Mama alivyotoka tu bafuni, nikaenda kumimina ile
dawa yote kisha nikatoka nje na kukaa mbali
kidogo na bafu ili kusikilizia majibu ya ile dawa
atakavyooga yule baba.
Muda kidogo nilimuona mama akitoka ndani kwa
hasira huku akisema kuwa ni bora tu akaoge
mwenyewe hapo nikaelewa wazi kuwa lazima baba
amekataa.
Nikataka nikimbilie bafuni ili nikamwage yale maji
ila kabla sijafika bafuni mama alikuwa kashaingia
tayari.
Ikabidi nitumie akili yangu ya ziada.
Ni hapo nilipoamua kukimbilia bafuni kwa kuhofia mama asije kuoga yale maji.
Kwakweli nilimkuta mama kashatoa nguo zote ila sikujali zaidi ya kumwaga ile ndoo na kuondoka bila kujua ni jinsi gani mama amechukizwa na kile kitendo changu.
Niliondoka pale nyumbani kabisa na kurudi kwa mamdogo huku nikitamani kumwambia kilichotokea ila nikaona aibu.
Kesho yake nikajifungasha tena ili niende kumuomba mama msamaha ila nilipofika yani hakuna aliyenisalimia hata mama aliyekuwa akinipokea peke yake aliniona ni mtoto mbaya huku kila mmoja akidai kuwa nina laana na ndio hapo nilipoamua kurudi tena kwa mamdogo na kuvunja ukimya, nilimueleza kilichotokea kwakweli mamdogo alisikitika sana na kuniambia kuwa dada yake ana haki ya kuchukia kwa kile kitendo ila laiti kama angejua nilifanya vile kumuokoa basi angechukia ila sio sana ila akaniambia kuwa na kama ningemueleza ukweli mama lengo la hiyo dawa ndio angenichukia zaidi.
Nikamuuliza mamdogo kwahiyo nifanye nini sasa akaniambia nitulie na mama atanisamehe mwenyewe, nikafikiria sana bila ya kupata majibu na siku zikaenda bila ya mama kunisamehe.
Kitu kingine kilichokuwa kikiniumiza katika maisha yangu ni kuwa hakuna mwanamke aliyeweza kunikubali moja kwa moja kutokana na hali ya maisha yangu nilikuwa nikimtegemea sana mamdogo ambaye naye hakuwa na shughuli maalumu ya kufanya. Roho ilikuwa ikiniuma sana haswa nilipokuwa nikienda nyumbani kwa mama mzazi na kufukuzwa na wanae na pale hata wanawake wa mitbni waliponikataa hapo nilijiona kuwa nina laana kweli aliyosema mama, nikalaumu kitendo changu cha kwenda kwa mganga kwani ni bora mwanzo nilichukiwa na bac wa kambo tu ila kitendo cha kuchukiwa na mama pia kiliniuma ukizingatia yule baba alikuwa na watoto wawili wa nje wa kike yani hawakuwa wa mama yangu ila mama aliwapenda kama watoto wake sasa kwanini mimi nichukiwe kiasi kile? Niliumia sana, kwenye ukoo napo karibia kila mtu alinichukia yani hawakuwa karibu na mimi kabisa zaidi ya huyo mama mdogo tu.
Siku moja nilikaa na mamdogo na kuongea nae kuwa kwanini inakuwa hivi, majibu yake yalikuwa haya,
"Mwanangu, katika dunia usitegemee kwamba utapendwa na kila mtu haswa pale ambapo utaonekana huna kipato. Jitahidi mwanangu, tafuta kazi na ukipata ifanye hiyo kazi kwa bidii na usisikilize watu wanasemaje bali usikilize moyo wako. Pesa ndio kitu pekee kitakachokupa kiburi, pesa itafanya hawa wanaokuona hufai sasa waje kukuomba msaada. Fanya kazi mwanangu, niangalie mimi na mambo yote yaliyosemwa juu yangu ila bado nipo tena ngangari kabisa, sitaki presha za watu sababu nasikiliza moyo wangu"
Swala la mamdogo kuwa nifanye kazi kwa bidii likaniingia sana kichwani mwangu, na ndicho nilichokuwa nikifikiria kwani nilihitaji kupata heshima katika jamii, nilihitaji kuheshimika ni hapo nilipopata wazo la kuzamia Mererani hata mamdogo hakujua kama naenda Mererani sababu nilimwambia kuwa naenda kutafuta kazi tu.
