Sabrina akaona itakuwa shida na kuamua kuinuka
ili akamlaze mtoto kwanza ila alipofika chumbani
akashangaa alichokiona na kuamua kuwaita Sam
na Jeff nao walishangaa walichokiona kwani
walimuona mtoto mwingine mdogo kama mtoto
wao akiwa amelala kitandani.
Walijikuta wakiguna kwa pamoja, Jeff akawa wa kwanza kuongea,
"Mmh haya majanga jamani"
"Sasa tufanyaje?"
"Huyu mtu hawezi kutuacha jamani mpaka apate anachotaka"
Sabrina alijikuta akiyasema hayo kwani hakuelewa kitu, Jeff naye akaongezea kuwa bora waondoke tu eneo lile.
Pia akaongezea kuwa,
"Tena kabla ya kuondoka tujue kwanza mtoto wetu ni yupi"
"Hapana, mi najua wangu ni huyu wa mikononi wa pale kitandani simtambui jamani"
"Ila mkumbuke yule mganga anatuchezea akili humu ndani, tuondoke tukiwa na uhakika kabisa wa mtoto"
"Uhakika ninao, mwanangu ni huyu wa mikononi"
"Basi kama una uhakika tutokeni, tuondokeni hapa kwani naona si sehemu sahihi tena."
Wakakubaliana hivyo na kutoka nje bila ya kujua kuwa waelekee wapi kwanza.
Ila walipofika mlangoni tu, Sabrina akajihisi maumivu ya moyo dhidi ya mtoto aliyemuacha ndani na tena akajihisi mikoni ikichoka sana kwa yule mtoto aliyembeba kwani alikuwa na uzito usio wa kawaida.
Akawasimamisha Sam na Jeff kisha akampa Sam yule mtoto ambebe,
"Hebu jaribu na wewe kumbeba mtoto huyu"
Sam akamchukua na kushangaa,
"Mbona kawa mzito sana?"
Wakajikuta wakiguna na kubaki na mshangao.
Jeff akaona ni bora wakamchukue yule mtoto wa ndani kwani huyu wa mikononi aliwapa mashaka tayari.
Akaingia na kutoka na yule mtoto.
Sam alipoona Jeff kashatoka na yule mtoto yeye akampa yule mtoto Sabrina na kumwambia kuwa akamlaze ndani, Sabrina nae hakusita na kwenda kumlaza.
Wakati Sabrina anaenda kumlaza yule mtoto, Sam akamshika mkono Jeff na kuelekea nae kwenye gari, wakapanda na kuanza kulitoa gari nje kwanza ili wakamsubirie Sabrina nje.
Sam aliona Sabrina kakawia kidogo na kuamua kumfata ndani.
Alipoingia ndani alimuona yule mtoto akiwa amemng'ang'ania Sabrina yani alikuwa hataki kuachilia nguo ya Sabrina ili aondoke.
Sam akaona ule mtihani sasa ila akapata wazo la haraka haraka na kumpa wazo hilo Sabrina kuwa avue hata blauzi yake na kumuachia yule mtoto kisha yeye aweze kukimbia ila wakati anamalizia kutoa ile blauzi alishtukia akizabwa kibao cha hali ya juu na yule mtoto hadi kupatwa na kizunguzungu na kufikia hatua ya kutaka kudondoka ndio hapo ambapo Sam akawahi na kumdaka kisha kutoka naye nje huku akisikilizia maumivu ya kibao kile.
Moja kwa moja Sam alienda na Sabrina hadi kwenye gari na kupanda.
Sabrina alijishika shavu tu kusikilizia maumivu yale na kusahau kama mwilini amebakiwa na sidiria tu kwavile blauzi ilibaki ndani.
Sam alimpa pole pale huku akiondoa gari, Jeff alijikuta akisikitika tu
"Duh ya leo kali, sasa tunaenda wapi jamani?"
"Nyie tulieni tu, mtaona tutakapoenda"
Ndipo alipomtazama Sabrina na kugundua kuwa amebakiwa na sidiria tu,
"Ngoja nisimame hapo kwenye duka la nguo nikuchukulie mtandio"
Sam akasimamisha gari na kushuka.
