwanangu humjali tena? Au kwavile kapoteza kumbukumbu? Hata damu yako mwenyewe naye pia huijali?"
"Samahani mama, majukumu yalinizidia"
"Acha uongo jamani, majukumu gani hayo ya kukufanya uisahau familia yako? Yani hujali chochote kuhusu Sabrina na mwanao"
"Unanishutumu bure mama, kwanza yule mtoto si............."
Simu ya mama wa Sabrina ikaita na kumfanya Sam akatishe maneno yake kwani mama wa Sabrina aliipokea ile simu.
Na baada ya kuongea na  ile simu alionekana kama kupoteza muelekeo.
"Jamani mwanangu mimi jamani jamani, kapatwa na nini mwanangu"
Akaanza kumuita baba wa Sabrina kwavile alikuwepo kwa siku hiyo.
Na alipotoka akamueleza alichoambiwa na kilichofatia ni kwenda hospitali ambapo Sam alitaka kuwabeba kwa gari yake ila baba wa Sabrina akatamka kwa hasira,
"Hatuna dhiki ya kihivyo"
Huku akimpigia simu dereva wa gari za kukodi awafate.
"Kwani tatizo ni nini mzee wangu jamani? Mbona mnafanya hivyo?"
Mama wa Sabrina akamsihi mumewe apunguze hasira kisha wakapanda kwenye ile gari ya Sam na safari ya kwenda hospitali ikaanza.

Walipofika hospitali, wazazi wa Sabrina wakashuka.
Sam naye akataka kushuka ili akamuone Sabrina ila gafla moyo wake ukasita yani akajiona kabisa kutokuwa na hamu ya kumuona Sabrina, akajilazimisha kushuka ila kabla hajafika walipoelekea wazazi wa Sabrina akapigiwa simu na Neema,
"Naumwa sana mpenzi, nipo  nyumbani."
"Nakuja sasa hivi"
Sam akageuza huku akitabasamu, alifurahi kusikia Neema akimuita tena mpenzi kwahiyo kwake ikawa ni jambo la furaha sana.
Akafika kwenye gari yake na kuondoka hata akasahau kabisa kuwa alikuwa hospitali kwa lengo la kumuona Sabrina.

Wazazi wa Sabrina walifika na kukutana na Sakina ambaye aliwahabarisha ilivyokuwa na kuwafanya wasikitike sana.
"Nashukuru mtoto nilimbeba mimi maana sijui ingekuwaje kwani Sabrina angeweza hata kumuangukia mtoto"
Mlinzi wa Sam naye alikuwepo na kutoa ushuhuda wake,
"Hata mi nimeshangaa nyoka pale ametokea wapi wakati hakuna hata nyasi"
Kisha wazazi wa Sabrina wakakumbuka kama pale walienda na Sam.
"Yuko wapi sasa?"
"Yule kijana ni shetani, hafai yule hafai kabisa"
Walimsema sana kwani hakutokea hata kidogo kisha yule mlinzi wa Sam akawaaga na kuondoka kwani alihofia ikiwa Sam atarudi nyumbani na kumkosa.
Kwahiyo akaondoka pale hospitali.

   Baada ya muda kidogo pale hospitali wakaruhusiwa kwenda kumuona Sabrina ambaye alikuwa amefungwa ule mguu.
Kisha daktari akawaambia,
"Huu mguu wanasema kang'atwa na nyoka ila tumejaribu kuangalia sidhani kama ni nyoka"
Akadakia Sakina,
"Tumeona kwa macho yetu daktari alikuwa ni nyoka"
"Hakuna tatizo, kuna sindano tumemchoma, kwahiyo atakuwa sawa tu na mtarudi nae nyumbani"
Wakakubaliana na daktari ila bado Sakina alikuwa na mashaka sana.

