MREMBO WA KIJIJI.
SEHEMU YA SITA-06
Mzee J alijongea hadi kunako mti mkubwa kijijini Ndaulaike, mti huo ulikuwa msufi. Kipindi cha nyuma huo mti ulitumika kwa shughuli maalumu ambayo ilikuwa ya kutambikia mizimu. Hivyo mzee huyo baada kufika kwenye mtu huo alitandika chini kitambaa cheupe kisha akaweka kibuyu chake juu ya kitambaa hicho na kuanza kuimba. Aliimba nyimbo zake za asiri kwa muda wa nusu saa, punde baada kumaliza zoezi hilo kilitokea chungu pembeni yake na sauti nzito ikasikika ikisema "Ndio mwangulu wenje, imbonya mukasinya" Sauti hiyo ikiwa na maana kuwa ndio mjukuu wangu nakusikiliza.
Mzee J alishtuka baada kusikia sauti hiyo, sauti ya moja ya mizimu inayoishi ndani ya msufi huo. "Mizimu nimekuja kwenu ili mnipatie nguvu ya kupigana na Nhomo, sababu naona hataki kuendana na matakwa yangu.." Alisema mzee J wakati huo tayari akiwa amenyanyuka kutoka chini baada kusikia sauti ya mzimu.
"Anhaaa ha ha ha haaaaa" Mzimu ukicheka, kicheko hicho kilisikika kikijirudia mara mbili mbili, na wakati sauti hiyo ya kicheko ikisikika hivyo, mara ghafla popo walikurupuka kutoka katika majani ya mti huo. Sauti za mbawa wa popo hao na sauti ya kicheko cha mzimu zilipelekea sehemu hiyo kuzizima sauti ya ajabu. Mzee J aliogopa lakini akajikaza kisabubuni mpaka pale sauti hizo zilipotoweka.
"Jaruoo, wewe ni mwana utawa. Na tutafurahi kama utaufanyia kazi huu utawa. Kabla hujafika hapa tulijua dhamira yako ni ipi, na kukuaminisha hilo hebu geuka tazama nyuma yako" Ilisema sauti hiyo baada kukatisha cheko. Hima mzee J akageuka nyuma yake, akaona jungu lililosheheni mazaga ya kichawi. Hapo kicheko kilisikika kwa mara nyingine kisha ikasikika sauti ikiongeza kusema "Usihangaike ukihitaji kitu wewe njoo. Wangulu Jaruooo hahahahaaa!.."
"Lakoze chane chane" Alijibu mzee J akiushukuru mzimu. Baada ya hapo alichukuwa chungu hicho alichokabidhiwa akatandua kitambaa chake cheupe kisha akazipiga hatua kurudi nyumbani kwake. Lakini wakati mzee J ameondoka hapo msufini, punde si punde kundi la wachawi walitua mahali hapo na nyungo zao. Moto ulikokwa wa kuwamba ngoma, zoezi hilo lilichukua muda mfupi kumalizika ambapo muda mchache baadaye zilipigwa ngoma. Wachawi hao waliimba na kucheza kwa style ya kuwazunguka wapiga ngoma ambao walikuwa wamekaa karibu na moto. Baadaye kidogo ngoma ilisitisishwa na kila mmoja akakaa mahali pake kisha mkuu wa msafara huo akasimama na kusema "Habari zenu ndugu zanguni" wachawi waliokuwepo hapo chini ya msufi waliitikia wote kwa pamoja huku vigelegele na kupiga ngoma vikisindikiza muitikio wa salamu yao. Mkuu huyo wa msafara alionyesha tabasamu kidogo na kisha akaendelea kusema "Jamani najua kila mmoja amecheza vizuri ngoma yetu ya usindengo. Ngoma maarufu sana hapa kijiji cha Ndaulaike, bila kubagua nyote mmecheza vizuri kiukweli. Lakini pia tukiachilia mbali hafla hii, napenda kumkaribisha makamu wangu bibi Pili. Siku hii ya leo anajambo anataka kuwaambia. Bibi Pili karibu sana "
Bibi Pili alinyanyuka kutoka mahali alipokaa, shangwe na vigelegele vilisikika wakati huo akijongea mbele. Alipofika alitoa salamu yake kisha akasema "Ndugu zanguni, nafikiri kila mmoja anafahamu kuwa mimi nina mjukuu nyumbani " Alisema bibi Pili huku akionekana kutaka kuendelea kusema alichotaka kukusudia kuongea, lakini alishindwa baada fujo za kushangilia kuzuka mahali hapo ilihali wakati huo minong'ono nayo pembeni ikisikika ikisema "Atakuwa anataka kututambulisha kwa mjukuu wake ama nini?.."