Nilikutana na changamoto nyingi sana lakini sitaweza kukuelezea ila cha msingi elewa kwamba utajiri wangu na pesa yangu niliibahatisha huko.
Nilipata hela kweli na kisha kuzamia mgodi mwingine huko Mwadui nako Mungu alinibariki kwakweli.
Ni hapo nilipofikiria swala zima la kuwekeza katika mali mbali mbali na ndipo nilipojenga ile hoteli Arusha ambayo ni sehemu mliyowahi kufika na kunikuta.
Pesa na mali zilinipa kiburi ila zilifanya wengi watambue uwepo wa Sam. Ni hapo nilipojenga nyumba Arusha na kumuomba mama mdogo akaishi huko, sikuweza kumwambia mama kwani bado hakutaka kunisamehe na kunisema kuwa nimelaanika.
Yote hayo hayakuwa tatizo kwangu, ila kuna tatizo moja ambalo huwa najuta na kujuta sana kuwa kwanini nililifanya. Nilitaka kukomesha baadhi ya watu ila mwisho wa siku nikajikomesha mwenyewe hadi leo najutia hili kosa.
(Hapo Sam alinyamaza kwa muda na kuinama kama mtu anayefikiria sana, kisha akainuka na kuendelea kuongea)
Kitendo cha wadada kunifata sababu ya pesa zangu kiliniumiza na kusema kuwa lazima nitawakomesha hao wanawake kwani kuna hadi wale niliowahi kuwapenda zamani sababu ya umaskini wangu wakanikataa ila nilipokuwa na pesa ndio hao hao wakajileta kwangu tena, nikajiapia kuwa lazima niwakomeshe hao wanawake wenye tamaa ni hapo nilipopata wazo la kwenye kwa mganga wa kienyeji.
Nilipata taarifa kuwa kuna mganga mashuhuri yupo Sumbawanga na wala sikujali umbali wa Arusha na Sumbawanga kwahiyo nikafunga safari kutoka Arusha mpaka Sumbawanga kwaajili ya kukutana na huyo mtaalamu na kwavile kipindi hicho nilikuwa na pesa kwahiyo swala hilo halikuwa gumu hata kidogo.
Namkumbuka yule mtaalamu alikuwa ni mzee mmoja hivi ila ni marehemu tayari, alinipokea vizuri sana na kusema kuwa shida yangu anaijua tokea mbali na alichoongezea nakumbuka alisema,
"Nina dawa ambayo niliitengeneza siku nyingi sana ila haikupata wa kuijaribisha ila kwavile wewe umekuja naomba nikueleze na najua kuwa lazima utaipenda dawa hiyo"
Nikawa makini sana kumsikiliza mzee huyo aliyeonekana kuwa na nia ya hali ya juu kunisaidia kwa kile ninachokitaka.
Nakumbuka alisema kuwa ananipa dawa ya jini ila jini hilo halitanidhuru kamwe ila nitawadhuru hao wanawake ninaowachukia halafu pia jini hilo litasaidia biashara zangu na zitaimarika zaidi.
Niliifurahia sana hiyo dawa kwani niliona nimepata dawa moja kwa kazi mbili, kwanza kuwakomesha wanawake na pili kuimarisha biashara zangu.
Nikakubali pale na ndipo aliponipa masharti ya dawa ile kwanza kabla hata ya kunipaka wala kuniambia kuwa naitumiaje. Aliniambia hivi,
"Kwanza kabisa hii dawa hakuna atakayejua kama unayo kwani itakuwa ndani yako. Mwanamke anapotaka kukutana na wewe kimwili, akikufanyia manjonjo hata kidogo tu hii dawa itakulazimu ulale nae kwani utapatwa na nguvu ya ajabu sana. Ukilala nae yeye atapatwa na maumivu makali sana, mpe onyo moja kuwa asimwambie mtu kwani akikiuka atakufa tu ila asiposema ataendelea kuteseka. Na katika biashara yako mambo yatazidi kuimarika kila unapolala na mwanamke."