Baadae kidogo wakaruhusiwa na kurudi nyumbani huku Sabrina akiburuza ule mguu aliong'atwa na nyoka.
Walifika nyumbani na kumkuta James yuko pale nje ambapo mama yake alimfata na kumuuliza,
"Vipi mwanangu James"
"Yani mama umeshindwa hata kuja kumuona baba hospitali!"
"Unamaana gani?"
"Inamaana mama hunielewi? Wewe ni mtu gani usiyetaka kumuona hata akiwa hospitali mwanaume uleyezaa naye?"
Mama wa Sabrina akamnasa kibao James kisha akamwambia,
"Nenda zako sasa kwa huyo   unayemuona ni wa maana kwako"
Kisha James akaanza kuondoka, Deo akamtazama James bila kuelewa kuwa ana matatizo gani kisha akamuita.
"James, James una matatizo gani?"
Mama wa Sabrina akamfata mumewe na kumvuta,
"Achana nae huyo mtoto kapagawa"
Kisha wakaingia ndani ila hakuna aliyeelewa kuwa kwanini James ameondoka vile zaidi ya mama yake tu kuelewa sababu.
Sakina hakutaka kufatilia hayo, yeye alikuwa na hofu tu ya Sabrina na ule mguu ambao alimuona nyoka kabisa ingawa hospitali walisema si nyoka.
Akatamani kumwambia mama wa Sabrina kuwa huenda Sabrina karogwa ila hakujua kuwa aanzaje kumwambia kwani alijua wazi atamshushua tu.
Basi aliamua kuwaaga pale na kuondoka.

Deo aliamua kumuuliza kwa ukaribu mkewe kuhusu mtoto wao James,
"Kwani huyu mtoto ana matatizo gani siku hizi?"
"Utaumia kichwa tu mume wangu, achana na mambo ya yule mtoto"
"Naachana nayo vipi wakati ni mtoto wetu!"
"Mimi naelewa hilo    ila mtoto yule haelewi hilo kabisa"
Bado Deo alikuwa na mashaka na kumuuliza mkewe kwa mshangao zaidi,
"Kivipi? Kwani umemwambia ukweli?"
"Sio mimi, ni mdogo wako huyo ndio kamwambia ukweli"
"Nimeelewa sababu sasa, ndiomana amekuwa vile. Mwache kwanza ipo siku ataelewa na kutambua ingawa nami roho imeanza kuniuma"
Deo akainuka na kusema anatoka kidogo, muda huo mama wa Sabrina alibaki kimya kwani hakuwa na usemi zaidi ya kuangalia kitakachoendelea tu.

Deo aliporudi nyumbani kwake alikuwa amesha chekecha akili vya kutosha kabisa na kumuaga mkewe.
"Kesho nasafiri"
"Mbona gafla hivyo? Na unaenda wapi?"
"Kwani kila siku ninaposafiri huwa naenda wapi? Wewe tambua tu kwamba kesho nasafiri, acha nikatulize akili yangu kwanza"
"Naomba unisamehe mume wangu, ila mimi sikukusudia hili"
"Sikia Joy, sikuwa mpumbavu kumkubali huyu mtoto toka alipokuwa mdogo ingawa kosa lilishatendeka. Sikuwa mjinga kumlea kama damu yangu na kumpa chochote alichotaka. Na sikuwa mjinga kwa kutokumjua huyo mwanaume ambaye ni baba yake mzazi kwani ilinisaidia kuepusha mambo mengi kwenye fikra yangu. Na sio mpumbavu kwasasa kukuaga kuwa nasafiri ili nikapumzishe akili yangu mbali na nyumbani. Nawe hunabudi kuniacha niende"
Mama wa Sabrina akamtazama mumewe kwa masikitiko ila hakuwa na namna zaidi ya kumruhusu tu.
Na kulipokucha Deo akasafiri na kumuacha Sabrina na mama yake.

Sakina bado alitamani kumwambia mama wa Sabrina kuhusu yule mganga ila alikuwa akijifikiria kuwa ataweza kumwambia kwa namna gani ukizingatia mama wa Sabrina hayapendi mambo ya kishirikina, kwahiyo alikuwa anaenda tu kwakina Sabrina na kubaki na hoja yake moyoni.
Siku hiyo aliporudi kwake alikuwa na mawazo zaidi kuhusu Sabrina, Dorry naye alikuwa karibu kumpa moyo.
"Mama, hakuna namna hapo. Ni kumuomba Mungu tu"
"Tatizo hujui Dorry, kama mama Sabrina angekuwa muelewa basi mi ningeshamueleza na Sabrina angekuwa ameshapona."
"Kwakweli watu huwa wanabadilika jamani, yani imeshindikana kabisa kwa Sam kuja kumuona mamdogo Sabrina mmh!"
"Ni ushirikina tu mwanangu"
"Mi nitajaribu kufanya kitu mama"
"Kitu gani?"
"Subiri tu utaona mama"
Sakina akaachana na maneno ya Dorry kwani aliona hayana faida kwake.