"Mmh sidhani ila itakuwa poa sana kama na mjukuu wake tukiwa naye huku"
"Hapana jamani nitafurahi sana"
"Anhahahahahah hahahahaaa " Minong'ono hiyo na vicheko vya hapa na pale vilidumu kwa muda wa dakika kadhaa, lakini mwishowe mkuu wa msafara alipasa sauti akisema "Jamani tusikilizane, kaeni kimya. Basi inatosha"
Wachawi hao waliposikia sauti ya mkuu wao walitii, wote kwa pamoja walikaa kimya na kumsikiliza bibi Pili. Bibi Pili alikohoa kidogo kisha akaendelea kusema "Kwa kipindi kirefu mjukuu wangu alikuwa yupo katika mahusiono na kijana wa mzee J. Kama mnavyojua tena mambo ya vijana. Mjukuu wangu mwenyewe akawa ananiambia bibi nampenda sana mtoto wa mzee J ipo siku atanioa. Kiukweli sikutaka kumpinga wala kumbishia mjukuu wangu sababu nampenda halafu istoshe ni yatima, kwahiyo niliona endapo nitambania atakosa furaha na kujikuta akiwakumbuka wazazi wake. Lakini leo nilipotoka shamba nikamkuta analia nikamuuliza nini tatizo? Akanijibu kwamba mtoto wa mzee J, baadhi yenu mtakuwa mnamfahamu, huyu Chitemo. Eenhe basi mjukuu wangu akaniambia Chitemo kaniacha. Kiukweli hili ni suala ambalo limeniuma sana ndugu zanguni, maana haiwezekani mjukuu wangu achezewe mwishowe aachwe kizembe. Naombeni ushirikiano wenu ili niweze kumuadabisha, mjukuu wangu sio uwanja wa mazoezi" Alisema bibi Pili huku akiwa amejawa na hasira. Wachawi waliokuwepo pale wote akiwemo na mkuu wa msafara walisikitishwa na kisa hicho.
Kijana mmoja aliyeonekana kavaa bukta huku akiwa kifua wazi, alisimama na kisha kusema "Ni heri mmeliona suala hili, ukweli huyu mtoto wa mzee J anatukosesha amani hapa kijijini. Asilimia kubwa vijana wa hapa tuna...." Kabla kijana huyo hajamalizia shtaka lake, mkuu akapasa sauti akasema "Tuondokeni hapa sio pakuendelea kukaa" Amri hiyo ilitekelezwa haraka sana iwezekanavyo, wachawi hao wakapanda nyungo zao wakaondoka hapo msufini wakati huo huo kundi la popo liliwafuata nyuma kwa kasi ya ajabu ila mwishowe hao popo walirejea msufini baada kuwatimua wachawi hao waliokuwa wakiendesha kikao chini ya msufi huo.
Lakini licha ya kundi hilo la wachawi kutimuliwa na popo kutoka Msufini,walipofika mbali ya eneo hilo waliweka kambi kwa mara nyingine tena ambapo mkuu wa msafara hakutaka hoja tena ziendelee zaidi alisema "Usiku huu tayaru umeshatiwa gundu, hivyo hapa sitotaka kila mmoja aeleze masuala yake bali kilichobaki ni kuwa bega kwa bega na bibi Pili ili atimize azma yake. Sisi wote kwa pamoja tunasaidia, hivyo bibi Pili usijali kuhusu hilo. Lakini kabla hatujaanza mkakati huo naomba tukutane kwa mara nyingine, sababu nina mengi ya kusema nanyi" Kwisha kusema hayo kila mmoja alipanda kwenye ungo wake na kurejea nyumbani.