Sabrina nae akajiangalia na kujicheka,
"Hii kweli balaa, alikuwa akiongea huku akitetemeka kwani bado ule uoga wa mwanzo alikuwa nao.
Jeff alimpa pole tu huku akimuangalia mtoto aliyekuwa mikononi mwake kwa muda huo.
Sam naye aliporudi alikuja na blauzi pamoja na mtandio ambapo Sabrina aliona ni bora avae tu ile blauzi kwanza kisha safari ikaendelea.
Mlinzi wa Sam alikuwa akishangaa tu kile kilichoendelea pale kwani hata yeye hakuelewa kitu hususani kile kitendo cha kumuona Sabrina akitoka ndani na sidiria tu ndio kilimpa mashaka zaidi na kumfanya ajiulize kuwa kuna nini ndani.
Akatamani kwenda kuangalia kuwa kuna nini ila akapatwa na mashaka kidogo kwani alihofia kuwa hicho kitu kinaweza kikamkimbiza na yeye pia hata kumkosesha amani ya kuendelea kulinda hapo kwahiyo akaona vyema abakie pale nje.
Muda kidogo akawasili yule mzee na kuwa kama akiwaulizia wakina Sam tena,
"Hawapo, wameondoka tena muda sio mrefu"
"Wameenda wapi sasa?"
"Kwakweli sijui maana sijaagwa na hapa wameondoka hai hai kamavile kuna kitu kimewapata"
"Hivi huyu kijana kwanini ni mbishi kiasi hiki? Hajui kama mimi naweza kufanya lolote? Hajui kama mimi ni mtu mbaya kuliko anavyofikiria? Mwambie nitamuharibu, nitamuhangamiza kama hanijui vizuri"
"Usimfanyie hivyo mzee wangu, si unajua tena ndio ajira hizi na sisi tunategemea hapa! Familia zinatutegemea wengine kwa kazi hii hii sasa ukimuangamiza tutaishije wengine hapa jamani?"
"Tatizo lake ana kiburi sana, na kiburi chake ndio kitakachomponza. Sasa natoa nafasi ya mwisho na ya upendeleo kwake, nitakupa namba zangu. Yani akirudi tu hapa nipigie na umwambie anisubiri hapa nje akikiuka nitajua mimi cha kufanya"
Kisha yule mzee akamtajia mlinzi wa Sam namba zake naye akaziandika na kuahidi kufanya kile alichoambiwa kisha yule mzee akaondoka zake.
Sam alitaka kuwapeleka mahali pengine ila akasita kidogo na kuona kuwa ni vyema waelekee nyumbani kwakina Sabrina kwanza kwani hata muda nao ulikuwa umeenda.
Walimkuta mama Sabrina naye akawakaribisha ingawa hakuwatarajia.
Sabrina akaona ni vyema amueleze mama yake kwa kifupi kilichotokea ili asiwe na maswali mengi.
"Mmh poleni, hata hivyo mna moyo jamani. Mbona ni mambo ya kishirikina hayo na yanatisha balaa"
"Yani mama wee acha tu hata sijui huyu mzee anataka nini"
Sam akajibu kawaida kabisa,
"Nyie muacheni tu nitamkomesha najua na yeye hanijui vizuri mimi. Yule mganga ni kichaa kwakweli, kwake aende mtu mwingine halafu aje kutusumbua sisi wakati ameshaturoga wee hadi tukafanya mambo ya ajabu ila nitamkomesha"
Hakuna aliyemuelewa Sam kuwa atamkomesha vipi yule mganga zaidi ya kumsikia kuwa atamkomesha.
"Ila leo itabidi nilale hapa maana sitaweza kwenda kulala kwangu kwa mauzauza yale"
"Hakuna tatizo mkwe wangu hapa vyumba vipo vya kutosha tu kwahiyo usiwe na wasiwasi."
Sam akamshukuru mkwe wake pale kwani mama huyu wa Sabrina hakuwa na tatizo lolote dhidi ya Sam kama ambavyo mumewe alikuwa akimchukia Sam kwa kipindi hicho na uzuri ni kwamba mara zote ambazo Sam amelala pale basi baba Sabrina hayupo na hiyo ikawa ni salama kwake.
