Jeff na Sabrina wakatazamana tena kwani hakuna
aliyejua cha kufanya.
Sam akawashtua sasa na kusema,
"Nyie watu, sitaki masikhara mjue! Fanyeni
chochote mnachojua kabla sijawachagulia mimi
cha kufanya"
Kisha Sam akatoa bastora yake na kufanya uoga
uwashike.
Jeff akatamani kufanya kile anachokiwaza yeye ila akiangalia macho ya Sabrina yalikuwa yakipinga na kumfanya Jeff asubirie Sabrina afanye anachokitaka.
Sam aliwaelekezea ile bastora sasa na muda huo Sabrina akainuka na kwenda kumkumbatia Sam kwa gafla, ni kitendo ambacho Sam hakukitarajia kwakweli na kujikuta akiishusha ile bastora.
Sabrina alimwambia Sam kwa sauti ya chini kabisa,
"Kwanini unatufanyia hivi Sam? Najua wewe si mtu mbaya na wala huwezi kufikia hatua ya kutudhuru sisi ila kwanini unapenda kututishia maisha kila siku kwa bastora yako?"
Sam aliirudisha ile bastora, kisha akamtazama Jeff aliyekuwa amekaa kwa uoga.
Sam alimuangalia Jeff huku akimuuliza swali Sabrina,
"Kwanini umekuja kunikumbatia?"
"Nakujali na kukupenda"
Sam akacheka na kusema,
"Unanijali na kunipenda kisha unazaa na mwanaume mwingine halafu unasingizia kuwa ulibakwa!"
Sabrina alikaa kimya ila Sam akaongea tena na kumuomba Sabrina akae kwanza ambapo Sabrina alikaa pale pale pembeni ya Sam.
Kisha Sabrina akatoa ile barua ambayo alipewa na Sakina mara ya mwisho ili aisome.
Sam alianza kuisoma barua hiyo na kumuomba Jeff awapishe kidogo ambapo Jeff alitii na kutoka nje.
Sam aliisoma ile barua taratibu na alipoimaliza alimuangalia Sabrina na kumuuliza,
"Uliielewa hii barua?"
Sabrina akatingisha kichwa kuwa ameielewa, kisha Sam akamuuliza tena,
"Ni nani mwingine aliyeisoma hii barua"
"Ni Jeff"
"Aliipataje?"
Sabrina akamueleza Sam jinsi ilivyokuwa hadi Jeff kuipata barua hiyo na kumrudishia,
"Inamaana Jeff nae anajua kila kitu?"
"Ndio anaelewa kama nilivyoelewa mimi"
"Ok, tuachane na hayo. Tafadhari Sabrina niambie kilichopelekea wewe kunisaliti mimi? Na kwanini ulienda kutembea na Jeff bila kujua kasoro yangu?"
"Sam, ni kweli nimefanya makosa hata moyo wangu huwa unajutia. Ila Sam naomba na mimi nikuulize, hivi ni mwanamke gani anayeweza kuishi na mumewe ndani bila kufanya chochote kinachopelekea wao kuona kuwa ni kweli wapo kwenye ndoa? Sam nimeishi na wewe bila kujua tendo la ndoa likoje, ila mimi sio mwanamke tangatanga kama unavyonifikiria"
"Nalijua hilo Sabrina na nilijua kama wewe sio tangatanga kitambo sana ndiomana nikakuchagua huku nikiamini kuwa wewe utaenda kulimaliza tatizo langu. Na kweli kwa kiasi fulani ulinisaidia sana bila ya wewe mwenyewe kujua, na kama asingetokea Neema na kunipa madawa basi ni hakika kuwa asingekuwepo mdada mwingine tena kufa kwaajili yangu. Ila swali langu bado lipo palepale kuwa kwanini ulinisaliti na kusingizia kuwa ulibakwa?"
Sabrina kwa siku ya leo aliamua kuweka aibu pembeni na kumueleza Sam kilichotokea ile siku ambayo alibakwa kweli na Jeff.
Kule nje Jeff naye aliamua kuondoka huku akiamini kuwa ni rahisi kwa Sam na Sabrina kuelewana wakiwa wawili kuliko akiwepo na yeye.
Akiwa njiani akakutana tena na Aisha yule binti aliyekuwa akiishi na marehemu Neema kisha akasalimiana nae.
"Mbona hukunitafuta jamani!"