Niliiona kuwa hiyo ni dawa bora sana ya kuwakomesha wanawake wote wenye tamaa ya pesa na wala sikufikiria mara mbili zaidi ya kumwambia kuwa anitengenezee dawa hiyo.
Naye hakusita na kuanza kunitengenezea dawa hiyo ambapo alinichanja sehemu za siri na kunipaka kisha akanichanja kwenye paja na kuchukua damu yangu kidogo na kuiweka kwenye chupa ambapo akaifunga muda huo huo halafu pale aliponichanja akanipaka dawa.
Muda kidogo akaifungua ile chupa na kusema ameshanikabidhi hilo jini ila halitakuwa karibu na mimi kama majini mengine yafanyavyo ila lenyewe litakuwa karibu pindi tu nitakapokuwa nataka kufanya mapenzi.
Niliona ni jambo jema sana ingawa kuna kitu aliniahidi na huwa nakikumbuka hadi leo, aliniambia hivi
"Pindi ukichoshwa na hii dawa itakupasa urudi tena kwangu ili niliondoe hilo jini. Kumbuka kuwa mimi ndiye niliyelitengeneza na hakuna mwingine yoyote wa kuweza kuliondoa zaidi ya mimi. Na tena nitaliondoa kwa kulirudisha tena kwenye ile chupa."
Niliona ni zoezi dogo sana na sikuwa na shaka kwani nilijua kuwa pindi nikikamilisha adha yangu na kuwakomesha wanawake wote wenye tamaa basi nitarudi tena kujirudisha kwenye hali yangu ya kawaida.
Tulimaliza shughuli pale na kulipa pesa kwaajili ya mizimu kisha nikaondoka zangu.
Nakumbuka nilikaa wiki nzima bila ya kukutana na mwanamke yoyote kimwili kisha nikaanza shughuli kwa kukutana na yule mwanamke aliyewahi kunikataa sababu ya umaskini wangu. Ila alinikubali kwa haraka sana sababu ya pesa zangu nami nikaamua kumtumia vilivyo.
Na muda nakutana nae kimwili alitaka kukimbia kutokana na mabadiliko yaliyotokea kwenye mwili wangu na hapo ndipo nilipojifunza kuzima taa kabla ya kukutana na mwanamke kimwili, ila nilikuwa na nguvu ya ajabu sana na kuamua kutumia nguvu hiyo ila mwisho wa siku ilikuwa kama kumbaka na alizimia pale pale.
Na nilipomaliza nilijilaumu sana kwa kile kitendo ila ndio hivyo ilishatokea tayari.
Alipozinduka alilia sana na nikampa onyo la kutokusema ila aliporudi kwao tu baada ya muda moyo uliniuma sana na nikaja kupata taarifa kuwa amekufa.
Nilitamani niende kwa mganga siku hiyo hiyo kuikataa ile dawa ila upande mwingine wa moyo ukawa mgumu sana kufanya hivyo.
Nilifikiria sana ila nikapatwa na wazo la kwenda kumuumiza mtoto mmoja wa baba yangu wa kambo halafu ndio niende kwa mganga kuitoa hiyo dawa.
Nikafunga safari hadi nyumbani kwa mama, kwavile nilikuwa na pesa wakanipokea vizuri sana hata mama alikuwa amenisamehe tayari kwa kosa lile la mwanzo.
Nilitumia pesa yangu kumlaghai yule mtoto wa baba naye akaingia laini hadi kufikia hatua ya kulala nae ambapo ndio nikamuachia janga kama la mwenzie na kumpa onyo kuwa asiseme.
Na hapo roho yangu ikawa imetulia ila nilijua wazi ikibumbuluka tu basi kazi ninayo.
Nikapanda gari yangu na kufanya safari ya kurudi Arusha.
Nikiwa njiani moyo uliniuma sana na kunifanya nirudi kwa mamdogo kwani nilijua wazi kuwa kule ndio nitapata habari zote.
Mamdogo aliponiona tu akaniambia kuwa ameambiwa mambo ya ajabu sana na mama kuhusu mimi eti nimekuwa muuaji, nilijifanya kukataa pale kuwa sio mimi ila mamdogo akaniambia kuwa mama kasema hatotaka kuniona tena katika maisha yake.
