Akaamua kuzikusanya, ila akashtuka kidogo na
kujisemea.
"Huenda zikawa karatasi za maana"
Akakaa pale kitandani ili azipitie kidogo.
Akasikia mtu akimuita, kumsikilizia vizuri akagundua kuwa ni sauti ya Sabrina.
Akaamua aache zile karatasi pale kitandani kisha aende kumkaribisha Sabrina.
Sakina akatoka na kumkaribisha Sabrina pale kwake.
"Karibu mdogo wangu"
Sabrina kabla hata ya kukaa akaanza kubwabwaja,
"Yani leo ndio nimejua sababu ya wewe dada yangu kutokukaa na mumeo. Yani hawa wanaume ni kero jamani, kero kero kabisa mi nishawachoka"
Sakina akamuangalia kisha kumngoja akae kwanza na kumpa pole.
"Pole mdogo wangu, ila tatizo ni nini?"
"Nimechoka dada, yani nimechoka kwakweli"
Sabrina akaanza kumsimulia Sakina juu ya Neema.
"Yani huyo mwanamke kanivuruga halafu huyo mwanaume naye anarudi na kunivuruga pia"
"Pole mdogo wangu, ila ndoa inahitaji uvumilivu sana. Hutakiwi kuwa na hasira kiasi hicho"
"Mbona wewe hukuweza kuvumilia?"
"Mie maji yalinifika shingoni, hakuwa mume yule. Yalikuwa ni mauzauza tu"
Sabrina akamuangalia Sakina kisha akaendelea na msimamo wake kuwa Sam naye ni wale wale, hana utulivu wowote kama ambavyo Sakina amekuwa akimtetea.
Dorry aliwasili nyumbani kwa Sakina, kabla ya kubisha hodi akasikia sauti ya Sabrina na Sakina wakizungumza.
Dorry akaogopa kuingia kwani alijawa na hofu za aina mbili, moja ni kuwa huenda Sabrina kashamueleza Sakina, na mbili ni kuwa huenda bado hajamueleza ila atakapoonekana yeye anaweza kuwa kama anamkumbusha kuelezea.
Alijibanza pembeni ya nyumba ya Sakina huku akijifikiria cha kufanya kwa wakati huo.
Sam alimaliza shughuli zake siku hiyo na kuanza safari ya kurudi nyumbani kwake.
"Nataka leo niwahi kurudi, yani sipitii popote ili huyu Sabrina akanieleze vizuri tatizo lake. Maana najitahidi kumuelewa, na kumuweka sawa lakini inashindikana. Ngoja tu akaniambie tatizo lake."
Muda kidogo akawasili nyumbani kwake.
Alipoingia ndani hakumkuta Sabrina ikabidi akamuulize mlinzi wake,
"Yuko wapi mke wangu?"
"Katoka, kaniambia anaenda kwao"
Sam akajishika kichwa na kurudi ndani, akakuta Sabrina alishabeba nguo zake zote na za mtoto.
"Anamaana gani kufanya hivi? Huyu Sabrina anamatatizo gani jamani?"
Sam alijiuliza bila hata ya kupata jibu juu ya tabia ya Sabrina.
Sabrina alimuaga Sakina sasa kuwa anarudi kwao,
"Inamaana hutorudi tena kwa mumeo?"
"Sirudi hadi aje aniombe msamaha"
"Hongera, najua yote ni sababu unajua anakupenda na lazima atakuja. Umepata mume bora ingawa wewe binafsi hujakubali hilo"
"Sijui kwanini unapenda kumtetea, ila hakuna tatizo siku moja utaelewa vizuri kwanini nalalamika kiasi hiki"
Basi Sakina ikabidi akubaliane nae tu, kisha akatoka nae nje ili amsindikize kidogo.
Muda wametoka, Dorry nae akatumia nafasi hiyo kwa haraka. Na moja kwa moja, aka ingia chumbani kwa Jeff na kubeba vyote pale kitandani kisha akatoka navyo na kwenda kujibanza tena nyuma ya nyumba ili amngoje Sakina arudi kwanza nyumbani kwake kuhofia kukutana nae njiani.