"Kwa bahati mbaya namba ilifutika labda unipe tena namba yako"
"Hakuna tatizo ila nitachukua na yako pia"
Kisha Aisha akamtajia Jeff namba yake akaiandika kwenye simu na kuomba aijaribishe kuipiga ambapo aliipiga.
"Hivi unaishi kwako au kwenu?"
"Naishi kwetu"
"Aah yani mi nakuona kuwa nakufahamu kabisa, licha ya kuonana hospitali ila nahisi kuna mahali pengine nilipowahi kukuona. Nitakumbuka tu, basi nitakutafuta kesho ili unielekeze kwenu nije kukutembelea"
"Sawa hakuna tatizo"
Wakaagana na kuondoka, kwakweli Jeff alimshangaa sana huyu Aisha kujiweka karibu naye kiasi kile,
"Mmh huyu mdada atakuwa ananitaka tu hata sio bure, mara kunifananisha sijui nini na nini wakati mi nipo kwenye harakati zangu na mke wa mtu"
Kisha akajicheka mwenyewe na kuendelea na safari yake.
Sam alimsikiliza Sabrina kwa umakini sana na kugundua kosa lilikuwa kwa Jeff kumbaka Sabrina kwani asingembaka yote yasingeweza kutokea kama ambavyo yalivyotokea.
Kisha akamuomba Sabrina kuwa amuite Jeff pale nje.
Sabrina alitoka na kuangaza nje ila hakumuona Jeff na kuamua kumuuliza yule mlinzi wa Sam,
"Khee mbona ameondoka muda mrefu tu"
Ikabidi arudi ndani kumueleza Sam kuwa Jeff alishaondoka, naye Sam akatabasamu na kusema,
"Itakuwa Jeff kaogopa bastora yangu wakati kumdhuru siwezi"
Sabrina alimuangalia tu kisha akakaa ambapo Sam akamuuliza jambo tena Sabrina,
"Ni kitu gani unapenda kujua kuhusu mimi?"
"Vipo vingi tu, kwanza kabisa ningependa kujua kuhusu maisha yako. Pili ningependa kujua kuwa kwanini umeishi na mimi kama mke ila bila ya kufanya tendo la ndoa na tatu napenda kujua ukweli wa mambo kuhusu barua niliyopewa na marehemu Neema"
"Ni hayo tu?"
"Na nne ningependa kujua kuwa kwanini unapenda kuishi na mimi ingawa nimeshazaa watoto wawili nje."
"Hilo swali la mwisho ni jepesi sana Sabrina, nang'ang'ania kuishi na wewe ingawa umenisaliti ni kwavile nakupenda, na pia siwezi kumdhuru Jeff ingawa najua ndio mwizi wangu kwavile nakupenda wewe na kama nikimdhuru yeye basi nitakuumiza wewe ila uwezo wa kumdhuru ninao tena mkubwa tu ila sitaki kumdhuru kabisa na pia kuna kitu kwenye moyo wangu kinanizuia sana kufanya hivyo, usiulize kuwa ni kitu gani ila kifurahie kitu hiko kwani mimi kiuhalisia ni katili sana na huyo Jeff ningekuwa nimemmaliza siku nyingi sana kwani sijamjua jana wala juzi kuwa ndiye mwizi wangu ila nimetulia nikimuangalia tu"
Sabrina akapumua kidogo huku akisubiri majibu ya maswali yake mengine, ambapo ni Sam aliyeendelea kuongea,
"Kwahiyo unataka kujua maisha yangu tangu kuzaliwa kwangu?"
"Ndio nataka kujua"
Sam akamueleza Sabrina kwa kifupi kuhusu maisha yake, akamueleza kamavile alivyowahi kumueleza dada yake Joyce ambaye ni mke wa James.
Jeff alienda kwanza moja kwa moja kwakina Sabrina kumuangalia yule mtoto wao wa kwanza ambapo alimkuta akicheza na bibi yake yani mama Sabrina.
Jeff alifika pale na kusalimia, yule mtoto naye yani Cherry alikuwa akitembea kwa kipindi hicho na moja kwa moja akaenda kumkimbilia Jeff na kumkumbatia hata mama Sabrina akashangaa,
"Khee wewe Cherry umekuwaje leo!"
Jeff akambeba kisha akaenda kukaa nae pale karibu na mama Sabrina kisha akamsalimia tena ila kwa furaha zaidi kwani alifurahia vile alivyopokelewa na Cherry.