Wakati kwingineko napo alionekana mzee Nhomo ndani ya ungo, punde si punde mzee huyo alitua chini ya mti wa muembe. Mti mkubwa pia kuliko yote kijijini Ndaulaike. Aliimba nyimbo zake za asiri kama alivyofanya mzee J hapo awali, lakini zoezi hilo halikuchukuwa muda mrefu wakatokea watu wawili wakiwa na vibuyu mkononi. Vibuyu hivyo vilikuwa vimezungushiwa shanga za kila aina na rangi tofauti tofauti.
"Ndio Nhomo tumetii wito wako" Alisema mmoja kati ya wale watu wawili waliokuwa wamejifungaa nguo nyeusi kiunoni na kichwani wakiwa wamejifunga vitambaa vyekundu ilihali mikononi juu karibu na magega wakiwa wamejifunga hirizi.
"Nimekuja kwenu sasa, nina imani mtanisaidia. Kule nilipo hamia kuna mjinga anataka kuchezea akili yangu, hivyo naombeni msaada wenu tafadhali"
"Anhahahaaaaa hahahahaaa. Nhomo, unataka kurudi kwenye kilinge?.." Aliuliza mtu wa pili naye alikuwa ni mwanamke.
"Kabisa maana la sivyo itanighalimu, nataka nimuonyeshe kuwa utu uzima sio ndevu bali ni busara" Alijibu mzee Nhomo kwa utashi kabisa.
"Sawa kwa heshima yako msaada tunakupa" Aliongeza kusema mtu huyo.
"Hakika nitashukuru sana" Alijibu mzee Nhomo. Punde si punde mtu mmoja kati ya watu wale wawili alinyoosha mkono juu,ukatokea ungo mweusi uliojaa dhana mbali mbali za kichawi. Mtu huyo aliushusha chini mkono wake kisha akasema "Haya Nhomo hitaji lako limetimia, kazi kwako " Alipokwisha kusema hayo mtu huyo wakapotea wakamuacha mzee Nhomo akizisogelea dhana zile za kichawi huku akiachia tabasamu bashasha.
Kesho yake asubuhi, mzee Mligo alisikika akimuita mjukuu wake wakuitwa Saidon, kijana kutoka Dar es salaam. Tayari siku ya jana alifika, na hivyo asubuhi alisikika akiamshwa na babu yake.
"Saidon.. Saidon Saidon.."
"Mmh naam babu" Aliitikia Saidon.
"Amka nikupe maagizo kabla sijaelekea shamba" Alisema mzee Mligo. Saidon akajikushanya kutoka kitandani, hima akatii wito wa babu yake.
"Ndio babu shkamoo"
"Malakhabaa pole na uchovu bwana"
"Nilishapoa babu"
"Eeeh sasa mimi naelekea shamba mara moja. Mihogo tayari nimeshakuchemshia toka saa kumi na moja kwahiyo ukishanawa uso kula usiniachie" Alisema mzee Mligo.
Saidon akajinyoosha akapiga mwayo halafu akajibu "Sawa babu nimekuelewa"
"Lakini kuna jambo nataka nikuase mapema" Aliongeza kusema mzee Mligo.
"Ni lipi hilo!?" Kwa taharuki Saidoni aliuliza.
"Umekuja huku naomba utulie ukae ukujua kuwa hapa ni kijijini na sio mjini, kwahiyo chunga sana sio kila shimo lazima utie mguu"
"Mmmh unamaana gani babu?.." Alihoji Saidoni hata asielewe kile alicho manisha babu yake.
"Nitakujibu tu, ila fahamu hapa ni Ndaulaike na siku zote ukae ukijua kuwa ndimu changa hailiwi"
ITAENDELEA..
Ooooh kumbe mwanaume wa Dar kaingia Kijijini, Ahsante sana Saidoni nafikiri ile zawadi umeniletea ingawa babu anatutisha.
Naam! Bibi Pili ameongezeka, mzee J tayari amenoa makali lakini pia mzee Nhomo ametungua daluga. Wamedhamiria kweli kweli.. Kipi kitaendelea?
SHEA MARA NYINGI KWENYE MAGROUP YOTE ULIYO ILI USIPITWE NA KIGONGO HIKI CHA KUSISIMUA.
No comments:
Post a Comment