Hayo ndiyo yakawa maisha ya Kayumba na Edga, maisha ya furaha wakati wote. Wasaka tonge hao walipambana kufa na kupona kuisika shilingi, hakuna hata mmoja aliyeonyesha uvivu kumtegea mwenzie. Na kadri siku zilivyozidi kwenda, ndivyo mtaji wa kununua madafu ulipoongezeka. Awali Kayumba alikuwa akinunua madufu themanini, sasa hatimaye idadi iliongezeka.
"Mambo sio mabaya rafiki yangu", aliongea Kayumba akimwambia Edga, muda huo ilikuwa yapata saa moja usiku wakiwa wameketi ndani ya mgahawa wakila chakula.
"Naam! Nafikiri juma lijalo tununue mkokoteni wetu sasa", alijibu Edga.
"Hata mimi nilikuwa nafikiria suala hilo hilo"
"Kweli?..", alihoji Edga. Kayumba akajibu "Ndio..", kisha wote kwa pamoja wakaangua kicheko. Walipohitimisha vicheko vyao, Edga akasema "Unajua rafiki yangu siku zote jasho la mtu haliliwi, na endapo kama utathubutu kulila basi ujue utapata madhara. Kayumba wahenga wanasema kazi mbaya ikiwa yako, mimi naomba tupambane ukweli njia ya utajiri naiona siku za usoni"
"Hahahahahahah..", aliangua kicheko Kayumba, maneno ya Edga yalionekana kumvunja mbavu.
"Usicheke bwana huo ndio ukweli, na nilicho gundua wewe unanyota ya fedha. Hivyo basi nyota yako hiyo hiyo ndiyo itakayo tupatia utajiri", aliongeza kusema Edga.
"Huwenda ikawa kweli, maana kama lisemwalo halipo basi linakuja. Mimi nakubaliana na maneno yako Edga", alijibu Kayumba wakati huo wakitoka ndani ya mgahawa huo na kisha kuanza safari ya kuelekea maskani kwao. "Unajua mpaka sasa sijajua ni kwanini wale jamaa zako wameamua kuchagua maisha yale, maisha ambayo kifo kipo mkononi", aliongeza kusema Kayumba.
"Rafiki yangu Kayumba kuishi ni kuchagua, wale jamaa wameamua kuchagua yale maisha kama ambavyo sisi tumechagua...",Edga alijibu kisha kimya kidogo kilitawala. Lakini baadae kidogo kimya hicho kilitoweka, Edga akaongeza kusema "Utakuwa unajiuliza ni kwanini na mimi niliamua kuungana nao"
"Ndio kwa sababu tabia yako haiendani na tabia zao", Kayumba alikubali,na ndipo Edga aliposhusha pumzi ndefu, tayari walikuwa wamefika maskani waliketi balazani kabla hawajalala Edga akaongeza kusema "Ni simulizi ndefu sana Kayumba, tuombe Mungu hapo kesho tumalize shughuli zetu mapema ili tukifika nyumbani niweze kukusimulia. Ila kwa sasa naomba tupumzishe akili na nguvu kwa niaba ya kesho".
"Sawa usiku mwema kwako braza", aliongea Kayumba huku akijikunyata barazani tayari kwa safari ya kuutafuta usingizi. Kesho yake asubuhi palipokucha, anga karibia lote la jiji lilikuwa limetanda wingu nzito la mvu. Hali hiyo iliweza kutandabaisha kuwa wakati wote wote mvua itanyesha, Kayumba na Edga walikurupuka kutoka usingizini ghafla wakaingiwa na hofu kuhusu hali hiyo ya hewa.
"Naona hali ya hewa si rafiki", aliongea Edga.