Na muda kidogo tu Sakina alirudi, kisha Dorry akatoka kule alipojibanza na kuondoka zake.
Sakina akiwa nyumbani kwake, alikuwa akimsikitikia tu Sabrina kwa mambo ambayo anayafanya.
"Yule Sam anaupendo jamani, kitu gani Sabrina atake halafu Sam asimpe. Anaweza kujitetea kuwa sababu amezaa nae, ila hiyo bado siyo sababu. Kwani wangapi tumekimbiwa tukiwa na watoto, wangapi wanakimbiwa na mimba? Ila yeye kapata mwanaume mzuri, ingawa alitangulia kumpa mimba kwanza lakini alihakikisha kuwa mpaka anamuoa ili mtoto wao azaliwe ndani ya ndoa, akafanya sherehe kubwa sana kwaajili yako. Miezi yote yupo kwao na mwanaume anaenda kumuangalia kila siku, hivi kwanini watu hawapendi bahati kama hizi? Hebu ona kampeleka mwanangu nchi za nje kusoma, yote ni sababu ya upendo tu. Kwakweli sisi wanawake sijui tufanyiwe nini turidhike jamani!"
Sakina alijikuta akisikitika tu pale.
Muda kidogo akakumbuka alichokuwa anakifanya kabla ya kuongea na Sabrina,
"Ile ni barua ile nadhani Jeff aliandikiwa na mwanamke wake, na labda ndio sababu ya Dorry kuondoka haraka vile, nadhani hakupendezewa na kilichoandikwa mule. Ngoja nikamalizie kuisoma."
Muda huo alikuwa tayari ameingia chumbani kwa Jeff, akashangaa bila kuona chochote pale kitandani.
Akajiuliza kuwa vimeenda wapi, akainama uvunguni mwa kitanda lakini hakuona chochote.
Akaangaza kile chumba chote lakini hakuona kitu, akajikuta akijishika kichwa na kusema,
"Mungu wangu, ni mambo ya kichawi haya yameingia tena ndani kwangu"
Uoga ukamshika Sakina, akatoka kwa haraka kwenye kile chumba cha Jeff na kukifunga kwa funguo kabisa, kisha akaenda kukaa sebleni kwake na kujisemea,
"Itabidi kesho niende kwa mtaalamu akaniangalizie haya mambo. Uoga unanishika jamani"
Alibaki kujiuliza tu kuwa kwanini wachawi wameanza tena kumfatilia.
Sam akataka kwenda nyumbani kwakina Sabrina, ila akaona ni vyema asiende kwa siku hiyo.
Ampe nafasi kwanza kisha aende kesho yake kuonana nae.
Akapanga kwenda muda ambao atakuwa ametoka ofisini.
"Kila siku niharibu kazi yangu kwaajili ya mtu mmoja. Afanye nishindwe kusimamia chochote kile. Nitaenda baada ya kazi, tena hakuna mjadala hapo zaidi ya kurudi naye huku tu"
Sam alikuwa akiyapanga hayo kwa muda huo.
Ilipofika saa tatu usiku, Sabrina akatambua kuwa Sam hawezi kwenda tena kwa muda huo.
"Ingekuwa mapema, ningejipa matumaini kuwa atakuja. Ila mwache tu, mi namuangalia tu"
Sabrina alizidi kuweka hasira dhida ya Sam, kisha akaamua kulala.
Kulipokucha, alfajiri na mapema. Sakina alijiandaa na kuianza safari ya kwenda kwa mtaalamu ambaye amemuwazia usiku uliopita kuwa anaweza kumsaidia.
Alisafiri kwa basi kwa muda wa masaa mawili na kufika kwa huyo mtaalamu. Na kweli aliwahi kwani alikuta bado watu sio wengi mahali pale.
Muda wake ulipofika, akaingia kwa yule mganga na kuanza kumuelezea matatizo yake.