"Haya karibu, hivi unajua kama usiku wa jana nilikuona? Ni kitu gani kinaendelea baina yako wewe na Sabrina?"
Jeff akajifanya kushangaa kwa muda kidogo kisha akajibu,
"Hakuna chochote kinachoendelea"
"Jeff, mi ni mtu mzima tena najua mengi kushinda wewe kwahiyo ni vigumu sana kunificha mimi ila ninachokwambia ni kuwa unatakiwa uwe makini sana yule Sabrina ni mke wa mtu. Halafu hivi hujihurumii jamani? Na udogo huo kweli? Unajua Sabrina amekupita miaka mingapi wewe? Yule ni mkubwa sana kwako, kwanini unataka kufanya vitu ambavyo vitakufanya ujute hapo badae? Kwanini ujitese kwa mtu mzima wakati vijana wenzio wapo? Kingine heshima iliyopo kwetu ni kubwa sana, mama yako ni kama mwanangu na kwanini utake kuharibu ukoo Jeff? Kufanana na watoto isiwe sababu ya wewe kujifanya ndio baba yao, kila mtu anatambua kuwa Sabrina ni mke wa mtu kwanini wewe hutaki kuheshimu hilo? Sijapenda kwakweli ulichofanya jana"
"Ila bibi umenifikiria vibaya tu, mi namuheshimu sana Sabrina na wala hakuna kibaya nilichofanya jana zaidi ya kumkumbatia. Kwani hairuhusiwi ndugu kukumbatiana?"
"Usitake kupoteza maana Jeff, laiti kama ile ingekuwa ni kukumbatiana tu wala nisingekuwa na mashaka ila nilikushuhudia kwa macho yangu ukipeleka midomo yako kwa Sabrina, haipo sawa hiyo. Heshima inatakiwa ichukue nafasi yake, Sabrina anakuchekea sana na ndiomana yote haya yanatokea ila angekuwekea ukali isingefika hapa ilipofikia. Narudia tena sijapenda na sitapenda ijirudie"
Simu ya Jeff ikaanza kuita wakati mama Sabrina akiendelea kuongea na kumuomba kidogo aongee na simu, naye alimruhusu kisha Jeff akapokea simu ile na mpigaji alikuwa ni Aisha,
"Vipi Jeff ushafika nyumbani?"
"Ndio nipo nyumbani tayari, vipi wewe"
"Hata mi nipo nyumbani, msalimie mama"
"Haya nitamsalimia, badae"
Kisha Jeff akakata ile simu na kumfanya mama Sabrina aulize,
"Ni nani huyo maana nimesikia sauti ya kike kwa mbali"
"Ni mchumba angu huyu bibi"
"Unaona sasa ambavyo vijana hamridhiki, yani mchumba unaye ila macho juu juu kwa wake za watu. Mtakufa huku mnajitazama"
Jeff akaona kuwa maneno yamezidi kuwa mengi hivyo akaaga ili aondoke.
Wakati anaondoka, Cherry naye akaanza kumlilia kuwa aondoke nae na kumlazimu mama Sabrina amchukue Cherry na kumbeba mgongoni ili amtulize kisha Jeff akaondoka.
Sabrina alisikitishwa sana kuhusu Sam na wazazi wake, akajifikiria kama angekuwa ni yeye angejisikiaje.
"Kwahiyo yule uliyenipeleka kule Arusha na akaja kwenye harusi sio mama yako mzazi?"
"Ndio, yule ni mamdogo ila ananipenda kama mwanae wa kuzaa kabisa"
"Na kwanini mama yako hakuja kwenye harusi?"
"Najua mama anatamani sana ila kuna kitu kimemfunga, ila najua ipo siku tu atarudisha moyo wake na atakuja kuniona mwanae"
"Kwani ulifanya kipi kikubwa?"