Sam naye akiwa nyumbani kwake, alijaribu kuchekecha mambo katika akili yake ila hakuweza kuelewa.
Akakumbuka siku anaenda kumuona Sabrina hospitali na kupigiwa simu na Neema kuwa anaumwa sana.
"Mbona sikumkuta na ugonjwa wowote? Na kwanini sijisikii kwenda kumuona Sabrina? Kwani nina matatizo gani mimi siku hizi?"
Bado Sam hakujielewa ila alijiona kumjali zaidi Neema kuliko kumjali Sabrina na ubaya zaidi ni kule kutokutamani kumuona Sabrina kabisa.

Baada ya wiki moja, mama wa Sabrina akashangazwa na hali ya mguu wa mtoto wake kwani siku hiyo waliamka na kukuta ule mguu umevimba sana halafu unavuja maji.
"Jamani huo mguu tena vipi mwanangu?"
"Hata mimi sielewi mama, nimeshangaa tu leo umevimba zaidi na huku unavuja maji"
Mama hakujua cha kufanya zaidi ya kumpigia simu dereva wa gari za kukodi ili wampeleke hospitali.
Muda kidogo kabla dereva hajafika, alikuja Sakina na yeye pia kushangaa ile hali ya mguu wa Sabrina.
"Sasa mama umeamua nini juu ya hilo?"
"Niamue nini mwanangu na hali kama hiyo. Nimempigia simu dereva atupeleke hospitali"
"Hapana mama tusiende hospitali"
"Kheee Sakina, tusiende hospitali halafu twende wapi?"
"Samahani mama ila Sabrina huo ugonjwa wake ni wa kurogwa"
"Kwahiyo twende wapi?"
"Twende kwa mtaalamu mama, ila samahani kwa hilo"
"Yani Sakina akili yako mmh! Badala useme twende kwenye maombi unasema twende kwa waganga jamani loh! Twende tu hospitali"
Sakina hakuwa na la kuongezea zaidi ya kukubaliana na hali halisi tu.
Alipofika dereva wakapanda gari kwa lengo la kwenda hospitali sasa.

Walipofika hospitali moja kwa moja Sabrina akapelekwa kwa daktari.
Akampima na kila kitu kisha kuwaita mama wa Sabrina na Sakina awaeleze kwa kifupi ilivyokuwa.
Sakina akamuelezea kila kitu, lakini bado daktari alitikisa kichwa kana kwamba anautafuta ule ugonjwa kwa akili.
Kisha akawaandikia dawa,
"Leo akanywe dawa hizi, ila kesho hali ikiendelea hivi itabidi tumchome sindano"
Mama wa Sabrina akadakia,
"Kwanini usingemchoma leo sindano daktari?"
"Kila kitu huenda kwa mpangilio mama, acha leo akatumie hizi dawa"
Ikabidi wakubali pale na kuanza safari ya kurudi nyumbani kwa kutumia gari ile ile ya kukodi.

