MREMBO WA KIJIJI.
SEHEMU YA TANO-05
"Anhaaaa hahaaaa" Alicheka mwenyekiti baada kusikia mkwala wa mzee Nhomo aliposema kuwa ni ni rahisi ng'ombe kutikisa mkia kuliko mkia kumtikisa ng'ombe. Na mara baada kukatisha kicheko chake akasema "Hakuna tatizo mzee mwenzangu, nitamueleza. Ila kitakacho fuata mimi simo jamani"
"Walaa usihofu ndugu mwenyekiti" Alijibu mzee Nhomo kisha akarudi kwenye umati wa watu uliokusanyika msibani.
Jioni ilipowadia, mzee J alikwenda kwa mwenyekiti kwa mara nyingine tena. Safari hiyo alikwenda kwa niaba ya kufahamu kama ameshamfikishia ujumbe mzee Nhomo.
"Hodi hodi mwenyekiti" Alibisha hodi mzee J. Wakati huo mwenyekiti alikuwa ndani akatafuta kibiliti ili akoke moto nje apate kuota huku akichoma karanga, kwani msimu huo kijijini Ndaulaike ulikuwa wa kuvuna karanga. Mwenyikiti aliposikia sauti ya mzee J akibisha hodi malangoni kwake aliguna kidogo halafu akajisemea "Mwaka huu watatoana roho hawa wazee" Kwisha kujisemea hayo akamutika "Karibuuu.. Karibu karibu" Alisema sambamba na kutoka ndani na karanga mbichi zenye maganda ndani ya kisufulia kidogo.
"Ndio habari za tangu muda ule tulipoachana" Alisema mzee J. Mwenyekiti kabla hajamjibu aliweka chini kwanza vitu alivyokuwa navyo mkononi na kisha akajibu " Aaha salama tu sijui mwenzangu"
"Mimi pia niko salama, nimekuja bwana. Nia yangu kujua Je, ulimfikishia ujumbe mzee Nhomo?.."
Mwenyekiti alishusha pumzi kisha akajibu "Ndio nimemfikishia, ila kanijibu kwamba siku zote Ng'ombe hutikisa mkia na sio mkia kumtikisa Ng'ombe" Mzee J alishtuka kusikia maneno hayo, baada ya mshangao huo uliombatana na taharuki ya aina yake aliangua kicheko kisha akasema "Nashukuru ndugu mwenyekiti" Aliondoka zake mzee J baada kumshukuru mwenyekiti wakati huo moyoni mwake akiwa amefura hasira zisizo na mfano.
"Mzee Nhomo hakijui vizuri kijiji hiki, sasa nataka nimuonyeshe kuwa mimi J sio wa kuchezewa kama pombe ya ngomani " Alijisemea hivyo mzee J huku akizipiga hatua za haraka haraka kurudi nyumbani kwake. Lakini wakati anatembea hana hili wala lile, mara ghafla alisikia sauti ya mzee Mambosasa.
"J mbona watupita kama hutuoni?.." Alisema mzee Mambosasa
"Muacheni huyo kavurugwa. Hivi mnajua kuwa J na Nhomo wanavita ya chini kwa chini?.." Ilidakia sauti nyingine ambayo haikuwa ya mtu mwingine bali ni ya mzee Samueli. Wote kwa pamoja walikuwa wakiongea huku wakinywa pombe aina ya gongo. Hivyo sauti aliyopasa mzee Mambosasa ni kumtaka mzee J aungane nao kwenye hicho kilinge. Ila mzee J hakutaka hata kuwasikiliza, aliambaa na njia ya kuelekea nyumbani kwake hata asiseme neno lolote.
"Enhee vitagani hiyo bwana Samueli unaweza kutuambia? .." Alidakia mzee mwingine. Mzee Samueli alikaa kimya kwanza akanywa gongo yake kidogo, akaisikilizia akiwa amekunja uso mithili ya kiatu cha baniani kisha akasema "Mtoto huyu mzuri mzuri"
"Mmh yupi huyo?.." Aliuliza Mambosasa.
"Si huyu Chaudele? Huyu ndio chanzo cha haya yote bwana.." Alijibu mzee Samueli.
"Doh kisa?.."
"Kijana wa mzee J yule Chitemo anamtaka Chaudele binti wa mzee Nhomo, ajabu walishapeleka mpaka posa. Sasa mzee Nhomo kagoma, hataki binti aolewe na mtoto wa mzee J. Hapo ndipo kizaa zaa sasa. Cha kushangaza na chakustaajabisha mzee Nhomo posa amekula, lakini mtoto hataki kumtoa"
"Mmmh hapo ni kupatwa kwa jua na mwezi ndugu zangu, tunyweni gongo yetu tuondoke tu maana huo mchezo haustahili kuchezwa peku" Alisema mzee Mambosasa akiwaasa wenzake.
"Ni kweli kabisa" Alijibu mzee Samueli kisha wakaendelea kunywa pombe yao.
Upande wa pili, nyumbani kwa mzee Nhomo.
"Mke wangu nafikiri hiki kijiji bado hawajanitambua mimi ni nani?.." Aliongea mzee Nhomo.