Alipomaliza kuelezea, yule mganga akaanza kucheka na kumfanya Sakina ashangae na kumuuliza,
"Mbona unacheka mtaalamu?"
"Hahahaha, tatizo lako nimeshalijua"
"Niambie basi mtaalamu"
"Kuna mtu anakufatilia, kuna mtu hataki maendeleo yako. Yani ulipowaza kuwa ni uchawi wala hukukosea. Kuna mwanamke mmoja mnene mweusi, hajapendezewa na mwanao kwenda nje kusoma ndiomana anakufanyia vituko hivyo"
Sakina alikaa na kutafakari, taswira ya mtu aliyetajiwa ikaanza kumjia katika akili yake.
"Nalijua hilo janamke, lina roho mbaya sana. Ila nani kamwambia kama mwanangu ameenda nje kusoma?"
"Wachawi huwa wanaambizana yote, ndiomana hizo karatasi zimepotea katika mazingira ya kutatanisha. Nitakupa dawa, ukaweke kila kona ya nyumba yako kwa usalama wako na mtoto wako."
Sakina akashukuru pale, kisha yule mtaalamu akampa dawa ya kunyunyiza kwenye nyumba yake na kumwambia maneno ya kunuia anapokuwa anainyunyiza.
"Halafu baada ya siku mbili niletee nguo yoyote ya mwanao niifanyie dawa ili awe salama huko alipo"
Sakina alikubaliana na yule mganga kisha akamuuliza kitu kingine,
"Nina mdogo wangu anaitwa Sabrina, yani jana kagombana na mumewe. Mi nahisi kuna kitu au waonaje mtaalamu?"
"Ni kweli kuna kitu kwani kuna mtu hapendi ndoa yao ndio anamfanyia hayo mambo. Mi nitafanya dawa ya kumtuliza huyo mumewe kwa siku mbili hizi, halafu ukiwa unakuja kuleta nguo ya mwanao uje nae"
Sakina akakubali pale kisha akaondoka zake kurudi nyumbani kwake.
Alipofika tu nyumbani kwake, akaifanya ile dawa aliyoambiwa na mganga kisha akanuia na maneno yake.
Alipomaliza aliamua kwenda kwa wakina Sabrina ili kumuuliza kuwa ameishiana vipi na mumewe na kumwambia kile alichoambiwa na yule mganga.
Alifika kwakina Sabrina na kumkuta Sabrina akiwa amejiinamia kwa mawazo,
"Pole mdogo wangu, ila nimepata suluhisho la tatizo lako"
Sabrina akamuangalia na kumuuliza,
"Lipi hilo?"
Kisha Sakina akaanza kumueleza Sabrina juu ya mahali alipoenda na vile alivyoelezwa na yule mtaalamu.
Sabrina akacheka, Sakina akamuuliza
"Mbona unacheka sasa?"
"Yani wewe dada bado unawaamini hao wataalamu?"
"Ndio nawaamini mdogo wangu, ni kweli watu wanakuonea wivu. Sio kila mtu anapenda maendeleo yako Sabrina"
"Ni kweli sio kila mtu atapenda maendeleo yangu, ila mimi wataalamu siwaamini tena"
"Kwanini?"
"Unakumbuka walivyonipa onyo kipindi kile?"
"Nakumbuka ndio, ila wamekusaidia mdogo wangu"
"Hakuna walichonisaidia, ni Mungu tu ndio amenisaidia. Kwanza waliniambia nisifanye mapenzi na mwanaume yeyote eti mwanaume huyo atakufa. Loh mbona hajafa? Walisema kuwa sitaweza kuzaa, hata nikibeba mimba itatoka mbona sasa nina mtoto?"
Sakina alimuangalia tu Sabrina,
"Kwahiyo huwaamini hata kidogo?"
"Hata chembe siwaamini, wamenifanya niishi roho juu juu. Kama utabiri wao tu hata shangazi yangu ni mtabiri pia"
"Inamaana yaliyotokea ndani kwangu kama sio mauzauza ni nini?"