"Ni kweli kabisa ila haiwezi kututisha, twende zetu tukausake utajiri", alijibu Kayumba. Na sasa safari ikaanza, kila mmoja alielekea kwenye kiwanja chake. Upande wa Kayumba, biashara ilikuwa ngumu siku hiyo. Hali hewa ilimpelekea madafu kutonunulika. Ilimvunja moyo ila hawakuwa tayari kukata tamaa, mikono nyuma kichwa chini jasho ndembe ndembe likiulowesha mwili wake aliuvuta mkokoteni wake mpaka mahali ambapo palikuwa na maduka mengi huku watu kadhaa wa kadha wakionekana kuingia na kutoka ilihali manyunyu ya mvua nayo yakionekana kuanza kushuka kulimwagilia vilivyo jiji. Pumzi ndefu alishusha Kayumba, akamtazama huku na kule kisha macho yake akayarudisha kwenye mkokoteni wake akaona ni heri apumzishe mwili wake kwa kuegemea pembezoni mwa mkoteni na punde si punde usingizi ukianza kumnyemelea. Lakini kabla hajasinzia, alisikia mayowe "Mwizi..mwizi.. Jamani mwizii", ilikuwa ni sauti iliyopenya vema kwenye masikio ya masaka tonge Kayumba, mara ghafla akayafumbua macho yake. Alistuka kumuua binti mrembo,akipiga mayowe akilalama kupolwa mkoba wake. Macho ya Kayumba yakatazama mbele zaidi, yakamuona kijana wa makamo akitimua mbio huku mkononi akiwa ameshika mkoba wakati huo watu wakiishia kumsindikiza kwa macho na hata wasimsaidie binti yule. Moyo wa huruma ulimuingia Kayumba, alikurupuka kutoka kwenye mkokoteni wake akamkimiza yule kibaka. Juhudi zake zilizaa matunda, Kayumba alifanikiwa kumpokonya yule kibaka mkoba alipola. Kwa tabasamu bashasha Kayumba alimkabidhi binti yule mkoba wake, binti ambaye alionekana kuwa mzuri mithili ya maraika. Alivaa hijabu nyeusi, ngozi yake ilidhilisha kuwa ni mtu kutoka ng'ambo. Binti wa kiarabu.
"Ahsante sana", aliongea mrembo yule.
"Usijali, siku nyingine kuwa makini dada yangu. Dunia imebadirika sana", alijibu Kayumba na kisha akaondoka zake kuelekea kwenye mkokoteni wake huku nyuma yule binti akimsindikiza kwa macho na mwishowe aliachia tabasamu pana ikiwa Kayumba tayari ameshaondoka zake na mkokoteni wake.
Jioni aliporejea maskani alimueleza Edga hali harisi biashara ilivyokuwa, Edga akasema "Siku zote siku huwa hazifanani Kayumba, hata sisi leo magari yalikuwa machache sana kwahiyo mizigo haikuwa mingi. Nadhani mikoani mvua itakuwa imenyesha nyingi, labda magari mengi yamekwama"
"Naam! Maana barabara zetu bwana nayo changamoto kubwa hapa nchini", Kayumba aliunga mkono. Na sasa waliekea mgahawani kupata chakula cha jioni, wakiwa njiani Kayumba alimsimulia Edga namna alivyo msaidia mwanadada pindi alipo polwa mkoba wake. Edga alifurahi sana kisha akasema "Ni jambo la heri ulilolifanya, sababu huwezi jua atakaye kusaidia hapo baadaye".
