Na alipoingia kitendo cha kwanza kilikuwa ni
kumshika mjukuu wake huyo.
Ila alipatwa na mshangao kuona mjukuu wake
huyo kuwa mweupe sana na macho madogo
utafikiri ni mtoto wa kichina yani kamavile kazaliwa
na mzazi mwenye asili ya China.
Sakina alimshika yule mtoto huku maswali mengi akijiuliza kwenye akili yake na kukosa jibu ila hakuweza kuhoji chochote ukizingatia pale ni hospitali.
Kisha baada ya muda kidogo akamrudisha mtoto mikononi mwa wengine.
Muda kidogo wakasogea Sabrina na mama yake pale kumsalimia Dorry.
Na badae wote kutakiwa kwani Dorry naye alipewa ruhusa ya kurudi nyumbani na hapakuwa na namna nyingine zaidi ya Dorry kuongozana na Sakina ili kuelekea nyumbani kwake kwani asingeweza kwenda kwao ukizingatia mama yake ambaye ndio angemuhudumia ndiye alikuwa mgonjwa.
Wakarudi nyumbani sasa huku Sakina akiwaandalia vizuri mazingira ya chumba ili aweze kukaa humo na mtoto huku akili yake ikijiuliza maswali mengi sana juu ya muonekano wa huyu mtoto kwani hawakufanana nae hata kidogo.
Kuna muda mashaka yalimjaa sana hadi mama wa Sabrina akatambua hilo kwa Sakina na kumuita pembeni,
"Mwanangu, usiwe na mashaka kiasi hicho. Utashindwa kumuhudumia mtoto ipasavyo, ni kweli hamfanani nae lakini huwezi jua. Huenda bado ni damu yenu"
Sakina akaitikia kishingo upande kisha akaendelea kumuhudumia mkwe wake.
Kesho yake baada ya maziko ya Rose, Fredy alipita tena nyumbani kwakina Sabrina na kumkuta Sabrina na mama yake.
Alikaa pale na kuanza kuwasimulia khabari za ule msiba,
"Ule msiba ilikuwa khatari jamani, mvua imetunyeshea makaburini hadi tumekoma. Na yote, nilimuona mumeo Sam. Jamaa ana moyo sana yule, Mungu ambariki"
"Alifanyaje kwani?"
Akaulizwa swali na mama Sabrina ingawa alipenda hilo swali aulizwe na Sabrina mwenyewe,
"Alijitolea kumchukua Neema akiwa amelowa chapachapa, ila alivyoondoka nae tu na mvua ikakatika. Kwakweli ilikuwa khatari jamani, aliyemroga yule dada marehemu na alaaniwe miaka yote"
"Kheee kumbe karogwa?"
"Ndio karogwa, kuna tetesi nimesikia pale msibani eti sijui alitembea na mume wa mtu, sasa mwenye mume ndio kamroga ndiomana amekufa gafla."
Sabrina na mama yake wakasikitika sana juu ya hilo.
Kisha Fredy akaingizia khabari zingine za kwanini Sabrina haishi na mumewe ilihali mumewe yupo.
"Yani mama, ningekuwa mimi ndio nimepata hiyo bahati ya kumuoa huyu binti yako, hata kama angekuwa na tatizo gani bado ningeendelea kuwa nae karibu tu yani mtu kupoteza kumbukumbu tu ndio kuishi nae mbali mbali?"
"Aliyekwambia kuwa wanaishi mbali mbali ni nani?"
"Kuna yule ndugu yangu Francis aliniambia kuwa Sabrina anaumwa, hana kumbukumbu tena. Kuna siku nikakutana na Sam na kumuuliza kuhusu Sabrina naye akaniambia kuwa anaumwa na yupo kwao. Ndiomana jana nikapita kwanza hapa"
"Kwahiyo ulipita kuhakikisha tu?"
"Ndio, kuhakikisha na kumuonyesha Sabrina kuwa mimi ni mwanaume pekee ambaye ningekuwa bora kwake"
Mama Sabrina akatabasamu na kumuuliza,
"Kwa kazi gani unayofanya?"
