ENDELEA...........
.......Safari ile sikuwa nafahamu napelekwa wapi, kwa kuwa nilikuwa sijifahamu kabisa, hii ilitokana na mwili wangu kukosa nguvu baada ya lile tukio kunitokea kwa wakati mfupi kama ule na kupotea ghafla. Ilinichukua muda sana mpaka hali yangu kurudi kutoka kwenye usingizi mzito wa nusu kifo, Nilishtuka baada ya kuhisi ubaridi mkali mwilini mwangu, ndipo nilipoangalia macho yangu baada ya kugundua kuwa sipo sehemu salama. Kilichonijulisha kuwa sipo sehemu salama ni baada ya kuzisikia kelele za watu wakicheka kwa kebehi ya aina yake.
"Niko wapi hapa mimi"
Nilijiuliza mwenyewe bila hata ya kupata jibu. Niligeuza shingo yangu sehemu mbalimbali za ile nyumba ndipo nikakutana uso kwa uso na bwana Paul. Nilishtuka sana, kwani sikutegemea kama yule mzee atanileta sehemu kama hii.
"Mnali?"
Paul alniita
Nilimuangalia tu bila kuitikia
"Unajisikiaje kuwa maeneo haya?"
Paul aliniuliza.
Pia hata hilo sikuweza kumjibu.
Sehemu hiyo walikuwepo pamoja na Manyota akiwa na Musa. Mzee yule aliyenileta alikuja huku akiwa kafungwa P.O.P Lile dude ambalo wanafungwa shingoni kama mtu yule ambae amevunjika shingo, nilipata picha kuwa yule mzee kaumia na kutokana na kile kipigo nilichompa muda uliopita kwa kuwa sikufahamu ni saa ngapi wakati huo.
"Ehee! Ameamka huyu mpuuzi?"
Aliongea huyo mzee,
"Ndio kaamka sasa ni muda wako"
Niliduwaa ndipo nilijinyoosha kidogo, viungo vyangu havikuwa na ushirikiano kwani vilitoa sauti ya kujivunjavunja pah! Pah! Pah!. Hii ilitokana na uchovu mkubwa sana ambao niliupata.
"Kijana unanishangaza sana unajifanya mwerevu kumbe umetumwa toka kuzimu huko, sasa leo tutakumaliza na kukutia Asidi kali"
"Mzee ngoja kwanza, huyu hatupaswi kumuumiza sana bado nina majukumu nae"
Aliongea paul.
"Sawa bosi tunakusikiliza"
"Sasa, Manyota na Musa nawaombeni mkachukue lile begi pale kitandani kwangu"
Manyota na Musa walinyanyuka na kwenda kuchukua lile begi ambalo Bwana Paul alilihitaji kwa muda ule, huku nyuma tulibaki watatu mimi, Mzee pamoja na bwana Paul.
"Bosi sikufichi huyu si binaadamu"
Aliongea yule mzee
"Kwa nini asiwe binaadamu?"
"Kwa sababu nimemshuhudia mimi mwenyewe anabadilika na kuwa mtu tofauti, ulimi wake ulikuwa mrefuuu alafu una rangi nyeusi kama nyoka hivi, mimi sikufichi huyu tumuulie mbali"
"Sawa lakini si unajua Hoteli yangu ile mpya inahitaji Mboga kutoka baharini!, pia hakuna mtu mwenye ujuzi wa kuleta samaki wa kila aina tofauti na huyu mpuuzi".
"Sawa lakini kule baharini, mimi nafahamika, tukimuacha huyu atanitia dosari maana, maji tumeyavulia nguo sharti tuyaoge, tumekosa kumuua kule baharini na sijui alitoka vipi, yupo mzima inatakiwa tumuue kabisa kama watu wa kukufanyia kazi hiyo basi mimi namfahamu kijana mmoja atafanya hiyo kazi"
Wakiwa wanaongea mimi nilibaki kuwasikiliza, mawazo na akili yangu bado havikuweza kuchambua kwa kina nini nifanye.
Hapo ndipo Manyota alikuja akiwa na lile begi kama Sanduku, kwa mbali akili ilirudi kulikumbuka Sanduku langu ambalo Salha aliniambia Mzoa taka kabeba na kuondoka nayo, nilikumbuka pia kule kisiwani yule jamaa kaniagiza safari ndefu ya kuvuka Bahari kwenda upande mwingine ambako kuna familia yake na akaniomba nikalipe kisasi chake, hiyo ndio kazi aliyonipa na akanipatia zawadi ya lile sanduku akiniambia litanisaidia mahali popote hasa kiuchumi wangu.