"Hayo sijui ila waganga siwaamini"
Muda kidogo akawasili Sam pale nyumbani kwakina Sabrina.
Sakina alipomuona Sam akamsalimia kisha akaaga na kuondoka.
Moyo wake ukamwambia kuwa dawa ya mganga imefanya kazi na kumvuta Sam kwa Sabrina.
Sam alimuangalia Sabrina na kukaa pale karibu yake, kisha akamwambia kama staili ya kumnong'oneza,
"Nakuomba twende nyumbani Sabrina"
"Sitaki"
"Kwani tatizo ni nini mke wangu? Kosa langu ni lipi kwako Sabrina. Au kukupenda kwangu ndio imekuwa kosa? Nakuomba twende nyumbani"
Sabrina akajikuta akimuhurumia Sam kisha akakubali kurudi nyumbani kwa Sam.
Wakafungasha mizigo na kumuita mama yake kisha kumuaga.
Joy alitingisha kichwa tu na kumruhusu kwani aliiona akili ya mwanae sasa ikifanya kazi ndivyo sivyo.
Sabrina na Sam walifika nyumbani kwao, ila Sam hakumuuliza chochote cha ziada Sabrina na wala Sabrina nae hakuuliza kitu chochote.
Muda kidogo simu ya Sam ikaita, na alipopokea akaisikia ni sauti ya Dorry.
"Samahani, kuna namba nakutajia uniambie kama waijua"
Dorry akaitaja ile namba,
"Ndio naijua, ni ya mke wangu kwani vipi? Alikupigia simu?"
"Hapana, kuna mahali nimeiona ndiomana nikakuuliza"
Kabla Sam naye hajauliza swali jingine, Dorry alishakata ile simu.
Sabrina akamuuliza Sam,
"Ni nani? Na kwanini unitaje mimi?"
"Ni rafiki yangu, nadhani kuna siku nimempigia simu kwa namba yako ndio alikuwa akiulizia tu"
"Mmh"
Sabrina akaguna tu, kisha kudai kuwa anausingizi sana hivyo wakaenda kulala.
Dorry alijifikiria na kujiuliza sana,
"Iweje Jeff aandike kwenye namba ya mama yake mdogo kuwa ndiye mwanamke anayempenda sana? Kama ni upendo ule wa kawaida kwanini asiweke namba ya mama yake mzazi? Hivi inawezekana kweli kwa mtoto kumpenda zaidi mama yake mdogo kuliko mama mzazi mmh! Hapa lazima kuna kitu tu"
Dorry akataka kuanza uchunguzi wake wa taratibu ili aujue ukweli.
Usiku wa manane, Sabrina aliamka na kuchukua simu ya Sam. Kisha akapekua namba ya mwisho kumpigia, akaona jina Dorry.
Akainakili ile namba pembeni huku akijiuliza kuwa kwanini huyu Dorry anapenda sana kuwasiliana na Sam.
Akaoanisha na ule ujumbe wa mpango wao.
"Lazima wanakitu hawa na nitakijua tu"
Kisha akarudi tena kulala.
Kulipokucha, Sabrina aliamka na kuandaa chai ili aweze kunywa na Sam ukizingatia siku hiyo ilikuwa ni siku ya mapumziko.
Sabrina aliandaa ile chai kisha akamuita Sam na kuanza kunywa, Sam akamwambia
"Ingekuwa hivi siku zote kwakweli ingekuwa raha sana"
Sabrina akatabasamu na kusema,
"Huwa napenda kufanya hivi ila tatizo huwa nachoka sana halafu nashikwa na uvivu balaa"
"Pole ila nilikwambia kuhusu msichana wa kazi umekataa"
"Nikimuhitaji nitakwambia"
Muda kidogo Sabrina akakimbilia nje na kuanza kutapika, tena alitapika sana.
Sam huwa hapendi kuendekeza ugonjwa hivyo akamsaidia kujiandaa na kuanza safari ya kwenda hospitali wakiwa na mtoto wao.