Nilijua wazi kuwa mama kaambiwa ukweli na kufanya moyo uniume zaidi.
Kesho yake nikasafiri na kwenda Dar es salaam ili nikafanye maisha huko na nilipofika kwakweli mji ulinipokea kwa shangwe na kufanya nijenge ofisi ile kubwa na kuanza biashara zangu na wala sikujishughulisha na maswala ya wanawake kwa kipindi hicho kwani nilijali kupata pesa kwanza Nilikaa mwezi mzima bila ya kuwa na mwanamke wa aina yoyote yule, ila walianza wenyewe kujipendekeza kwangu na ikawa kila nikilala na mwanamke namuachia janga kisha mimi naendelea zaidi, na yakawa kweli yale maneno ya yule mganga kuwa ninapomtesa mwanamke kwa janga hilo basi mimi ndio napata pesa zaidi na ndiomana haikuwa tatizo kwangu kuwamaliza.
Kwakweli nilichafua mji huu kiasi kwamba wengi waliniogopa na ndio hapo nilipoacha biashara zangu kwenye usimamizi kisha mimi kurudi Arusha ila napo sikukaa sana nikafanya safari ya kwenda Sumbawana ili nikaitoe ile dawa na niwe huru na niweze kuoa sasa.
Nilifika kule Sumbawana na kukutana na janga, yule mganga alikuwa amekufa.
Hapo ndio sikuelewa cha kufanya kabisa kwani matumaini yangu yakapeperuka yote muda huo huo kwavile nikikumbuka maneno yake kuwa ni yeye tu wa kunisaidia.
Nikakata tamaa na kurudi Arusha, nilikaa wiki na kusafiri kuelekea Dubai huko nikakaa miezi mitatu bila ya kukutana na mwanamke yoyote huku nikiendelea kufanya mambo yangu ya maendeleo na kuendeleza biashara zangu chini ya usimamizi niliouweka kwa watu ninaowaamini.
Nilitafakari sana mambo yangu na kuona kuwa licha ya wanawake kunitenda vibaya ila na mimi nimewatenda vibaya sana. Nikaona ni vyema nikikutana na mwanamke nimsaidie tu hata kama moyo hautaki, kisha nikarudi Tanzania na kwenda kuishi moja kwa moja Arusha, na baada ya siku mbili tangu nirudi alikuja mwanamke baada ya kumsaidia aling'ang'ania kulala na mimi nami nikajikuta nikifanya hivyo bila kutaka na kummaliza ila ndio nilivyozidi kuwa na mali kushinda mwanzo yani huyu mwanamke alinipa bahati sana sijui kwavile nilikaa muda mrefu kidogo bila kukutana na mwanamke? Ila kitendo cha kummaliza huyo mwanamke pia kiliniumiza, na baada ya wiki ndipo ulipokuja wewe na familia yako na kunikuta hapo nje ya hoteli kwakweli maelezo yako na maelezo ya wazazi wako yalifanya niingiwe na moyo wa imani sana ndiomana nikajitolea kukusafirisha ili ukasome"
Sam alipofika hapo alipumua kidogo kwani alikuwa na mengi sana ya kumueleza Sabrina ila Sabrina nae alipoona Sam amenyamaza kumueleza ikabidi amuulize sasa maswali ambayo bado yanamtatizo kutoka kwa huyu Sam na kutokana na story aliyomuelezea,
"Eeh Sam niambie basi kuwa kwanini uliamua kuwa kimapenzi na mimi hadi kunioa ingawa ulijijua kuwa unamatatizo? Na kama ulikuwa na nia ya kunimaliza mimi kama hao wengine kwanini hukufanya hivyo kwangu na kuwamalizia wakina Neema? Na kwanini....."
Kabla Sabrina hajauliza walisikia kamavile nyumba ikitetemeka na kumfanya Sam naye amuulize Sabrina kwa hasira,
"Kwanini umemtaja Neema......"
Nyumba ikazidi kuwa na tetemeko na kuwafanya wapate kizungu zungu ndani.
Itaendelea
No comments:
Post a Comment