"Ni kweli kabisa lakini Edga unakumbuka jana uliniahidi nini?..", alihoji Kayumba. Edga akaguna halafu akasema "Ndio nakumbuka bila shaka ni lile suala la mimi kujiunga na kundi la Boko"
"Eeh, ulisema leo ndio utaniambia"
"Sawa Kayumba hofu ondoa, tukirudia maskani nitakupa mkasa mzima". Edga na Kayumba walifika mgahawani, walikula chakula walichonunua na hatimaye walirejea maskani huku Kayumba akiwa na shauku ya kutaka kujua ni sababu ipi iliyomfanya Edga kutumbukia kwenye kundi lile la maharamia, kundi la uharifu ambalo linaongozwa na Boko pande la baba mwanaume mwenye miraba minne. Pumzi ndefu alishusha Edga,ni simulizi ambayo inatonesha kidonda chake, lakini kwa kuwa rafiki yake wa karibu alihitaji kujua hakuwa na budi kumueleza namna ilivyo kuwa. Hivyo alipokwisha kushusha pumzi alisema. "Haya maisha yanasafari ndefu sana Kayumba. Katika tumbo la wazazi wangu, tumezaliwa wawili mimi na mdogo wangu wa kike anaitwa Sinsia. Wazazi wetu walifariki kwa ajari ya gari wakati huo mimi nina miaka kumi na mitano huku mdogo wangu akiwa na miaka kumi. Tiliishi maisha ya tabu sana pasipo kuwa na wazazi, tulinyanyaswa kadri ndugu walivyo weza. Huwezi amini Kayumba mashamba walitunyang'anya, nyumba wakauza tukakosa makazi. Na huo ndio ukawa mwanzo wa kuikosa Elimu,kwa sababu maisha yetu yalikuwa ya kutangatanga pasipo na muelekeo maalumu. Lakini miezi kadhaa mbele, kijijini kwetu alikuja aliyekuwa rafiki yake marehemu baba. Mzee yule alijiweza nikimanisha kwamba maisha yake yalikuwa si haba na siku hiyo alikuja kuhani msiba baada kutohudhuria mazishi. Bahati nzuri wakati anaingia kijijini, nilionana naye akastuka kuniona nipo katika mazingira yale ", alishusha pumzi ndefu Edga kabla hajaendelea kusema kile kilicho msibu mpaka kujiunga na kundi la Boko,machozi hayakuwa mbali na mboni za macho yake. Yalimtiririka huku Kayumba akimtazama kwa macho ya huzuni kunako giza totoro. Alikaa kimya kidogo, punde akaendelea kusimulia...
"Edga, ni wewe mtoto wa mzee Nyoni au macho yangu yanadanganya?..", Aliuliza kwa taharuki mzee huyo aliyekuwa na ukaribu na marehemu baba Edga. Mzee huyo aliitwa Ezlom.
"Ndio ni mimi", Edga alijibu wakati huo uso wake ukionyesha kubeba huzuni kubwa ndani yake.
"Sinsia naye yuko wapi?..", aliongeza kuhoji mzee Ezlom.
"Anaishi kwa mjomba, ila...",kabla Edga hajaendelea kuongea machozi yalimtoka, na ndipo mzee Ezlom alipozivuta hatua kumkaribia. Alipomfikia akasema "Edga, hebu kaza moyo. Niambie kipi kinaendelea kwa sasa tangu kifo cha wazazi wenu". Edga aliongea ukweli wote wa maisha anayoishi na mdogo wake tangu wazazi wao wafariki,hakika roho ilimuuma sana mzee Ezlom jambo ambalo lilimpelekea kuchukuwa jukumu la kwenda kuishi nao jijini Mwanza ambako ndipo yalipokuwa makazi yake huku akiwaahidi kuwasomesha nguvu zote. Mzee Ezlom aliishi mke na watoto wawili ambao wote ni wa kike, mzee huyo aliipenda sana familia yake na wote waliishi kwa furaha ila ujio wa Edga na Sinsia ghafla ulibadirisha mwenendo wa maisha. Ile furaha iliyokuwa ikitamaraki katika nyumba ya mzee Ezlom ilipotea, Edga na mdogo wake walinyanyaswa na mama mwenye nyumba, mkewe Ezlom. Sinsia alifanyishwa kazi ngumu zilizozidi umri alio nao, na pindi Edga ipokwenda kumsaidia aliambulia kipigo na matusi ya kejeri. Yote hayo watoto hao walikuwa wakifanyiwa baada mzee Ezlom kusafiri nje ya nchi.
"Kayumba hiyo hali iliweza kuniumiza sana, nilimpenda sana mdogo wangu na bado nampenda. Yale yote aliyokuwa akifanyiwa mimi roho ilikuwa inaniuma lakini nilimpa moyo nikiamini yale ni mapito na ipo siku yatakwisha..",alisema Edga kwa uchungu huku akipandisha kamasi jepesi,punde aliendelea kukumbuka.