Walipofika hospitali, Sabrina akapimwa vipimo vyote kisha daktari akawaletea majibu.
"Hongereni sana"
Sabrina na Sam wakaangaliana, kisha Sam akamuulizo dokta.
"Hongera ya nini?"
"Mkeo ni mjamzito"
Sabrina akajikuta akianguka na kuzimia.
Itaendelea
JE HAYA NI MAPENZI!! 73:
Sabrina na Sam wakaangaliana, kisha Sam
akamuulizo dokta.
"Hongera ya nini?"
"Mkeo ni mjamzito"
Sabrina akajikuta akianguka na kuzimia.
Sam alijikuta akibaki na mshangao, ikabidi daktari asaidie kumnyanyua Sabrina na kumuweka kitandani.
Kisha daktari akamuuliza Sam,
"Mbona umebaki na mshangao hivyo? Hamkuitegemea hii mimba au?"
"Ungekuwa wewe ungefurahi? Unaniona kabisa hapa nimebeba mtoto tena bado mdogo halafu unaniuliza kwanini nashangaa?"
Daktari akaisoma kwa haraka haraka saikolojia ya Sam kisha akaona ni vyema asimuulize tena maswali kwani aliona wazi anaweza kupaniki muda wowote ule.
Daktari akaanza kumpa huduma Sabrina ili angalau aweze kurudi kwenye hali ya kawaida.
Akamuomba Sam atoke nje ya kile chumba ili aweze kumpa Sabrina matibabu kwa nafasi.
Sam alitoka nje ila alikuwa kamavile akili imemruka kidogo kwani alikuwa akiongea peke yake tu muda wote.
Hakujielewa kwa wakati huo, na swali kubwa alilojiuliza ni kuwa, mimba ya sasa ya Sabrina ni ya nani? Kila akifikiria hapo moyo ulikuwa unamuuma sana.
Muda kidogo, mtoto akaanza kulia na kumfanya Sam achukie zaidi.
Daktari alipotoka aliweza kuiona hasira ya Sam kwa wazi wazi, akaamua kumuomba amkabidhi yule mtoto.
Sam alimkabidhi yule mtoto daktari kisha akaondoka kwa hasira, daktari hakuelewa ila alimuangalia tu kwani hata kumuita tena hakuweza.
Kwavile Sabrina alishazinduka, daktari akaona ni vyema amkabidhi mwenyewe mtoto wake kwani muda ule alitoka nje kwa lengo la kumwambia Sam kuwa mkewe amezinduka ila kutokana na ile hasira aliyomuona nayo hakuweza kumwambia.
Daktari akamkalisha Sabrina na kumuuliza,
"Kwani mna matatizo gani na mumeo?"
"Ni historia ndefu daktari, siwezi kukueleza kwasasa. Kwanza Sam mwenyewe yuko wapi?"
"Ameshaondoka"
Sabrina akashtuka na kujisikitikia, kisha akainama kwa dakika kadhaa na kuinuka, muda wote daktari alikuwa akimuangalia tu,
"Na mimi naondoka daktari"
"Unaenda wapi sasa?"
"Naenda nyumbani"
Daktari naye akamsikitik ia Sabrina kwani alimuona jinsi alivyopooza, daktari akamuuliza tena,
"Una nauli?"
Sabrina akamuangalia daktari kisha chozi likamtoka, moja kwa moja daktari akamuelewa.
Akatoa noti ya elfu kumi na kumkabidhi, Sabrina akaipokea na kumshukuru kisha akaondoka.
Sam alikuwa na mawazo sana, alijikuta akipaki gari yake mahali na kuanza kulia ndani ya gari.
Machozi ya hasira yalimtoka kwa mfululizo, akajisemea
"Sijawahi kulia, eti leo nalizwa na mwanamke! Siamini"
Moyo wake ulimuuma sana.