"Nilichofanya ndio kitakuonyesha na kukujibu maswali yote ya mwanzo kule juu na pia utaelewa kwanini sijawahi kukupeleka kwa mama na kwanini hakuja kwenye harusi yangu. Mama mdogo kanilea, kwakifupi ananifahamu sana kwani kanilea toka nikiwa mdogo. Alifukuzwa na mumewe ila aliendelea kunilea mimi. Kwa upande wa mama sasa ni ananijua kushinda vile anavyonifahamu mamdogo kwavile niliweka chuki wazi kwa kizazi cha mumewe ila bado anatambua kuwa mimi ni mwanae na ninaamini kuwa bado ananipenda katika moyo wake ingawa kawa mgumu kunisamehe"
"Basi niambie ulichomfanya mama yako na hao wengine"
"Ni historia ndefu kidogo ila kwavile nimejitolea kukujibu maswali yako yote basi sina budi kukueleza hali halisi ilivyo na kwanini nipo hivi"
Sabrina alitulia kwani alitaka sana kujua kuwa ni kitu gani kilichotokea kwa Sam.
Jeff naye alirudi kwao na kumkuta mama yake akiwa ametulia sebleni na kumsalimia, ila mama yake akamuuliza swali lililomshangaza kidogo,
"Hivi ni lini nitamtambua mkwe wangu Jeff?"
"Kwanini mama?"
"Hivi unajua furaha ambayo niliipata siku ya kwanza kusikia kuwa Dorry ana mimba yako? Hivi unajua wazo lililokuwa kichwani mwangu wakati Dorry anajifungua? Mtoto hakufanana na wewe ila bado niliendelea kujipa matumaini kuwa ni mjukuu wangu hadi pale nilipoona kuwa mtoto anazidi kufanana na wachina. Tafadhari Jeff fanya kitu cha kunifanya mama yako nifurahi, nipo tayari kumlea mjukuu wangu kwa hali na mali"
Jeff akafikiria kidogo jinsi mtoto Cherry alivyomlaki na akafikiria kama ndio angekuwa anaishi nae pale nyumbani kwao ingawa anaona wazi kuwa ni jambo lisilowezekana.
Baada ya ukimya kidogo akaamua kumpa moyo mama yake,
"Usijali mama, mkweo nitakuletea hivi karibuni"
"Na iwe kweli mwanangu"
Kisha Jeff akainuka na kuelekea chumbani kwake, huko akafikiria namna ya kumpanga Aisha ili amlete kwao na aweze kumwambia mama yake kuwa ndiye mkwe ila pia akamfikiria Sabrina kuwa atamuona ni msaliti.
"Ni kweli Sabrina ni mke wa mtu ila nampenda sana na nilimuahidi kuwa sitamuacha kamwe kwani sijali chochote, sasa nikimtambulisha huyo hata kwa utani tu atanielewa kweli?"
Jeff alijikuta akifikiria sana swala hilo.
Sabrina bado alihitaji kusikia kutoka kwa Sam ambaye alimuomba wale kwanza kwani chakula kilishafika.
"Usijali, nimeamua kukueleza na nitakueleza kila kitu ila subiri tule kwanza"
Sabrina alikubaliana na ile hoja ya Sam huku akila na kuanza kuwaza zaidi atakachoelezwa na Sam.
Walipomaliz a kula sasa, Sam aliamua kuanza kumueleza Sabrina.
"Katika ujana wangu niliamua kulipa kisasi, na kisasi hicho nilianza kwa familia yangu mwenyewe yani kwa watoto wa baba yangu wa kambo.
Sikuwa na uwezo kipindi hicho yani sikuwa na pesa ndio kitu kilichofanya wengi wasinipende na wadada wengi wanikatae. Ni hapo nilipoamua kwenda kwa mganga wa kienyeji lengo kuu lilikuwa kumkomesha baba wa kambo kabla ya kushughulika na mengine. Yule mganga akanipa dawa ili nikaweke kwenye maji ya kuoga huyo baba.
Nikafunga safari siku hiyo na kwenda kwa mama, nikamkuta kaandaa maji ya baba ya kuoga ni hapo nikaona kuwa nimepata nafasi ya kuweka dawa yangu.
Mama alivyotoka tu bafuni, nikaenda kumimina ile dawa yote kisha nikatoka nje na kukaa mbali kidogo na bafu ili kusikilizia majibu ya ile dawa atakavyooga yule baba.
Muda kidogo nilimuona mama akitoka ndani kwa hasira huku akisema kuwa ni bora tu akaoge mwenyewe hapo nikaelewa wazi kuwa lazima baba amekataa.
Nikataka nikimbilie bafuni ili nikamwage yale maji ila kabla sijafika bafuni mama alikuwa kashaingia tayari.
Itaendelea
No comments:
Post a Comment