"Naendesha bodaboda"
"Sasa maisha ya bodaboda kweli ungeweza kumuhudumia mwanangu wewe?"
"Jamani mama usinidharau, mapenzi ya kweli si pesa bali ni upendo uliopo baina ya watu"
"Aah nakutania tu"
Fredy aliamua kuaga na kuondoka zake ila kule kuambiwa kuwa na bodaboda angemlisha nini Sabrina kulimuumiza sana ingawa mama Sabrina alibaki akicheka tu.
Sabrina naye alimtazama mama yake na kumuuliza,
"Mbona umefurahi sana juu ya huyu mtu?"
"Alikupenda sana huyu kijana hadi nilikuwa namsikitikia"
"Na yule wa siku ile je?"
"Naye alikupenda sana mwanangu, yani hawa vijana wamekupenda balaa"
"Na mume wangu je?"
"Naye alikuwa anakupenda sana, yani huyo ndio sijui kapatwa na shetani gani? Mtu kakuoa vizuri ila leo sijui kavamiwa na nini?"
"Kwahiyo sasa hivi hakuna anayenipenda tena?"
"Lazima watakuwepo tu mwanangu, naomba tuachane na khabari hizo"
Mama wa Sabrina akaenda kushughulika na mambo mengine huku akimuacha bintiye akijiuliza maswali mwenyewe na kujijibu mwenyewe.
Ilipita wiki sasa na kumfanya Sakina akimshangaa mjukuu wake kuzidi kufanana na watoto wa kichina.
Ikabidi siku hiyo amuulize vizuri mkwe wake Dorry.
"Dorry mwanangu, mbona huyu mjukuu wangu anafanana na wachina?"
"Kumbe na wewe mama umeshangaa eeh! Basi hata mie nilishangaa hivyo hivyo, juzi nikampigia simu mamdogo na kuongea nae kumbe babu yetu alikuwa hivi hivi"
Sakina akashangaa sana na kuuliza,
"Na huyo babu yuko wapi saivi?"
"Alishakufa, ila mama kaniambia kuwa atabadilika tu huyu mtoto badae eti hadi achangamke"
Sakina akajikuta akichukia sana moyoni ukizingatia anaona kabisa akidanganywa.
Akajisemea moyoni mwake kumpa mwezi huyu Dorry ili arudi kwao kisha atakuja kukubaliana na mwanae akirudi kwani aliona akidanganywa kabisa.
Kipindi hiki ni huyu Aisha pekee aliyekaa na Neema nyumbani kwake kwani hakupenda kumuona na ule upweke alionao kwa kipindi kile kwani muda mwingi Neema alionekana kunyong'onyea kupita maelezo ya kawaida.
Siku hiyo akafika tena Sam kumsalimia Neema na kumkuta pale akiwa amelala sebleni huku Aisha akiwa pembeni kama kumliwaza.
Sam aliwasalimia pale ila Neema hakutaka kuitikia kabisa ila alimwambia neno moja tu,
"Sam, nakuomba uende"
Sam bado alisimama pale pale akimuangalia Neema kwani alikuwa akimpenda sana, ila Neema alikuwa akitokwa na machozi tu ambayo yaliumiza sana moyo wa Sam kwani alijisikia vibaya kila alipotazama chozi la Neema.
Sam akajikuta akiinama pale Neema alipo na kumbusu kwenye paji la uso,
"Sam nakuomba uende"
Neema akawa analia kwa staili ya uchungu sana na kumfanya Aisha aingilie kati kwa kumsihi Sam aondoke hadi akatoka nae nje kabisa ambapo Sam alionekana kuwa na uchungu sana.
Sam akamwambia Aisha,
"Naelewa maumivu ya Neema, najua jinsi gani anateseka"
Kisha akatoa pesa na kumkabidhi Aisha endapo kutakuwa na hitaji lolote kwa Neema.
Aisha aliporudi ndani akamkabidhi zile pesa Neema ambapo zilimtia uchungu zaidi na kumfanya akumbuke mambo yale ya nyuma.
Sakina akiwa nyumbani kwake, akapigiwa simu na mwanae Jeff, kisha wakasalimiana nae ila leo alimueleza akiwa amepooza sana,
"Mkeo kajifungua huku Jeff"
"Mke? Mama sina mke huko mbona huwa hunielewi"
"Kwahiyo huyu Dorry ni nani yako?"