Walifika nyumbani kisha Sakina akawaacha hapo na kurudi nyumbani kwake huku akiwa na masikitiko makubwa sana.
Kama kawaida, akenda kutuliza mawazo yake kwa kushauriana na Dorry kidogo.
"Hata sijui nifanyeje, yani ingekuwa amri yangu au ningekuwa na  uwezo basi ningetafuta hao ng'ombe mwenyewe ili Sabrina apone. Kwakweli namuhurumia sana. Lazima Sabrina atakuwa ametupiwa jini tu"
"Sasa hapo utafanyaje mama?"
"Sijui, ila ninachojua ni kuwa jini halipatani na sindano. Na kwa mtindo huu limejidhihirisha wazi kwa kumvimbisha Sabrina mguu, basi hapa inawezekana Sabrina akichomwa sindano tutampoteza kabisa. Jamani Sabrina mdogo wangu namuhurumia sana, yote hiyo wanamtesa kwa wivu wa kuolewa na mume tajiri"
Sakina alikuwa akisikitika tu huku akijaribu kutafakari cha kufanya.
Muda kidogo wakapigiwa simu na Jeff na kumfanya Sakina atabasamu kidogo kwani ni kitambo hajapata mawasiliano na mwanae.
"Mama, mbona mpo kimya sana! Na vipi mamdogo nae anaendeleaje?"
Sakina akaamua kumueleza kidogo Jeff kuhusu hali ya Sabrina kwani alijua kama akimueleza kiundani zaidi atamchanganya.
"Sam naye anasemaje kuhusu hilo maana naye simpati kabisa"
"Yani mwanangu ya huku yaache tu maana hali ni mbaya. Huyo Sam hata hajui huku Sabrina anaendeleaje"
Jeff akaongea na mama yake pale na mwisho wa siku akaikata ile simu.

Usiku wa siku hiyo Dorry akiwa chumbani, akashangaa kuona namba mpya ikimpigia.
Akashtuka sana kwavile ilikuwa ni namba ya nchi za nje.
Akaipokea kwa mashaka, akashangaa kusikia ni sauti ya Jeff na kujiuliza kuwa kwanini Jeff ameamua kumpigia siku hiyo.
Sauti ilikuwa ni ya Jeff ila Dorry alishangaa huyo Jeff akiongea kwa ustaarabu na kwa maelekezo zaidi.
Yani hadi ile simu inakatika bado Dorry alikuwa akishangaa ila alikumbuka maelekezo yote aliyopewa kwenye simu.

Kulipokucha asubuhi na mapema, Dorry aliamka na kujiandaa kisha akamuaga mama mkwe wake.
"Wapi asubuhi yote hii?"
"Kuna mahari naenda mama"
"Khee ndio asubuhi yote hii? Ila mi hutonikuta ukirudi hapa nitakuwa kwakina Sabrina"
Basi Dorry akaaga pale na kuondoka hadi alipoelekezwa.
Ilikuwa ni  barabarani tu akingoja gari ya Sam ipite.
Na ilipopita tu akaisimamisha na kupanda.
"Khee Dorry, nimeshangaa kukuona hapo barabarani"
"Sawa, ila nilikuwa nakungoja wewe Sam. Tena chonde chonde nakuomba twende ukamuone Sabrina"
"Muda huu? Acha niende ofisini kwanza, nitakuja badae kumuona"
"Mi nakuomba Sam, wewe ni kama kaka yangu. Nakuomba twende muda huu na wala sitakusumbua tena"
Sam akaona ni vyema amridhishe tu huyu Dorry kwa kwenda kumuona huyo Sabrina.

Sakina naye alifika nyumbani kwakina Sabrina na kumkuta mama Sabrina alishamtoa Sabrina nje wakisubiri gari waende hospitali.
"Jamani, mguu ndio umevimba zaidi"
Sakina alisikitika na kutoa machozi kwani alimuhurumia Sabrina kwa ile mimba na hali aliyonayo kwa kipindi hicho.
Walikaa pale nje wakimngoja dereva tax, na muda kidogo dereva akafika na kuwafanya waanze kumkongoja Sabrina kuelekea kwenye gari.
Muda huo Sam na Dorry nao wakafika, Dorry  akamuomba Sam ashuke kisha akawaita wakina Sabrina.
Sam na Dorry wakaanza kuelekea waliko kwani walisimama baada ya kuitwa, Sam akamshangaa Sabrina kwa jinsi mguu ulivyovimba na kuuliza kwa mshangao.
"Imekuwaje tena?"
Hakuna aliyemjibu, Sam akasogea na kumshika bega Sabrina kamavile mtu anayehitaji jibu.
Ila kabla ya yeyote kati yao kusema chochote, wakashangaa kumuona Sam akianguka chini na kuwa kimya kabisa.

Itaendelea



No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

https://play.google.com/store/apps/details?id=chumba.cha.wakubwa