Jioni moja, familia ya mzee Ezlom ilitoka kuelekea kwenye matembezi, nyumbani wakiwacha Edga na Sinsia wakilinda nyumba huku.
" Kaka Edga, maisha haya tutaishi mpaka lini?..", aliuliza Sinsia kwa sauti ya chini iliyojaa huzuni ndani yake.
"Naona bora nirudi kijijini kwa mjomba kuliko kuendelea kunyanyasika hivi", aliongeza kusema Sinsia, na safari hiyo machozi yalionekana kutiririka kunako mashavu yake. Edga alishusha pumzi ndefu, alijaribu kuyazuia machozi ila alishindwa naye hivyo hivyo yalimtoka wakati huo huo akasema "Ukweli sipendi kusikia habari ya kurudi kijiji kwa mjomba, maisha ya kule heri ya hapa hapa. Cha muhimu mdogo wangu, vumilia baba akirudi tutamueleza kila kitu na tutaishi kwa amani"
"Amani gani kaka?..", Sinsia aling'aka kisha akasema "Siku yoyote naondoka ndani ya nyumba hii, mimi najua baba yangu amefariki na huyo unayemsubiri ni baba yako wewe". Kwisha kusema Sinsia akaingia chumbani.
"Na hiyo ndiyo ilikuwa siku yangu ya mwisho kuonana na kuongea na mdogo wangu,anaitwa Sinsia. Alitoroka nyumbani hatukujua ni wapi kaelekea,siku hiyo sikuwa na furaha ,kwani sikujua huko alipo u hali gani lakini baadaye mtu mmoja aliiambia kwamba ameuona Sinsia akiwa ndani ya basi liendalo Dar es salaam. Hofu ilizidi kutanda, sikuwa tayari kukaa mbali na mdogo wangu,ndani ya moyo wangu nikala kiapo lazima nimfuate Dar. Lakini niliwaza nitapat aje nauli?.. ", Edga alisimulia huku Kayumba akiwa kimya akimsikiliza rafiki yake. Edga akiendelea kukumbuka.
Anaonekana Edga akiwa chumbani amelala, ghafla mlango wa chumba chake unagongwa. Hima anakurupuka, sauti inasikika ikisema" We mwanaharamu unalala mpaka sahizi!? Hii nyumba ya baba yako?.. ", maneno hayo alikuwa akiyatamka mkewe mzee Ezlom, aliyaongea kwa sauti ya juu.
" Samahani mama, uchovu ndio umepelekea kuchelewa kuamka ", alijibu Edga kwa sauti ya upole. Mwanamke huyo alimtazama kwa hasira kisha akaongeza kusema" Natoka na mabinti zangu, naomba maua yale yote uyamwagilie, madirisha yafute vumbi nikirudi nikute kila kitu kipo safi "
" Sawa mama ", alikubali Edga kisha akarejea kitandani alijitupa mithili ya mzigo huku mawazo yake yote yakifikifia kuondoka. Mlinzi wa nyumba hiyo alipofunga geti, Edga tayari alikuwa nje akiishuhudia gari ndogo iliyobeba familia ya mzee Ezlom ikiishia. Haraka sana Edga alirudi ndani, moja kwa moja alijitupa kwenye sofa sebuleni,ghafla macho yake yakatazama mahali kilipo chumba cha mzee Ezlom, Edga akagundua kuwa chumba kipo wazi.
"Khaa, inamaana huyu mama kasahau kufunga chumba?..", alijuliza Edga na kisha akanyanyuka, kazipiga hatua za pole pole kukisogelea chumba hicho. Alipokikaribia alizama ndani zaidi, akafungua droo pole pole huku akiwa na wingi wa hofu. Punde alistuka, alichokiona ndani ya droo hakuweza kukuamini palikuwa na pesa nyingi. Lakini wakati akiwa kwenye hali hiyo ya taharuki, mara ghafla.....
.
No comments:
Post a Comment