Kwavile muda nao ulienda kidogo, Jeff akawaaga na kuondoka akielekea kwao ila njia nzima alikuwa akimuwaza mwanae na yale majanga ya Sam,
"Eeh Mungu nilindie mwanangu, laiti kama ningekuwa na uwezo ningemchukua ili niishi nae mwenyewe"
Aliongea maneno hayo wakati tayari amefika kwao na bila kujua kuwa mama yake amemsikia wakati akitamka hayo.
Alipoingia ndani tu mama yake akamuuliza,
"Jeff kumbe una mtoto! Sasa kwanini hutaki kuniambia mwanangu?"
Jeff akakaa kwenye kochi na kusema neno kwa mama yake,
"Hata nikikwambia huwezi kunielewa mama, kwani huwezi tambua ni jinsi gani nampenda yule mwanamke"
Sakina akamuuliza mwanae kwa mshangao,
"Mwanamke gani? Sabrina?"
Jeff akashtuka huku akitamani kumwambia mama yake kuwa ndio huyo huyo ila akasita kidogo kwani aliona wazi kuwa mambo hayajatulia kwahiyo mama yake angeweza kufanya hata varangati.
Ni hapo naye akajifanya amemshangaa mama yake,
"Kheee Sabrina!! Sabrina gani mama?"
"Kwani humjui? Si yule mama yako mdogo"
Jeff akacheka kidogo kama kuziba maana kwa mama yake,
"Jamani mama, si ushasema ni mama mdogo jamani sasa ndio inakuwaje hapo?"
"Aah basi tuachane na hayo"
Jeff akainuka na kuelekea chumbani kwake huku akimuachia maswali lukuki mama yake kwani bado hakumuelewa mwanae.
Usiku wakiwa wamelala, Sakina akajiwa na ndoto ambayo ilimshtua sana.
Kwenye ndoto ile alimuona Sabrina akiwa amesimama huku kamshikilia yule mwanae mikononi na kumwambia Sakina
"Hivi wewe Sakina lini utakubali kuwa huyu niliyemshika ni mjukuu wako? Lini utaamini kuwa mimi na Jeff tunapendana? Hivi ni nani kakwambia kuwa mapenzi yanachagua? Penzi ni kama jani huota popote. Naomba ukubali tu na umshike mjukuu wako"
Sabrina akawa kama anampa Sakina yule mtoto ila kabla hajampokea akatokea Sam na kumwambia,
"Ole wako umpokee huyo mtoto, najua hunijui vizuri. Nitakufanya kitu mbaya"
Ikabidi asimpokee ila akamuona Sabrina akianguka na yule mtoto mikononi ndio hapo aliposhtuka kutoka usingizini na kujikuta akikaa huku akijiuliza kuwa ile ndoto inamaana gani katika maisha yake.
Akajikuta akiwaza kuwa asubuhi na mapema aende kwakina Sabrina.
Kulipokucha tu, Sakina aliamka na kuoga kisha akatoka na kuelekea kwakina Sabrina.
Alipofika alimkuta Sabrina akiwa amesimama huku kambeba mtoto mkononi na Sam akiwa mbele yake kanakwamba kuna kitu wanazungumza pale nje.
Alisogea na kuwasalimia ambapo Sabrina alimkaribisha vizuri tu Sakina na wakasalimiana nae vizuri kabisa,
"Karibu ndani Dada, na mbona asubuhi asubuhi hivyo?"
"Aah nimekuja kuwasalimia tu"
Kisha akasogea kamavile anahitaji kumshika mtoto ambapo Sabrina alimkabidhi mtoto yule kisha akaingia nae ndani na kuwaacha Sabrina na Sam pale nje.