Leo hii nipo mikononi mwa huyu Mshenzi, anaelazimisha uwezekano ambao kwangu ni mgumu. Basi Manyota alinipiga miguu yangu huku akiwa anaelekea kwa Paul.
"Sasa, nataka mumpeleke kwenye kile chumba haraka, baada ya hapo hakikisheni mnamlazimisha kukubaliana na kazi yangu, ila mfungeni Nyororo nzito sawa?"
Aliongea Paul
"Sawa bosi"
Leo rafiki ambao nilijua kuwa watanisaidia ndio haohao wanashirikiana na mbaya kuniumiza, sikuwa na uwezo wa kukataa, waliniburuza mule sakafuni, hakika mwili wangu ulipatwa na maumivu kutokana na vidonda vilivyotokana na mikwaruzo ya pale chini.
"Mnali, unashindwa nini kukubali kufanya kazi na huyu jamaa mambo yako yaende safi?"
Alisema Musa.
"Basi fikiria ukikubali utatuambia, hatukufungi chochote kama anavyotaka Paul, ukipata majawabu tuambie sawa"
Walitoka na ndipo wakaniacha peke yangu. Nilijikaguakagua yale maeneo ambayo niliumia, lakini kile chumba ni kizuri mbele yangu kulikuwa na kabati ambalo lina Kioo, nilinyanyuka, kisha nikajikagua huku nikisema
"Inawezekana vipi nimeathirika namna hii, maana sio binadamu kamili?, je kwa nini nisikubali kabisa kufanya kazi yake si Kuvua samaki tu! Nitakaopata haohao basi, kwanza nina hamu ya kumtafuta mwanangu Asante pamoja na lile Sanduku kwa Salha anipe".
Nilikata shauri kuwa bora hata nikubali ili haya mateso yasije kunifikishia umauti, baada ya kuona kuwa hakuna njia ya kukimbia ndipo nikagonga mlango ili wafungue na niwaeleze nini nimefikilia kuhusu swala hilo.
Walifungua kisha nikawa nawaitikia tu.
"Oy umekubali?"
Manyota aliuliza
Mimi niliitikia kwa kichwa.
"Sasa ulikuwa unazingua nini, sasa Musa nenda kamuite Bosi"
Musa akiwa katoka tulibaki wawili huku nyuma.
"Manyota nakuomba unieleze wapi naweza kumpata mwanangu Asante"
Nilimuuliza
"Mpumbavu!, hapa sipo kushughulikia shida zako za watoto fanya kazi kwanza"
"Lakini Manyota..."
"Manyota niniiiii!...nimekuambia kimya usiniuzi sasa hivi bwanaa"
"Sawa..lakini wewe ni rafiki yangu naomb..."
"Paaaaaaah!..."
Kabla hata sijamaliza nilipokea kofi la shavuni, nilipepesuka mpaka nikadondoka chini, nilihamaki kutaka kumvamia.
"Eheeee! Unataka kupigana si ndio haya twende sasa tuzipange...fala mkubwa wewe, unadhani nipo kama zamani"
Nilitulia tu baada ya kuhisi naweza kuzidiwa hapa, maana Manyota alikuwa amejazia mikono yake na mwili sikujua alikuwa anakula nini maana kawa bausa pamoja na musa.
Paul alikuja na kutukuta tukiwa tunaangaliana kwa macho makavu.
"Ehee! Amekubali kweli?"
"Ndio bosi amekubali"
"Mnali..kweli umekubali?"
"Ndio nimekubali...kuvua samaki"
"Haaa!..haahahaaa!..haaahaaa...teh!..teh!".
Walinicheka sana kwa kweli sijui nilikosea kusema au kwa sababu ya kule kukubali kuona wamenikamata vyema.
"Manyota! kachukue mzigo haraka, sawaa!"
Manyota alifanya haraka na kurudi,
"Sasa kazi inaanza hapa! Unapeleka hili begi, barabara ya saba kule mjini, kuna hotel moja inaitwa #Zanzini_hotel. Manyota mpeleke alafu hakikisha unampa maelekezo sawa".
Nilishangaa kazi gani hiyo ambayo naenda kuifanya na sijajua kama nitafanikiwa hiyo kazi.
Je? Ni kazi gan?
TUKUTANE TOLEO LIJALO




No comments:
Post a Comment