Nilishawahi kuzungumzia suala la baadhi ya wanaume kuwa wabahiri kwa wapenzi wao. Yaani wao kutoa pesa zao kuwafanyia ‘shopping’ wapenzi wao, kuwasaidia pale wanapokuwa na matatizo ni wagumu kuliko maelezo.
Unakuta mwanaume anapata mshahara mzuri au katika mishemishe zake anakuwa na bahati ya kupata mshiko wa kutosha lakini ukifuatilia sana utabaini ni mgumu kutoa na mpenzi wake hanufaiki chochote na kipato hicho kizuri.
Akiombwa pesa ya bando anakuwa mkali sana, akililiwa shida anaweza hata kukata mawasiliano. Jamani, labda niseme kwamba, mpenzi wako anayekupenda kwa dhati hawezi kukuchuna. Anapokulilia shida, anajua wewe ndiye mtu sahihi wa kumsaidia.
Hawezi kwenda kwa mtu wa pembeni na kuomba msaada wakati wewe upo. Hivi mpenzi wako akimlilia shida rafiki yako (shemeji yake) na akapewa wakati wewe unaweza kumsaidia utajisikiaje? Huoni aibu?
Usipokuwa wa kwanza kumfanya mpenzi wako ajisikie furaha kwenye maisha yake, unatarajia nani afanye hivyo? Sikatai huenda kazi huna na fedha inakupitia kushoto, hilo wala siyo tatizo. Kwa kuwa mpenzi wako anajua naamini ataendelea kuwa na wewe akifahamu kuwa kukosa kwako ni mipango ya Mungu.
Tatizo ni pale ambapo unazo na unakuwa mbahiri bila sababu za msingi. Huku ni kutaka kumfanya mpenzi wako ashawishike kuchepuka. Atakutana na wanaume wanaojua kumwaga pesa na wenye ushawishi mkubwa na kwa kuwa wewe humjali, atajikuta amechepuka. Tusitake yatukute hayo!
Lakini sasa wakati hilo likiwa hivyo, leo nataka kuwazungumzia baadhi ya wanawake ambao wana katabia f’lani kasikofaa. Nawazungumzia wale wanaofanya kazi zinazowaingizia kipato, hata kama siyo kikubwa kuzidi kile cha waume zao.
Ni kweli mume ana jukumu la kumfanya mkewe ajisikie furaha ya kuolewa lakini wewe mwanamke ambaye unapata pesa kwa kazi zako au mshahara, ni lini ulisema leo ngoja nimsaidie mpenzi wangu katika hili?
Yaani kwa kuwa umeolewa basi unataka kila kitu mumeo afanye, yeye ndiye anunue chakula, yeye ndiye atoe mahitaji muhimu kwa watoto, yeye akuvishe na akulishe, fedha zako wewe unafanyia nini? Ni lini ulisema leo ngoja ninunue mahitaji ya nyumbani? Ni lini ulimnunulia zawadi mpenzi wako? Mara ya mwisho ni lini kumtumia mumeo vocha?
Nasema hivyo kwa kuwa, wapo wanawake ambao wanaamini kipato chao wana haki ya kukifanyia chochote ila cha mume ndicho kinachotakiwa kutumika ipasavyo. Wapo wanawake ambao wako makini sana na mshahara wa waume zao lakini za kwao wakiulizwa wanakuwa wakali, hii siyo poa!
Mnapokuwa wapenzi au mmeoana, mnakuwa kitu kimoja. Mwenzako akiwa na shida f’lani unamsaidia pale inapobidi lakini itakuwa haileti picha nzuri kama pesa yako ni yako lakini ya mpenzi wako unaitolea macho.
No comments:
Post a Comment