Alikuwa akijifikiria tu, mawazo ya mtoto Cherry yakamjia kichwani mwake, akakumbuka jinsi katoto hako kalivyoonekana na sura ya upole, kamejaa upendo.
Sam akageuka nyuma na kusema,
"Huyu bado ni mwanangu"
Akageuza gari na kuanza kurudi hospitali.
Sabrina aliondoka pale hospitali huku kichwa chake na akili yake vikijutia.
Alipanda kwenye daladala ila bado machozi yalimtoka kiasi kwamba akaona kuwa dunia sasa imemgeuka.
Alijikuta akijuta sana na kujiona ni mwanamke mjinga, alikuwa na mawazo tu muda wote huku akijiuliza alipoipatia ile mimba.
Akakumbuka siku aliyoitwa na Jeff, roho ikamuuma sana.
Sabrina alipofika nyumbani kwao, akataka kwenda chumbani kwake moja kwa moja ila aliamua kujigelesha kwanza baada ya kumuona mama yake akiwa na wifi yake Joy.
Ikabidi asogee kuwasalimia kwanza.
Mama yake akamshangaa na kumuuliza,
"Unatatizo gani mwanangu? Mbona macho mekundu na sikuelewi"
"Sina tatizo mama ila macho tu yananiuma"
"Yani ndio Sam kakuacha uje hivyo mwenyewe?"
"Hapana, hata hajui kama macho yananiuma kwani yameanza muda sio mrefu"
Wakampa pole pale, kisha mama yake akamuhabarisha Sabrina,
"Wifi yako umuonapo hapo ana mimba"
Sabrina akashtuka kamavile ameambiwa yeye, kisha Joy naye akajitetea,
"Yani mama, wengi wananisema juu ya hili. Ila nashukuru ni mimi na mume wangu ndio tulikubaliana jambo hili mama"
Sabrina akatabasamu kinafki na kumpongeza Joy,
"Hongera wifi"
Na kabla hawajaongea lingine, aliinuka na kwenda kwenye chumba chake.
Akamlaza mwanae kitandani, kisha yeye akakaa na kujiinamia kwa mawazo.
Sam alifika hospitali na kwenda moja kwa moja kwa daktari, akamkuta na kumuuliza,
"Mke wangu yuko wapi?"
"Ameondoka"
"Ameondoka vipi wakati..... Aaarrgh"
Akatoka kwa daktari na yeye akaondoka.
Yule daktari alimshangaa Sam kuwa vile kwani sio kama alivyomzoea siku zote.
Sam alipokuwa anatoka pale hospitali huku akielekea kwenye gari yake, kuna mdada akamfata kwa nyuma na kumuita,
"Sam"
Sam akageuka na kumuangalia yule mdada, akajaribu kuvuta kumbukumbu kama kuna mahali alipowahi kuonana nae lakini kumbukumbu hazikumjia kabisa na kuona ni wazi hamfahamu ila akamshangaa kwani yule dada alionyesha uchangamfu kanakwamba ni mtu anayemfahamu.
Sam akamuangalia tu hadi yule dada alipomkaribia kabisa,
"Mambo Sam"
Sam aliitikia huku bado akionyesha kumshangaa,
"Najua unashangaa kwavile hujawahi kuniona, ila mimi nakufahamu vizuri Sam"
"Nashukuru, ila ungeniambia uliponifahamia maana nina haraka kidogo"
"Usijali, nipe mawasiliano yako badae nikutafute ili nikwambie nilipokufahamu"
Sam akazidi kumshangaa huyu dada ila kwavile hakutaka kupoteza muda, akatoa kadi yenye mawasiliano yake kisha akampatia yule dada na kumuaga.
Sam aliondoka ila yule mdada alimtazama Sam hadi alivyotokomea na gari yake.
Joy alipoaga na kuondoka, ikabidi mama wa Sabrina amfate mwanae chumbani kwani hakumuelewa kuwa ana matatizo gani.
Alimkuta Sabrina akiwa amejiinamia na kugundua wazi analia.