"Mama, nikujibu mara ngapi kama sina utambuzi na huyo Dorry? Mi sio mtu wangu huyo mama, kwani ni mambo gani anakudanganya huyo?"
"Subiri uje ujionee mwenyewe nisije nikasema mengi na kuonekana mbaya bure"
"Mama, huyo Dorry asikudanganye lolote. Hata hivyo narudi, na ole nimkute huyo Dorry hapo nyumbani"
"Ni siku gani unarudi?"
"Sitaweza kusema ni siku gani ila wewe ujue kuwa narudi mama"
Sakina alipomaliza kuongea na mwanae akamuangalia Dorry aliyekuwa ametulia akimnyonyesha mwanae na kumfanya Sakina ajiulize kuwa kwanini Dorry anaonekana kuwa jasiri na kujiamini bila wasiwasi, akahisi kuwa huenda ikawa kweli yule ni mtoto wa Jeff ingawa alikuwa na mashaka sana juu ya swala hilo.
Sakina aliondoka pale kwake na kwenda kwakina Sabrina kwa lengo la kumsalimia Sabrina ila lengo lake kubwa ilikuwa ni kutoa dukuduku lake.
Alifika na kumkuta Sabrina akiwa na mama yake pale nyumbani.
Baada ya maongezi mawili matatu alianza kuwaeleza anavyomuona mjukuu wake,
"Jamani mi nina mashaka kabisa kuwa yule sio mtoto wa mwanangu"
Mama Sabrina akacheka na kuuliza,
"Kwanini uwe na mashaka na mjukuu wako jamani?"
"Kwakweli simuelewi, mjukuu ni mchina kabisa yani macho na kila kitu itakuwaje awe mjukuu wangu?"
"Siri ya mtoto anayo mama, ukiona mwanao kakubali basi na wewe ukubali tu mwanangu"
"Haiwezekani mama, yani nishapanga hapa Jeff akirudi tu lazima wakapime damu ingawa huyo Jeff anakataa kabisa kuhusu kuwa na mahusiano na Dorry ila mimi tu ndio nilikuwa nang'ang'aniza toka mwanzo kuwa Dorry ndio mkwe wangu ukizingatia sijawahi kumfahamu mkwe wangu kwa Jeff."
Sabrina akaanza kucheka na kufanya wamshangae, kisha Sakina akamuuliza,
"Au wewe kuna mkwe wetu mwingine unayemfahamu?"
"Huyo mwanao mwenyewe simfahamu. Sasa huyo mkweo mwingine nitamfahamia wapi?"
"Lakini nakumbuka kama uliwahi kuniambiaga kuwa Jeff alizaa na mtoto wa mwanajeshi, nilikufatilia unionyeshe mjukuu wangu huyo lakini sikufanikiwa sababu ulikuwa ukinipa vitisho tu vya mwanajeshi ila sasa nasubiri upone ili ukanionyeshe yote ya zamani"
Sabrina bado alicheka kwani hakuwa na kumbukumbu wala utambuzi wa chochote kilichokuwa kikizungumziwa pale.
Sam alikuwa akijutia sana kwani kwa hali aliyokuwa nayo Neema aliona wazi kuwa kwa vyovyote vile atakufa tu.
Ingawa Neema ndio alikuwa mwanamke msiri sana kupita wote aliokutana nao hata akashangaa kuwa ule ujasiri na usiri Neema anauwezaje, alitamani ampate mtu wa kuweza kumfanya Neema arudi katika hali yake ya kawaida ila je atampatia wapi mtu huyo kwa ugonjwa wa ajabu kama ule?
Sam aliumiza sana kichwa chake bila matumaini yoyote yale.
Siku hiyo Aisha alitoka pale kwa Neema na kwenda kumtafutia matunda, kwa bahati akakutana na rafiki yake ambaye hawakuonana nae kwa muda mrefu sana.
Alifurahi sana kukutana na rafiki yake huyo,
"Jamani Sia, hata siamini kama nimekuona leo"
Wakaongea mengi sana na kubadilishana namba za simu.
