TAMBUA kuanzia leo kwamba mapenzi ni safari; inayohitaji tafakuri na mazingatio. Kusafiri bila kujua uwendako ni balaa kubwa; lakini hata kuitegemea safari ikupe unachokihitaji ni kujiongopea. Wengi wetu tunaanza safari za mapenzi kwa kuamini tukiwa na ‘kiu’ tutapata maji safarini na kwamba mahitaji yote tunayotaka tutayapata tuendako. Ikiwa ni mapenzi, tutayapata kwa huyo mwenza tunayeelekea kwake na hapo tunasita kujiuliza asipokuwa navyo tunavyohitaji tutafanyaje?
Mara zote kabla safari haijakulipa, lazima ujilipe mwenyewe; ndiyo maana wasafiri hubeba maji na chakula ingawa huko waendako kuna maji na vyakula vizuri watapata. Kwa maana hiyo, kila unapofikiria kuanzisha safari ya mapenzi au kumdatisha mpenzi uliye naye, hakikisha humtegemei yeye akupe mahitaji yako yote; kuna wakati wewe utatakiwa kutoa ulichobeba ili safari yenu ya mapenzi iendelee.
Mapenzi yanahitaji kujitolea; je, unayo akiba ya kujitolea kwa mwenza wako hata kabla yeye hajaanza kujitoa kwako?Kumbuka kwenye safari ya mapenzi kunahitaji pia kujali, umejiandaa kuanza kumjali mwenza wako kabla hajakujali? Uko tayari kuanza kupenda kabla ya kupendwa? Maana kadiri unavyotimiza matakwa ya safari ndivyo unavyousogelea mwisho mwema ambako utakutana na maneno kama haya:
“Mwanzo sikumfikiria kama angenifaa, lakini kadiri siku zinavyokwenda nimegundua hili ndilo chaguo langu sahihi kwa sababu amenionesha upendo ambao hakuna mwanamke aliyewahi kunifanyia hivi.” Wanaume wengi wamekuwa na shuhuda za namna hii, lakini hata wanawake nao wapo ambao wamewahi kueleza namna ambavyo walianza wakiwa na upendo wa chini lakini baadaye wakajikuta wamekolea.
Hii maana yake nini? Hushuhudia umuhimu wa kila mpenzi kuwa na ‘pakeji’ ya ziada ya kuliendesha penzi kabla ya kulifikisha kwenye mwendo kasi. Tofauti na hapo kuanzisha mapenzi kwa kutegemea ‘kusaidiwa’ kwa kila kitu utajikuta kuna wakati unahitaji msaada na hupewi na mwenza wako kwa sababu hujafika safari yako.
Na kama nilivyosema, ni kweli huko uendako kwenye mapenzi kuna mazuri mengi lakini pambana kwa uwezo wako kwanza ufike safari yako ili unayoyatarajia yawe haki yako. Siyo siku ya kwanza tu kukutana na mwenza wako unalia: “Mama mgonjwa sana; unaweza kunisaidia hela kidogo ya matibabu?”
Weweee! Aliyekuambia kuwa mwenza wako ameshaanza kumuona mama yako kama mkwewe hadi amhudumie ni nani? Tabia hiyo ni sawa na kusahau maji kwenye safari halafu unafika kituo kimoja tu unataka mwenyeji wako akupe maji; atakupaje nawe hujawa mgeni wake?
Ukitaka kuyafaidi mapenzi jifunze kuigharamia safari, uwe tayari wakati mwingine kutoa ujuzi wako kumlidhisha mwenzako kimahaba, umsaidie ufundi wa kujua chochote kizuri ili kiwafae safarini na ikiwezekana toa ulichonacho ili mapenzi yenu yazidi kupaa.
Tumezaliwa na kulelewa tofauti; lini tunaweza kuwa mwili mmoja kama kila mmoja wetu hatakuwa tayari kuigharamia safari ya mapenzi? Kwenye mapenzi hakuna mtu mwenye haki ya kupewa upendo kuliko mwingine, kadiri mnavyobadilishana mapenzi ndivyo mnavyozidi kukifikia kilele cha upendo.
No comments:
Post a Comment