Alimfata na kumkumbatia, kisha akamuuliza,
"Kwani tatizo ni nini mwanangu?"
"Tatizo mimba mama, nina mimba"
Mama yake akacheka kidogo na kumuuliza,
"Sasa mimba ndio tatizo? Mimba ni baraka mwanangu"
"Baraka gani wakati nina mtoto mdogo kiasi hiki!"
"Mbona Joy naye ana mtoto mdogo tena kushinda wako ila ana mimba! Hiyo ni baraka tu mwanangu, kuna watu wanalilia mimba usiku na mchana ila hawapati"
"Mi sikuitaka hii mimba mama"
"Kama hukuitaka ungetumia njia za uzazi wa mpango"
"Mi sikujua kama mwanamke mwenye mtoto mdogo anaweza kupata mimba"
"Swala ni kwamba, mwanamke anapotoka kujifungua hata anapotoa mimba, milango ya uzazi yote inakuwa wazi na tayari kubeba mimba nyingine. Kwahiyo usishangae, ni jambo la kawaida tu. Tatizo lako binti yangu umekuwa msiri sana ndiomana hukupata elimu hii, kliniki hukwenda yani ulikuwepo tu. Na hilo ni tatizo"
Sabrina akainama chini na kufikiria, alikuwa akimfikiria Jeff tu na kuona kamavile alimfanyia mchezo wa makusudi kwavile alijua atamuacha na mimba kama hivi. Mama yake akamshtua kwenye yale mawazo,
"Ila Sam naye yupo fasta, anajua kama tayari una mimba?"
Sabrina akaitikia kwa kutikisa kichwa, aliogopa kutoa sauti akihofia siri yake kufichuka kwani angeweza kutoa machozi.
Mama yake akaendelea kumwambia,
"Kama mumeo anajua basi usiwe na wasiwasi, maana watoto ni zawadi mwanangu"
"Ni kweli mama ni zawadi ila sio katika hali yangu"
"Kwani hali yako inatatizo gani? Kuwa wazi mwanangu"
Sabrina akawa anajiuma uma tu huku moyo wake ukimshauri kuwa amwambie ukweli mama yake, ila mdomo wake ukagoma kuusema ukweli huo.
Muda kidogo wakasikia mtu akibisha hodi, mama wa Sabrina akadakia
"Ni sauti ya Sam hiyo"
Kisha akainuka kwenda kumkaribisha.
Ni kweli alikuwa Sam, ambapo mama wa Sabrina akamkaribisha vizuri ndani
"Najua umemfata mwenzio"
"Ndio mama nimemfata"
"Karibu sana"
Sam akakaa kwenye kiti na kumngoja mama wa Sabrina akamuitie Sabrina.
Sabrina alipofatwa na mama yake na kuambiwa kuwa Sam amemfata, alitamani kugoma kwenda ila atamuelezaje mama yake.
Alikosa jibu na kuamua kukubali huku akijisemea kuwa liwalo na liwe.
Sabrina alitoka na kumkuta Sam akiwa na furaha tu, kanakwamba hakuna chochote kibaya kilichotokea.
Kisha wakabeba mtoto wao na kuondoka.
Njia nzima hakuna aliyemsemesha mwenzie hadi walipofika nyumbani kwao.
Sam alishuka na mtoto, kisha Sabrina naye akashuka.
Moja kwa moja wakaingia ndani na Sam akaenda kumlaza mtoto chumbani, muda huo Sabrina alibaki sebleni huku akiwa amejiinamia tu.
Muda kidogo Sam akatoka chumbani na kwenda kukaa sebleni karibu na alipokaa Sabrina.
Wote wawili walitulia kimya huku Sam akitafakari namna ya kumuuliza Sabrina, na wakati huo Sabrina nae alikuwa akitafakari hatma yake kwa Sam.
Muda kidogo simu ya Sam ikaita, naye akaipokea
"Mambo Sam"
"Safi, nani mwenzangu?"