"Kwanini unasema hivyo mume wangu?.." Aliuliza mama Chaudele. Mzee Nhomo alishusha pumzi ndefu halafu akajibu "Wakati nipo msibani, mwenyekiti aliniita faragha. Nikatii wito. Akaniambia bwana mzee J kasema kuwa yeye sio mtu wa kuchezewa, kama sikutaka mwanangu aolewe kwanini nilipokea posa yao. Akasema kwamba hahitaji ni mrudishie hiyo posa ila anachotaka yeye ni mke la sivyo nitakiona cha mtema kuni"
"Mmh ndivyo kasema hivyo? " Alitaharuki mama Chaudele akionekana kukumbwa na wasiwasi. Lakini wakati mama huyo yupo katika hali hiyo, mzee Nhomo aliongeza kusema "Nadhani huyu mzee hanijui. Mimi sio wa kupigwa mkwala wa kitoto, na sema hivi posa sirudishi wala mke hapati. Halafu nione atanifanya nini. Mpuuzi mkubwa tu yule" Alipokwisha kusema hayo mzee huyo akaingia ndani. Alizama moja kwa moja mpaka chumbani, akainama ufunguni mwa kitanda chake. Punde si punde akatoka na jungu kukuu lililosheheni mazagazaga ya kichawi. "Kuna wakati mwanajeshi anastafu vita, ila anapoona taifa lake limeandamwa na vita hali ya kuwa msaada wake ni wamuhimu sana. Basi hurudia kuvaa gwanda na kurejea uwanja wa vita" Alijisemea mzee Nhomo wakati huo akichambua baadhi ya hirizi zilizokuwemo ndani ya jungu lake. Jungu kuu lililojaa utandu wa bui bui.
Kwingineko, Pili alikuwa amejiinamia akilia kwa uchungu. Ukweli Pili alimpenda Chitemo, hivyo kuachwa kwake kulimfanya aumie moyoni na ndio maana hapo awali alionekana kutoamini uamuzi wa Chitemo, ila baada kutimuliwa na mama Chitemo hapo ndipo alipoamini kuwa Chitemo sio wake tena. Lakini wakati Pili anayalila mapenzi, mara ghafla alisikia mzigo wa kuni ukitupwa chini. Pili alishtuka akainua uso wake kutazama kule ulipoangukia mzigo, akamuona bibi yake. Alikuwa amerejea kutoka shambani.
"Pili mbona unalia? Kulikoni" Aliuliza huku akimsogelea. Bibi huyo ambaye alimpenda mno mjukuu wake, katu hakutaka kuona Pili akifadhaika moyoni mwake. Kwani aliamini kufanya hivyo inaweza kumpelekea kuwakumbuka wazazi wake ambao tayari wameshatangulia mbele ya haki.
"Pili mjukuu wangu niambie nini kimekusibu mpaka uonekane hivyo" Aliongeza kusema bibi huyo. Pili alipandisha kwikwi na kisha akasema kwa sauti iliyoambatana na kilio "Bibi, Chitemo. Chitemo bibi"
"Chitemo?.." Alijiuliza bibi Pili.
"Kafanyaje huyo Chitemo?.."
"Chitemo kani... kani aaacha" Alijibu Pili huku akilia.
Bibi Pili alishtushwa na maneno hayo. Hapo akanyanyuka na kisha kuhoji kisa hasa kilicho pelekea kuachwa. Lakini Pili hakujibu zaidi ya kuendelea kububujikwa na machozi. Machozi ya Pili yalimchoma bibi yake, ambapo alizipiga hatua kuingia ndani huku akisema "Mjukuu wangu wewe sio kuchezewa na kuachwa kirahisi hivyo, ngoja nitamkomesha mshenzi yule" wakati o bibi Pili akipania kumfanya kitu kibaya Chitemo, kwingineko mzee J alikuwa tayari yupo katika mavazi yake maalumu, nguo nyeusi huku kichwani akiwa amejifunga kitambaa chekundu, mkononi alikuwa ameshika na kibuyu kidogo kilicho tapakaa damu. Alizipiga hatua kutoka nyumbani kwake na kuchikichia kunako poli ndogo, ila kabla hajafika mbali mkewe akamuuliza "kulikoni tena baba Chitemo unaenda wapi na giza hili totoro?.."
"Nataka nimuonyeshe kazi mzee Nhomo ili akae akijua kuwa sio kila anayevaa kanzu ni sheikhe wingine wanaficha mabusha tu" Alijibu mzee J kwa kujiamini.
"Khaa unamaana gani?" Alirudia kuhoji mama Chitemo, lakini safari hiyo mzee J hakumjibu zaidi ya kuamba na njia katika giza totoro ambalo lilikuwa limetanda katika kijiji cha Ndaulaike.
Itaendelea
KIPI KILIJILI HAPO HAPO? HAYA TIMU #Nhomo kumbe na sisi kiongozi wetu yuko freshi anatungua daluga lake. Watatuweza kweli?
BALAA ZITO... SHEA MARA NYINGI ILI USIPITWE NA KIGONGO HIKI CHA KUSISIMUA.
No comments:
Post a Comment