Wakati wanaongea, kuna gari ikasimama mbele yao na aliyeshuka alikuwa ni Sam ambapo alisimama ili aweze kumsalimia Aisha.
Wakasalimiana pale na kisha Aisha kumtambulisha Sam kwa yule rafiki yake Sia.
"Yani huyu ni rafiki yangu sana ila tulipotezana kidogo tu"
Sam akaona ni vyema kama akiwapandisha kwenye gari yake na kuwarudisha, wakati huo Sia nae akajitetea
"Ila mie kwetu ni mbali"
"Hakuna shida nitakupele ka, tutaenda kwanza anapokaa huyu Aisha kwasasa halafu na wewe nitakupeleka"
Wakafurahi pale kwani atakuwa amewapunguzia mambo ya nauli.
Sam aliondoka nao pale na kwenda moja kwa moja kwa Neema ili Aisha amuonyeshe rafiki yake alipo kwasasa.
"Basi haina shida, nitakuja kesho maana leo kama nilivyokwambia inabidi nimuwahi mtu nyumbani"
Sam naye hakutaka kushuka kwavile alishafika kabla na Neema kumfukuza.
Ila alitoa pesa na kumkabidhi Aisha kisha akamwambia,
"Tafadhari utampatia Neema maana hataki nikimpa mimi kabisa"
Kisha wakaagana pale na kuanza safari ya kumpeleka Sia na kujikuta wakiongea mambo mengi sana hadi pale Sia alipofika anapoelekea.
"Nashukuru sana kwa ukarimu wako kaka"
"Usijali kitu"
"Mmh sawa, basi huu ndio mwanzo mzuri wa kufahamiana. Unaweza kunipatia namba zako?"
"Hakuna tatizo"
Kisha Sam akamtajia Sia namba zake pale na kuagana nae kisha yeye kwenda kuendelea na shughuli zake zingine kwa wakati huo.
Sia alijiona wazi kuvutiwa na ule ukarimu wa Sam, ila kikubwa zaidi ni kule kumuona kuwa ni mwanaume mwenye uwezo na pesa zake na kumfanya afikirie swala la kuwa naye karibu ili aweze kumfahamu kwa undani zaidi kwani mawazo yake yalishagota juu ya huyu Sam.
Sakina alikuwa akisubiri kwa hamu ujio wa mwanae kwani muonekano huu wa mjukuu wake haukumuingia akilini kabisa, na kule kujiamini kwa Dorry kulimfanya ashindwe kumuelewa kabisa.
Dorry hakuwa na uoga wowote kwa kipindi hiki, hakuhofia kuwa Jeff anarudi wala nini, hakuwa na mashaka juu ya mtoto ingawa alijua wazi kuwa mama mkwe wake kashagundua mchezo kamili ila yeye hakutaka kujitia wasiwasi wowote na alijiamini kupita maelezo.
Sakina alikuwa akijiongelea tu,
"Yani hata kama watu husema kuwa kitanda hakizai haramu, ila safari hii kimezaa jamani mmh huyu si damu yetu ila navumilia tu"
Dorry alisikia ila akajifanya kamavile hajasikia chochote kwani aliendelea na mambo mengine kama kawaida, kitendo hicho kilimfanya Sakina aombe usiku na mchana kuwa mwanae arudi.
Sabrina akiwa amejichokea na ile mimba yake, alikuwa amekaa kwenye mkeka huku akitafakari mambo yake na kuona kama anaweza kurudisha kumbukumbu zake.
Akamuona mtu akija huku akitabasamu sana, huyu mtu alionyesha kumfahamu vizuri Sabrina ingawa yeye alikuwa akimshangaa tu.
"Unanishangaa jamani, mimi ni Jeff"
Kisha akamkumbatia Sabrina ila Sabrina bado alimshangaa na kufanya Jeff ajaribu kujieleza kwani alikuja kwa kushtukiza tena bila taarifa kamili.
Ila kabla Jeff hajajieleza, akashangaa kumuona Sabrina akianguka na kuanza kutapatapa.
Itaendelea
No comments:
Post a Comment