"Mi ni yule mdada tulikutana hospitali nikakuomba namba ya simu ili nikwambie nilivyokufahamu"
"Sawa nimekumbuka, niambie basi"
"Ngoja nakutumia meseji sasa hivi"
"Sawa basi nangoja meseji yako"
Sam akakata ile simu, lakini muda huo Sabrina alijikuta akijawa na dimbwi la wivu lakini hakuweza kuuliza kwavile tayari alikuwa na makosa.
Muda kidogo akasikia mlio wa ujumbe kwenye simu ya Sam, kisha akamuona Sam akisoma ujumbe huo na kutabasamu.
Na baada ya dakika kadhaa Sam akainuka na kumuaga Sabrina kwa kumwambia,
"Badae"
Sabrina alimuangalia tu Sam hadi alipotoka nje kabisa.
Sabrina aliinama na machozi ya uchungu kumtoka, moyo wake uliumia sana, alijiona kamavile fungu la kukosa.
Alijiuliza sasa,
"Hivi Sam ameamua kunifata nyumbani na kunirudisha huku ili kuniumiza au ni kitu gani?"
Roho yake ikaumia sana na kumfanya azidi kujutia.
Sam alienda hadi mahali alipoweza kuonana tena na yule mdada ambapo yule mdada alijawa na tabasamu tu usoni.
Wakatafuta eneo la karibu na kukaa kwaajili ya maongezi,
"Kwanza kabisa Sam samahani sana kwa kukuita hapa"
"Hata usijali, sina tatizo ndiomana nimeitikia wito "
"Sawa basi nashukuru kwa hilo, kwanza kabisa napenda ujue kuwa mimi nakufahamu wewe vizuri kabisa ila namfahamu zaidi mkeo"
Sam akashtuka baada ya kusikia kuwa mkewe anafahamika zaidi na kumfanya aanze kumsikiliza kwa makini.
"Niambie mke wangu unamfahamu vipi na mimi umenifahamu vipi?"
Kabla huyu dada hajamueleza chochote Sam, akaona ishara kama ya mtu kumuita na kumuomba samahani Sam,
"Naomba nikamsikilize kidogo, narudi muda sio mrefu"
Sam akamuitikia na yule dada akaondoka, huku Sam akitamani kujua kitu ambacho yule dada anajua kuhusu mke wake.
Dorry aliamua leo kuyachoma yale makaratasi ili kupoteza ushahidi wote ambao ulikuwepo.
Ila kabla ya kuchoma, akakifunua tena kile kitabu kidogo na kukutana na maneno mwishoni,
"Sabrina roho yangu, Sabrina mwanamke wa maisha yangu. Nakupenda na sitakuja kumpenda yeyote kama nikupendavyo wewe. Haya maneno ningependa kuyatamka mbele yako ila siwezi kwavile utaona nakukosea adabu, ila ukweli upo kwenye moyo wangu na matendo yangu. Nitakupenda milele yote"
Dorry akapata jibu la Sabrina anayeongelewa pale, alielewa wazi kuwa ni Sabrina yule yule ila bado hakuelewa kwanini Jeff awe na upendo wa namna ile kwa mama yake mdogo?
Makaratasi yake ya mimba na barua akayachoma moto ila kale kakitabu kadogo akakahifadhi kwenye mkoba wake.
Sabrina akiwa nyumbani huku mawazo yakifurika kwenye kichwa chake, akaamua kuchukua simu yake na kuingia kwenye mtandao wa kijamii.
Alikuta akiwa na ujumbe mwingi kwenye sehemu ya ujumbe iliyopo kwenye akaunti yake ya facebook.
Akaamua kufungua ujumbe alioona umebeba picha, na alipofungua tu akaona picha kubwa ikiwa imetangulia.
Sabrina akashtushwa na ile picha, kwani alijiona yeye na Jeff wakiwa kitandani, kisha ujumbe ukafata chini.
Mapigo yake ya moyo yalienda kwa kasi ya ajabu kupita ilivyo kawaida yake.
Itaendelea
No comments:
Post a Comment