YAPO mengi mazuri ambayo huenda mpenzi wako aliwahi kukufanyia, je uliwahi kumshukuru kwa kukufanya ufarijike? Naamini Mungu amekujaalia kuwa na mpenzi mzuri, mwenye kila sifa ambayo ulitamani awe nayo, je ulishawahi kumsifia hata kwa kumwambia ni mzuri?
Huenda ulishawahi kufanya hivyo lakini kwa taarifa yako wapo ambao wanahisi kufanya hivyo eti ni ulimbukeni. Ulimbukeni? Kumsifia mpenzi wako unaona ni ulimbukeni wakati wataalam wa masuala ya mapenzi wanaeleza kuwa, wanawake ni watu wanaopenda kusifiwa sana hata kwa madogo wanayoyafanya?
Unaona hatari gani kumsifia mpenzi wako kuwa ni mzuri? Unadhani unatumia nguvu gani kumsifia mpenzi wako kutokana na mahaba mazito anayokupata?
Kwa taarifa yako unaweza kuona ni kitu kidogo sana lakini madhara yake kwenye penzi ni makubwa.
Kumsifia mpenzi wako kwa yale anayokufanyia kuna faida nyingi sana lakini kwa leo nitagusia chache. Kwanza kunaongeza mapenzi. Mume/mke anaposifiwa kuwa anajua mapenzi hata kama si kwa kiwango kikubwa, anafarijika sana.
Unapomwambia mpenzi wako: ‘Dear nashukuru kwa mapenzi uliyonipa jana, umenipa furaha ya ajabu ambayo siamini kama kuna mtu mwingine wa kunipa, nakupenda sana’.
Maneno kama haya hutumii nguvu wala muda mwingi kuyafikisha kwa mpenzi wako lakini uzito wake ni mkubwa. Kwanza anajihisi aliyekamilika kwa kufikia hatua ya kufanya mambo yakamridhisha mpenzi wake na kwa mazingira hayo anaamini huwezi kumsaliti. Hisia hizo zitamfanya azidi kukupenda.
Hilo ni kwa wote yaani kwa mwanaume na mwanamke. Lakini pia unapomsifia mpenzi wako kwa yale anayokufanyia, unamfanya aongeze kasi ya kukufanyia ili nawe uzidi kumpenda.
Kwa mfano, unapokutana na mpenzi wako kisha ukamwambia ‘umependeza kweli mpenzi wangu, nazidi kukupenda kwa unavyovaa’.
Mtu anayeambiwa maneno haya atajitahidi sana siku zote aonekane nadhifu na wa kuvutia kwa mpenzi wake akijua kwamba, akivaa ilimradi kuvaa, hatamfurahisha mpenzi wake. Kwa maana hiyo kumsifia mpenzi wako kunamfanya azidi kuwa bora.
Lakini kusifia kusiwe kwa kinafiki. Usimsifie mpenzi wako eti ili kumfanya ajione bora kumbe katika uhalisia siyo hivyo.
Tusifiane pale inapobidi huku tukijua kuwa kwa kufanya hivyo tutapata faida. Tusiwe na tabia ya kuchukulia poa kila tunachofanyiwa na wapenzi wetu.
Kama kakuridhisha kimapenzi, msifie kwamba yeye ni muhimu kwako kwa kuwa amekupa ulichotarajia. Amekupikia chakula kizuri, msifie kuwa yeye ni mpishi mzuri. Hiyo italinogesha penzi na utashangaa kila siku inayokwenda kwa Mungu penzi lenu linachanua.
Lakini mbali na hayo, unatakiwa kuridhika kwa kile unachokipata kutoka kwa huyo mpenzi wako ulinaye kwa sasa. Najua kwenye uhusiano wengi tumetoka mbali. Wapo waliowahi kuwa na wapenzi zaidi ya mmoja huko nyuma na kila mmoja alikuwa na kiwango chake cha kukuridhisha.
Inawezekana kuna ambaye unamkumbuka kwa mapenzi mazito aliyokuwa anakupa zaidi ya huyo uliyenaye. Hiyo ni historia, imepita! Kama huyo uliyenaye si mtaalam sana wa kukufikisha pale unapopata, ridhika na hicho kidogo unachokipata endapo atakuwa anaonesha kukupenda kwa dhati.
Mpe moyo, msifiesifie kidogo kwa hiyo furaha kiduchu anayokupa huku ukiamini kuwa, atabadilika kadiri siku zinavyokwenda.
Kumbuka cha msingi katika maisha yetu ni kumpata mtu mwenye mapenzi ya kweli na si kumpata anayeweza kukuridhisha katika mambo kadha wa kadha.
No comments:
Post a Comment