Sabrina alikuwa anataka Sam amueleze atakachoenda kufanya na yule mzee,
"Usiwe na mashaka Sabrina, mi huwa sikosei nikipanga jambo ingawa kwako nilikosea"
"Ila uwe makini Sam, kwani kumbuka kwamba yule mzee ni mganga wa kienyeji na anaweza kukudhuru akitaka. We fikiria tu kama ndani ameweza kutufanyia vituko kiasi kile sasa ukimfata si ndio balaa"
"Usijali Sabrina, mi naenda kumpa pesa yule mzee na hatotusumbua tena"
"Ila zikiisha atasumbua tena tu, si unajua pesa ni mwanaharamu? Na hata siku moja mtu haridhiki na pesa hata awe bilionea"
"Nimekwambia usijali, yule mzee shida yake ni pesa na mimi nitaenda kumpa pesa ili asinisumbue tena"
Sabrina akaona ni vyema amuache akafanye hiko anachoona yeye kuwa ndio sahii kwake na kuagana nae pale.
"Nitakuja badae halafu tutamaliza mazungumzo yetu na muhafaka wetu"
"Sawa hakuna shida, kwaheri"
Sam alienda kupanda gari yake na kuondoka kisha Sabrina akarudi ndani kwao.
Sabrina akafika mlangoni na kusimama kwa muda kwanza kwani alikuwa akimuangalia Sakina jinsi anavyomuangalia mtoto wake akatabasamu kwani alijua wazi kuwa Sakina kuna kitu anakihisi kuhusu yule mtoto ila anashindwa kumuuliza.
Muda kidogo Sakina nae akajihisi kama akiangaliwa na kujikuta akiinua kichwa na yeye halafu macho yake yakagongana na Sabrina na kuliona lile tabasamu la Sabrina na kujikuta akimuuliza swali ambalo hata hakupanga kumuuliza kwa muda huo,
"Hivi huyu mtoto anaitwa nani tena?"
"Anaitwa Sam, niliamua kumpa jina la baba yake"
"Aah umefanya vizuri mwaya"
Huku akiendelea kumuangalia mtoto yule na kumkadilia.
Sabrina akapita pale na kuelekea chumbani kwake huku akimuacha Sakina pale sebleni na yule mtoto.
Sakina alitafakari kidogo na kukumbuka hospitali maneno yale ya manesi wakati Sabrina anajifungua.
Akakumbuka na kauli ya Jeff ya kusema kwamba aliamua kujifanyisha ni mume wa Sabrina ili kuokoa maisha ya Sabrina.
Akamtazama na mtoto sasa anavyofanana na Jeff na kujiuliza kuwa kwanini wanamficha huku akifikiria pia kuwa Sabrina aliwezaje kumkubali mtoto mdogo kama Jeff? Yani Sakina alijihisi akili yake kutokujisoma vizuri kabisa.
Muda kidogo Jeff nae akafika pale kwakina Sabrina kwani hakujua kama mama yake nae yuko pale.
"Mama, kumbe umekuja huku?"
"Ndio, mbona na wewe umekuja?"
"Mie nimekuja kuwasalimia mama"
" Mmh na mimi nimekuja kusalimia pia"
Yule mtoto nae aliposikia tu sauti ya Jeff akageuza shingo na kumuangalia na kuanza kama kulia.
Ikabidi Jeff amchukue mtoto huyo na kumbeba yeye, na muda kidogo akalala akiwa kwenye mikono ya Jeff na kumfanya Sakina azidi kupatwa na mashaka dhidi ya Jeff na Sabrina ila ndio hivyo hakuwa na uhakika kwa anachokiwaza.
Sam alienda moja kwa moja mpaka nyumbani kwake na kumkuta yule mlinzi nje ambaye alimueleza kila kitu kuhusu yule mzee.
"Kwahiyo huyo mzee ndio kakuachia maagizo hayo Omary?"
"Ndio alivyoniambia"
"Basi mpigie simu aje, me nitamsubiria"
Yule mlinzi wa Sam akachukua simu na kumpigia yule mzee na muda kidogo alikuwa amefika eneo lile kanakwamba hakuwa mbali na eneo lile.
Sam akasalimiana na yule mzee kisha akaingia nae ndani ya geti sasa.
Muda kidogo yule mlinzi wa Sam akasikia mlio wa risasi na kumfanya nae aingie ndani ya geti, akashangaa kumuona yule mzee chini huku damu ikiwa imetapakaa eneo lile.
Itaendelea
No comments:
Post a Comment